METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, November 11, 2021

MIZENGWE YA SHERIA KWA MWANAHABARI III

 

Adeladius Makwega,Mbagala.

Wanahabari wamekuwa wakizamwa kuwa ni taaluma ya kuwasemea wengine lakini swali ni moja je wanahabari hao wanaweza kweli kuwasemeea wengine? Unapotaka kulijibu swali hii kwanza jiulize, hao wanahabari je wanaweza kujisemea wenyewe?

Ili kuweza kuwasemea wengine jambo moja la kujiuliza je hapo ulipo (kwako) kuna upande wowote ambao unalalamikia jmabo lolote lile? Ni jambo la kuchekesha mtu mwenye ndoa yenye matatizo lukuki akasimama kifua mbele akidai kuwa yeye ni mtatuzo bora wa migogoro ya ndoa za wenzake.

Haiwezekani wenzetu waliosomea cheti cha habari kwa gharama kubwa sana cheti hicho cha habari hakitambuliki popote. Unaposoma cheti cha habari tambua kuwa fedha zilitumika kulipia karo. Unapomuona mtu anaripoti habari kwenye TV hata kama hajasomea kozi za habari kumbuka alitumia gharama na muda kujifunza kupiga picha za video.

Wapo ambao ilipotamkwa hivyo waliamua kwenda kusoma diploma ya habari na hata mara baada ya kumaliza hiyo diploma hata ajira hakuna.

Kwa hiyo ili kuweza kumsemea mwingine kuna wajibu wa wana taaluma hii kujipambanua kwa kuyasemea mambo yote ambayo yanaonekana yanalalamikiwa ndani ya taaluma hii ikiwamo hizo sheria zenye mizengwe.

Kwa siku ya jana saa nane na dakika mbili mchana nilipata ujumbe ambapo ninauweka humu kama ulivyotumwa kwangu kwa mtu mwenye namba hii 0655264003 ambaye sikuangaika wala kujua jina lake.

“Nimesoma makala yako michuzi blog, sikubaliani na ulichokiandika, kwanini leo? Suala hapa si kuwatenga wenye vyeti, muda uliotolewa watu kuongeza kiwango cha elimu tangu 2016 miaka 5 leo utasemaje wanabaguliwa, huo ni uchochezi. Mbona haukusema wahasibu? Mbona hukusema ubaguzi wa wanasheria? Lengo ni kuipa heshima profeshno sio kila anayeshindwa maisha aje huku, BINAFSI SIKUBALIANI NA HOJA YAKO. Ahsante.”

Makala hiyo ambayo ilipandisha katika Blog aliyoitaja ndugu huyu nilishangaa waliiondoa, hilo ni shauri lao wenyewe.

Kwa upande wangu ilipofika saa12.55 jioni nilimjibu ndugu huyu ujumbe huu

“Wakina nani walioshindwa Maisha….Sheria hii ni ya kibaguzi”.

Suala la hoja hii sasa siyo uchochezi wowote ule bali ni haki ya kutoa maoni juu ya sheria yoyote ambapo maoni hayo yanaweza kusaidia sheria hiyo kuboreshwa zaidi au kuondolewa na ndiyo maana hata hukumu ya kifo ipo kisheria lakini maoni mengi yamekuwa yakitolewa dhidi ya hukumu hiii wapo wanaopinga na wapo wanaounga mkono.

Shida ni moja kuwa kuna watu wengi hawaifahamu vizuri taaluma hii, ndugu yangu huyo kumjibu kwa kifupi tu ni jambo la kichekesho sana kulinganisha taaluma zingine na uwanahabari.

Tangu uhuru mwaka 1961 vyombo vya habari vilikuwa ni vya kuokoteza na vyote vilikuwa vya umma. Taaluma zingine zote zilikuwa na watu wanaofanya kazi kwenye taasisi za umma na binafsi kwa mfano shule, hospitali na hata mawakili wa kujitegemea. Vyuo vya habari havikuwapo na wala redio na magazeti binafsi yalikuwa adimu.

Waliokuwepo ni RTD pekee na ndiyo maana wakati wakuanzishwa vyombo binafsi waliwachukua watangazaji na mafundi wote kutoka RTD na waandishi walikuwa magazeti ya chama na serikali tu kwenda ITV na Redio One.

Pale RTD ukiingia TBC-Broadcasting House-Tazara pale ilipokuwa makao makuu ya RTD wanachumba maalumu chenye ubao ambacho kilikuwa kinatumika kama darasa mara baada ya watu walioajiriwa katika tasnia hii hapo walikuwa wakifundishwa mafunzo kazini. Mathalani watayarishaiji wengi wa vipindi vya RTD walikuwa ni walimu mfano mzuri ni marehemu Ben Kiko na marehemu Benedict Komba.

Ukiwa pale RTD ndipo unafundishwa namna kazi hiyo inavyotakiwa kufanywa unatambua kuwa sasa haupo darasani kama mwalimu bali unapotangaza unatangazia umma wa watu zaidi ya 40 ya darasa moja na hawa walimu waliweza kufanya vizuri sana katika kutayarisha vipindi vya redio.

Mfano mwingine hata huyo Benjamin Mkapa hakuwa mwanahabari wa kusomea shuleni kwani alisoma Shahada ya Kwanza ya Kiingereza na Shahada ya Uzamili ni Mahusiano ya Kimataifa. Mara baada ya kuajiriwa serikalini na kuwa na mahitaji ya Mtanzania kusimamia magazeti ya serikali alipelekwa Uingereza kama secondment na kujifunza namna kazi hiyo inavyofanyika ndipo aliporudi akawa mhariri msimamizi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, na pia machapisho ya magazeti ya Daily News na Sunday News na baadaye akawa mkurugenzi wa SHIHATA.

Kwa hiyo kama tunataka kutengeneza kinyago kizuri na kiweze kuuzwa na kupendwa lazima tuwape nafasi watu wenye vipaji kufanya kazi hii na ukiwapa nafasi watu hao wenye vipaji hata hizo propaganda unaweza kuzifanya vizuri

Je tunaweza kuwaondoa watu wenye mvuto na ushawishi magic tourch/maginetic tourch ili kuwapa nafasi watu wasio na sifa hizo. Kweli kuwapa nafasi watu wa namna hii imewezekana lakini wamekuwa wakishindwa kufanya lolote lile.

Mwaka 2008/2009 Dastan Mhando(Tido Mhando) akiwa mkurugenzi wa TBC aliweza kuileza Kamati ya Bunge inayosimamia Shirika la Utangazaji Tanzania namna atakavyoweza kuliboresha shirika hili la umma, miongoni mwa mambo aliyoyataja katika andiko lake Tido Mhando alisema kuwa atajitahidi kuajiri vijana wa Kitanzania wenye sifa na vipaji ili kuweza kuliinua shirika hilo na kuwa na uwezo wa kujitegemea.

Kwa wale wanaokumbuka kipindi hiko TBC ikiajiri vijana wengine wenye sifa kutoka vyombo mbalimbali ambao wengi walitoka katika TV, magazeti na redio binafsi. Vijana hawa waliweza kwenda kuongeza nguvu katika shirika hilo. Nakukumbusha tu majina kama Baruani Mhuuza, Stela Setumbi, Jamali Hashimu, Philipo Cyprian na wengine wengi walijiunga na Shirika la Utangazaji Tanzania na aliweza kuuaminisha umma kuwa shirika hilo likawa nambari moja Tanzania. Swali ni je TBC bado nambari moja Tanzania? Najua msomaji wangu jibu unalo.

Nakutolea mfano mmoja wa ndani kidogo juu ya TBC INTERNATIONAL hii ni redio ya TBC kama ilivyo TBC Taifa na TBC FM ambayo kwa mawazo mema ya Tido Mhando alitaka iwe TBC Internationall kama zilivyo redio zingine za kimataifa. Kuliweka jambo hilo vizuri mzee huyu alijiri vijana kadhaa wenye vipaji na kwa faida ya msomaji nawataja vijana hawa ambao karibu wote sasa wapo katika taasisi za kimataifa wakifanya kazi.

Mkuu wa Idhaa hiii alikuwa ni Taji Liundi amesomea Mahusiano ya Kimataifa, Steven Mhando alisomea Mahusiano ya Kimataifa, Rahima Kipozi amesomea Sanaa ya Maonesho(bado yupo TBC), Masero Nyirabu alisomea Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano naye Donard Caroli yeye alisomea Masoko.

Kwa mchanganyiko huo TBC International ya wakati huo ilikuwa ikifanya kazi nzuri na hata matangazo yalikuwa yakisikika huku wakiwa na wasikilizaji wengi na makampuni ya biashara yaliwapa matangazo. Kwa vipaji hivyo redio hii iliweza kufanya vizuri kwa kutumia vipaji hivyo vya Watanzania ipasavyo.

Swali ni je leo hii TBC International inafanya vizuri? Pengine hata ukimuuliza mtu ataje frequance zake leo hii ni jambo gumu au walau kumtaja hata mtangazaji mmoja wa redio hii ya umma, jibu litakuwa gumu kwa muulizaji hata kama nikipewa mji.

Kwa leo naweka kalamu yangu chini nikisema kuwa wanahabari wenye cheti na hata wale wenye vipaji/talanta wapewe nafasi kuiboresha tasnia hii.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com