METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, September 20, 2021

SERIKALI ITAENDELEA KUWALINDA WENYE VIWANDA-MAJALIWA

Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kutembelea Kiwanda cha Kahawa Ngara Coffee akiwa katika ziara ya Mkoa wa Kagera, Septemba 19, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwalinda wenye viwanda nchini na haitavumilia kuona wawekezaji wakinyanyaswa.

Pia, Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Samia amewaagiza wasaidizi wake[m1]  wasimamie mwenendo mzima wa masoko ya mazao mbalimbali nchini likiwemo na zao la Kahawa ili kuhakikisha wakulima wananufaika na kazi wanayoifanya.

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumapili, Septemba 19, 2021) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua kiwanda cha kuchakata kahawa cha Ngara Coffee kilichopo wilayani Ngara, Kagera.

Amesema Rais Mheshimiwa Samia ameendelea kuwahamasisha wawekezaji waje nchini na wawekeze katika sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda ambavyo vitawawezesha wakulima kupata masoko ya uhakika ya mazao yao.

Akizungumzia kuhusu kiwanda hicho, Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi wa Ngara watumie fursa ya uwepo wa kiwanda cha Ngara Coffee kwa kuongeza ukubwa wa mashamba ya kahawa kwa kuwa wana soko la uhakika.

Waziri Mkuu amesema uzalishaji wa kahawa kwa wilaya ya Ngara ni tani 1,000 kwa mwaka kiasi ambacho ni kidogo ukilinganisha na uwezo wa kiwanda hicho, hivyo amewashauri wakulima waongeza uzalishali ili kukiwezesha kiwanda hicho kupata malighafi ya kutosha.

Kadhalika, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali, Charles Mbuge aunde timu maalumu itakayofanya mapitio ya mfumo mzima wa uuzaji wa zao la kahawa wilayani Ngara.

Ametoa agizo hilo baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa uuzaji wa zao hilo unaosimamiwa na Chama cha Msingi cha Wakulima wa Kahawa Ngara ambacho kimekuwa kikiwakata wakulima makato mengi na kuwapunguzia tija.

“Makato mengi mnayowakata wakulima hayana msingi kwa mkulima, mfano wa makato hayo ambayo yanakatwa katika kila kilo moja ya kahawa ya mkulima ni pamoja na riba ya mkopo unaokopwa na chama hicho (36%), usafirishaji (34%), gharama za ukoboaji (shilingi 112), gharama ya usafirishaji nje (1%).”  

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda cha Ngara Coffee Abdallah Seif ameiomba Serikali iwape kibali kitakachowaruhusu kununua kahawa kwa wakulima kwa bei nzuri tofauti na ilivyo sasa.

“Mfano bei ya kahawa inayotumika kwa msimu huu hapa Ngara ni shilingi 1,300 kwa kilo na sisi Ngara Coffee hatuwezi kununua kahawa chini ya shilingi 1,500. Huko nyuma tumewahi kununua kahawa kati ya shilingi 1,200 hadi 1,700.”

Pia, Mkurugenzi huyo ameiomba Serikali isaidie kuchochea mwamko wa wananchi kulima zao la kahawa kwa wingi zaidi kwa sababu uzalishaji uliopo sasa kiwandani kwao haufikii hata robo ya uwezo wa kiwanda.

Amesema kiwanda cha Ngara Coffee kinauwezo wa kukoboa tani 28,000 sambamba na kukaanga, kusaga na kufungasha tani 62,000 kwa mwaka. Kiwanda hicho kilianzishwa 2010 kwa gharama ya shilingi bilioni tatu.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com