METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, October 23, 2021

MKOA WA MWANZA WAZINDUA KAMPENI YA USAFI WA MAZINGIRA


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi



Naibu Meya wa Jiji la Mwanza na Diwani wa Kata ya Pamba Mhe. Lodrick Ngowi


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza aliyeinama mwenye kofia nyeusi

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana alieshika Toroli mwenye kofia nyeupe

Mkuu wa Mkoa Wa Mwanza akipanda mti 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel amewaongoza wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wakiwemo viongozi mbalimbali wa Mkoa katika Uzinduzi wa kampeni endelevu ya usafi wa Mazingira ambayo imezinduliwa rasmi Oktoba 23, 2021 ikihusisha mitaa mbalimbali iliyopo katikati ya Jiji hilo.

Akiwa ameambatana na Mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Katibu tawala wa Wilaya, Naibu Mayor wa Jiji,  kamati ya ulinzi na Usalama ya mkoa, wakuu wa idara mbalimbali,  viongozi wa vyama mbalimbali na wananchi Mkuu wa Mkoa alizindua Kampeni hiyo kwa kupanda miti na kufanya usafi katika maeneo yanayozunguka Jiji hilo likiwemo eneo la Makoroboi.

Akizungumza na wananchi waliofika katika hafla hiyo ya uzinduzi Mkuu wa Mkoa amesema Kampeni hii itakuwa endelevu kwa lengo la kuirejesha Mwanza katika nafasi yake ya Kwanza kwa Majiji Masafi Tanzania katika nafasi ambayo ilikuwa ikiiongoza kwa miaka kadhaa huko nyuma.

“Kampeni yetu hii ni endelevu na tutaendelea kutoa elimu kwenye Halmashauri zetu zote kwa muda wa miezi miwili, kujenga uelewa wa pamoja, najua kwamba Kuna sheria na kanuni za kusimamia mazingira lakini tuweke kampeni kubwa kwenye elimu, mwisho tutafikia malengo kwa haraka kwa upande wa mazingira.” Amesema

Amesema watu wakipata elimu kuhusu faida za mazingira, faida za upandaji miti watahamasika na kuona faida kwani kwenye miti tunapata matunda tunaboresha afya zetu na kwa Mkoa Mwanza bado kuna maeneo mengi ambayo yanaweza kutumika  kwa ajili ya kupanda miti ya mbao ambayo ikiuzwa faida yake ni kubwa kwa uchumi wa Taifa.

Akizungumzia zoezi la kuwahamisha wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) Mkuu wa Mkoa ameutaka uongozi wa Halmashauri kuhakikisha mazingira ya maeneo waliyopelekwa yanakuwa rafiki, kuwepo kwa miundombinu yote zikiwemo barabara, huduma ya maji na umeme.

“Nimetembea na kuona kazi inayoendelea napenda kukupongeza Mkuu wa Wilaya lakini nitoe maelekezo muanze kutenga bajeti kwa kila Mwaka kuhakikisha wafanyabiashara wa Mwanza maeneo yao yanaimarishwa ili yaanze kuwa na hadhi wakati wa jua  waweze kufanya shughuli zao bila usumbufu wowote.”Amesema

Ameongeza kuwa baada ya wafanyabiashara kuhamia katika maeneo yao iwepo kamati ya ufatiliaji na kupokea malalamiko madogomadogo  na kuyapatia ufumbuzi ikiwemo kuwepo kwa vituo vya magari vipya  katika maeneo ya biashara ili kupeleka wateja.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi Akitoa salamu za Wilaya amesema Miradi yote ya kimkakati na miradi yote inayoendeshwa kupitia vyanzo vya ndani ikiwemo mradi wa ujenzi wa meli kubwa inayogharimu bilioni 89, ujenzi wa soko la kisasa unaogharimu kiasi cha bilioni 15 na stendi ya mabasi Nyegezi inayogharimu kiasi cha bilioni 20 na miradi mingine yote inaendelea vizuri.

Kuhusu zoezi la kuwapanga wafanyabiashara ndogondogo(Machinga) amemueleza Mkuu wa Mkoa kwamba limefanikiwa kwa 89% kwani maeneo 17 ya masoko yamepatikana na tayari machinga wameshapangwa na wanaendelea na shughuli zao.

“Mkuu wa Mkoa kazi tuliyoanza nayo ilikuwa ni kuwatambua na kutambua maeneo ya kuwapeleka na ninavyokujulisha maeneo tuliyotambua kwenye masoko na maeneo ya kuwapeleka tumepata 17 na hapa mjini tuna eneo linaitwa Mchafukoga tumepanga Machinga na wafanyabiashara ndogo ndogo 2000, Buhongwa 3800 na Nyegezi 1500 mpaka sasa zoezi linaendelea na kwenye masoko ambayo yalikuwa wazi tumepeleka machinga.”

Amesema Masoko mengi yalikuwa yamebaki wazi mfano Soko la Mirongo wamepeleka wafanyabiashara ndogondogo 580 wakiwemo akina mama, Mbugani 670 huku zoezi likiendelea kwa Masoko mengine likiwemo soko la Mkuyuni, Bugarika, Igogo, Mabatini na Igoma.

Sambamba  na hilo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha  kwa Mkoa wa Mwanza kwa  ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika wilaya zilizopo Mkoani humo ikiwemo Wilaya ya Nyamagana kukabiliana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Akiongea katika uzinduzi huo Naibu Meya Wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Mhe. Lodrick Ngowi amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa wazo hilo la kuwa na kampeni maalumu ya usafi, amemuahidi mkuu wa mkoa na kusema kuwa atakuwa nae bega kwa bega katika kuhakikisha usafi unaendelezwa katika mitaa yote ya Jiji la Mwanza ikiwemo kata yake ya Pamba.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com