Mkuu wa Mkoa wa Mwanza
Mhandisi Robert Gabriel amewaongoza wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wakiwemo
viongozi mbalimbali wa Mkoa katika Uzinduzi wa kampeni endelevu ya usafi wa
Mazingira ambayo imezinduliwa rasmi Oktoba 23, 2021 ikihusisha mitaa mbalimbali
iliyopo katikati ya Jiji hilo.
Akiwa ameambatana na
Mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Katibu tawala wa Wilaya, Naibu Mayor wa Jiji, kamati ya ulinzi na Usalama ya mkoa, wakuu wa
idara mbalimbali, viongozi wa vyama
mbalimbali na wananchi Mkuu wa Mkoa alizindua Kampeni hiyo kwa kupanda miti na
kufanya usafi katika maeneo yanayozunguka Jiji hilo likiwemo eneo la Makoroboi.
Akizungumza na wananchi
waliofika katika hafla hiyo ya uzinduzi Mkuu wa Mkoa amesema Kampeni hii
itakuwa endelevu kwa lengo la kuirejesha Mwanza katika nafasi yake ya Kwanza
kwa Majiji Masafi Tanzania katika nafasi ambayo ilikuwa ikiiongoza kwa miaka
kadhaa huko nyuma.
“Kampeni yetu hii ni
endelevu na tutaendelea kutoa elimu kwenye Halmashauri zetu zote kwa muda wa
miezi miwili, kujenga uelewa wa pamoja, najua kwamba Kuna sheria na kanuni za
kusimamia mazingira lakini tuweke kampeni kubwa kwenye elimu, mwisho tutafikia
malengo kwa haraka kwa upande wa mazingira.” Amesema
Amesema watu wakipata
elimu kuhusu faida za mazingira, faida za upandaji miti watahamasika na kuona
faida kwani kwenye miti tunapata matunda tunaboresha afya zetu na kwa Mkoa
Mwanza bado kuna maeneo mengi ambayo yanaweza kutumika kwa ajili ya kupanda miti ya mbao ambayo
ikiuzwa faida yake ni kubwa kwa uchumi wa Taifa.
Akizungumzia zoezi la
kuwahamisha wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) Mkuu wa Mkoa ameutaka uongozi
wa Halmashauri kuhakikisha mazingira ya maeneo waliyopelekwa yanakuwa rafiki,
kuwepo kwa miundombinu yote zikiwemo barabara, huduma ya maji na umeme.
“Nimetembea na kuona
kazi inayoendelea napenda kukupongeza Mkuu wa Wilaya lakini nitoe maelekezo
muanze kutenga bajeti kwa kila Mwaka kuhakikisha wafanyabiashara wa Mwanza
maeneo yao yanaimarishwa ili yaanze kuwa na hadhi wakati wa jua waweze kufanya shughuli zao bila usumbufu wowote.”Amesema
Ameongeza kuwa baada ya
wafanyabiashara kuhamia katika maeneo yao iwepo kamati ya ufatiliaji na kupokea
malalamiko madogomadogo na kuyapatia
ufumbuzi ikiwemo kuwepo kwa vituo vya magari vipya katika maeneo ya biashara ili kupeleka wateja.
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi Akitoa salamu za Wilaya amesema Miradi
yote ya kimkakati na miradi yote inayoendeshwa kupitia vyanzo vya ndani ikiwemo
mradi wa ujenzi wa meli kubwa inayogharimu bilioni 89, ujenzi wa soko la kisasa
unaogharimu kiasi cha bilioni 15 na stendi ya mabasi Nyegezi inayogharimu kiasi
cha bilioni 20 na miradi mingine yote inaendelea vizuri.
Kuhusu zoezi la
kuwapanga wafanyabiashara ndogondogo(Machinga) amemueleza Mkuu wa Mkoa kwamba limefanikiwa
kwa 89% kwani maeneo 17 ya masoko yamepatikana na tayari machinga wameshapangwa
na wanaendelea na shughuli zao.
“Mkuu wa Mkoa kazi
tuliyoanza nayo ilikuwa ni kuwatambua na kutambua maeneo ya kuwapeleka na
ninavyokujulisha maeneo tuliyotambua kwenye masoko na maeneo ya kuwapeleka
tumepata 17 na hapa mjini tuna eneo linaitwa Mchafukoga tumepanga Machinga na
wafanyabiashara ndogo ndogo 2000, Buhongwa 3800 na Nyegezi 1500 mpaka sasa zoezi
linaendelea na kwenye masoko ambayo yalikuwa wazi tumepeleka machinga.”
Amesema Masoko mengi
yalikuwa yamebaki wazi mfano Soko la Mirongo wamepeleka wafanyabiashara
ndogondogo 580 wakiwemo akina mama, Mbugani 670 huku zoezi likiendelea kwa
Masoko mengine likiwemo soko la Mkuyuni, Bugarika, Igogo, Mabatini na Igoma.
Sambamba na hilo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika
wilaya zilizopo Mkoani humo ikiwemo Wilaya ya Nyamagana kukabiliana na uhaba wa
vyumba vya madarasa.
Akiongea katika
uzinduzi huo Naibu Meya Wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Mhe. Lodrick Ngowi
amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa wazo hilo la kuwa na kampeni maalumu ya usafi, amemuahidi
mkuu wa mkoa na kusema kuwa atakuwa nae bega kwa bega katika kuhakikisha usafi
unaendelezwa katika mitaa yote ya Jiji la Mwanza ikiwemo kata yake ya Pamba.
No comments:
Post a Comment