Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Kafulila akizungumza na Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Songwe Mhandisi Fidelis Cosmas katika eneo la ujenzi wa Nyumba ya Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala Mkoa, Kafulila amevunja Mkataba na TBA wa ujenzi wa Nyumba hizo kutokana na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo.
Eneo likionyesha hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Nyumba ya Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala Mkoa ambapo kwa muda wa miezi miwili tangu wakabidhiwe eneo la ujenzi TBA wamefikia hatua hiyo huku wakibakiwa na miezi mingine miwili ya kukamilisha ujenzi huo, hali iliyopelekea Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Kafulila kuvunja mkataba na TBA kutokana na kutoridhishwa na kasi hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Kafulila amesitisha Mkataba wa ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Mkoa na ya Katibu Tawala Mkoa uliokuwa kati ya yake na Shirika la Ujenzi la Taifa (TBA), kutokana na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo.
Kafulila akiambatana na wakuu wa Sehemu wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe amefikia uamuzi huo jana mara baada ya kutembelea eneo la ujenzi wa nyumba hizo na kukuta hatua ya ujenzi iliyofikiwa hairidhishi.
Kafulila amesema kasi ya ujenzi wa nyumba hizo inatia mashaka kutokana na kuwa kazi iliyokwisha fanyika kwa muda wa siku sitini ni ndogo ukilinganisha kazi na muda uliobakia kufikia tarehe ya makubaliano ya kukamilika ujenzi.
“Kazi iliyobaki kiuhalisia haiwezekani TBA wakaikamilisha kwa muda uliobakia, kwani tuliwakabidhi eneo la ujenzi tarehe 2-2-2019 na tulikubaliana ikifika tarehe 30-06-2019 nyumba hizo mbili ziwe zimekamilika lakini kwa kipindi cha miezi miwili hakuna kitu wamefanya na kuna dalili zote za kutokamilisha kwa muda”, ameeleza Kafulila.
Ameongeza kuwa TBA wamekuwa na tabia ya kutekeleza miradi ya ujenzi kwa kasi ndogo mkoani Songwe na hivyo kusababisha fedha kurudishwa hazina kuu kutokana na kutozitumia kwa muda unaotakiwa yaani ndani ya mwaka wa fedha wa serikali ambapo fedha hizo zinakuwa zimetolewa.
“TBA mmekuwa na kawaida ya kutekeleza miradi yetu kwa kasi ndogo na hivyo kusababisha fedha kurudishwa hazina, mfano ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wamesababisha takribani Bilioni 3.8 zirudishwe na sasa tunahangaika kuziomba tena, uzembe huu tunaona unelekea kujirudia tena na sisi kama Mkoa hatuko tayari kila mara tunapewa fedha za ujenzi halafu zinarudishwa kwa uzembe wa TBA”, ameongeza Kafulila.
Amesema kuwa Mkoa hauna matatizo na Wizara ya Ujenzi wala shirika hilo la TBA ila lazima hatua za kusitisha mkataba huo zichuliwe ili kunusuru fedha hizo kurudishwa hazina kuu kutokana na kuchelewa kuzitumia ndani yam waka wa fedha wa serikali pia ili nyumba hizo zikamilike kwa muda na kuwezesha makazi ya viongozi.
“Naomba ifahamike mimi na mkoa kwa ujumla hatuna matatizo na Wizara ya Ujenzi pamoja na TBA lakini tukilifumbia macho hili hata sisi tutapimwa utimamu wa akili zetu, nimetembelea eneo la ujenzi zaidi ya mara nne lakini hakuna maendeleo yoyote, kiuhalisia kwa kasi hii TBA Mtatuangusha, sisi tunapenda kufanya kazi kwa kuendana na kasi ya Rais wetu”, amesisitiza Kafulila.
Amesema gharama ya Ujenzi wa Nyumba ya Mkuu wa Mkoa ni shilingi milioni 499.9 na tayari TBA walipewa malipo ya awali ya shilingi milioni 74.9 huku nyumba ya Katibu Tawala Mkoa ikiwa na gharama ya shilingi milioni 499.7 na malipo ya awali yaliyotolewa ni shilingi milioni 74.9
Imeelezwa kuwa TBA hawajawahi kuwasilisha taarifa ya kazi iliyokwisha fanyika lakini pia hawajaomba fedha zozote tangu walipwe malipo ya awali huku muda uliobaki ukionyesha kuwa hataweza kukamilisha kazi iliyobaki.
0 comments:
Post a Comment