Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Kambi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kuwepo kuendelea kuwepo kwa ugonjwa wa Homa ya Dengue nchini.
Baadhi ya waandishi wa habari waliojitokeza kusikiliza tamko la kuhusu kuwepo kwa ugonjwa wa Homa ya Dengue nchini wakati likitolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Kambi Jijini Dodoma.
NA WAJMW-DODOMA
Serikali kupitia Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezidi kutoa tahadhari ya
kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya Dengue nchini hususani katika Jiji la Dar Es
Salaam na Tanga.
Tahadhari hiyo imetolewa leo na
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Kambi wakati akizungumza na waandishi wa
habari katika ofisi za wizara hiyo zilizoko jijini Dodoma.
Prof. kambi amesema hadi kufikia
tarehe 6 Mei 2019, kati ya watu waliopimwa, wagonjwa 1237 wamethibitishwa kuwa
na virusi au walikwishapata ugonjwa wa Dengue na kati yao 1150 ni kutoka Dar Es
Salaam, 86 ni kutoka Tanga na mtu mmoja kutoka Singida.
Aidha, Prof Kambi amesema takwimu za
ugonjwa wa Dengue kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2019 zinaonesha mwenendo
wa ugonjwa huu kuwa na idadi ya wagonjwa 1237, vifo vya watu wawili na kuongeza
kuwa waliofariki walikua na maradhi mengine.
Pamoja na hayo Mganga Mkuu huyo wa
Serikali amelipongeza jiji la Dar Es Salaam kwa kuanza kunyunyizia dawa
viuadudu (Biolarvicides) kwa ajili ya kuangamiza mazalia ya mbu ili kupambana
na ugonjwa huu.
Vile vile amesema Wizara inaelekeza
Mikoa na Halmashauri zote nchini kuendelea kuchukua hatua katika kudhibiti
ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kufukia madimbwi ya maji, kunyunyizia dawa ya
kuua viluwiluwi, kuondoa vitu vinavyosababisha mazalia ya mbu, kufyeka vichaka,
kufunika mashimo ya maji taka kwa mifuniko pamoja kusafisha gata za paa la
nyumba na kutoruhusu maji kusimama.
Prof. Kambi amesema Wizara kwa
kushirikiana na Mikoa na Halmashauri zote nchini itaendelea kuchukua hatua
mbalimbali za kudhibiti ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kuendelea kuangamiza
mazalia ya mbu na viluwiluwi, kuweka mpango wa dharura wa miezi sita kuanzia
Mei mpaka Oktoba ili kukabiliana na ugonjwa huu. Pia amesema Serikali imenunua
Vitendanishi vyenye uwezo wa kupima wagonjwa 1870 na vimesambazwa kwenye vituo
maalum vya ufuatiliaji wa ugonjwa huu nchini kote.
Mwisho Prof. Kambi amewataka wananchi
kuendelea kuchukua hatua za kujikinga kuumwa na mbu kwa kuvaa nguo ndefu,
kutumia vyandarua vyenye viuatilifu, kutumia dawa za kufukuza mbu na kuweka
nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi ili kukabiliana na
ugonjwa huu.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment