Asema wasitumie nafasi zao
kunyanyasa wengine, akemea ubaguzi
Ataka wajitoe kusaidia wasionacho
kama njia ya kumuenzi Dk. Mengi
MKUU wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Mkuu Dk. Ferdinand Shoo amewaonya viongozi wa
Tanzania na kuwataka watumie nafasi zao kuwasaidia wengine hasa wale wenye uhitaji.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Mei
9, 2019) wakati akitoa mahubiri kwenye ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti
Mtendaji wa kampuni za IPP, Dkt. Reginald Mengi iliyofanyika kwenye kanisa la
KKKT, Usharika wa Moshi mjini.
Amesema kuna watu wakipata vyeo ama
utajiri kidogo tu, wanatumia nafasi zao kunyanyasa wengine na akaonya
Watanzania wasie wepesi wa kuhukumu, kunyanyasa wengine au kubagua wengine.
Katika mahubiri yake, Dk. Shoo
amesema kama kuna dhambi ambayo binadamu anapaswa kuifanyia toba ni ile ya
kubaguana na kama Watanzania wanahitaji Taifa lipokee baraka kutoka kwa Mungu,
ni vema wakaacha kufanya hivyo. Amesema dhambi nyingine inayopaswa kufanyiwa
toba ni ile ya watu wenye nafasi kuwakanyaga wengine.
“Ndugu zangu tukiwa na cheo, tukiwa
matajiri, tukiwa na uwezo tuvitumie kuwasaidia wengine, tuache ubinafsi, tuache
kiburi, tuache kujitutumua hasa kwa viongozi wa umri mdogomdogo. Kuna mahali
mmefika mnajitutumua kama chatu, acheni kabisa. Naomba tuwe unyenyekevu ndugu
zangu.”
“Wale wanaopata utajiri, acheni
kukumbatia mali zenu, toeni na kuwasaidia wenye uhitaji kwani mnapata
satisfaction kwa kufanya hivyo. Huu ni ujumbe kwetu sote na Mungu atusaidie
tulishike hili. Muendelee kuiombea familia na yale mazuri mengi tuliyojifunza
kwake tukayatende tukayatende, tuyaenzi,” amesema.
Akimuelezea Dkt. Mengi, Askofu Mkuu
huyo amesema: “Aliwahi kusema kuwa, mali na utajiri ambao Mungu amempatia siyo
kwa sababu yeye ni bora kuliko wengine, bali alimpa ili awe kama bomba la
kufikisha baraka kwa wengine.”
“Leo mtu anapata vimilioni kadhaa tu
anataka atembee juu ya migongo ya watu, anapata ka-cheo sijui ni diwani, Mkuu
wa Mkoa au wa Wilaya, halafu unaona wenzako si kitu. Tuache na tutubu, acha
kiburi namuomba Mungu atujalie roho hiyo ya unyenyekevu,” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya
Serikali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Dkt. Mengi atakumbukwa kwa
kitendo chake cha kuuchukia umaskini na zaidi kwa kazi mbalimbali ambazo
alishiriki.
“Bila shaka kila mmoja wetu ameguswa
kwa namna ya kipekee na mchango wa Dkt. Mengi. Kiukweli, marehemu Dkt. Mengi,
atakumbukwa kama mwanahabari, mwanaviwanda na mfanyabiashara maarufu ambaye
alitumia elimu, maarifa na utajiri wake kwa ajili ya manufaa ya wote hususan
watu wenye mahitaji maalum,” amesema Waziri Mkuu.
Amewaomba wanafamilia wasimamie
makampuni ambayo Dkt. Mengi aliyaanzisha na kama watakwama wasisite kuomba
msaada serikalini kwani iko pamoja nao.
Akielezea wasifu wa baba yake, mtoto
wa marehemu, Bw. Abdiel mengi alisema siyo rahisi kuyazungumzia yote kwa wakati
mmoja mambo ambayo yamefanywa na Dkt. Mengi bali aliwashukuru waombolezaji
wote, viongozi wa Serikali na wafanyakazi wa makampuni ya IPP kwa upendo wao.
“Mambo yote aliyoyafanya naweza
kumwelezea katika sifa tatu kubwa ambazo ni alikuwa mzalendo, mwenye uthubutu
na mwenye kupenda breakthrough. Alikuwa nafikiria tofauti na wengine. Kwanza
anajiuliza kwa nini nifanye jambo hili, na nifanyeje ilikuwa ni suala la pili,”
alisema.
Dkt. Mengi ambaye alifariki
dunia alfajiri ya Mei 2, mwaka huu akiwa kwenye matibabu huko Dubai, Falme za
Kiarabu, amezikwa katika makaburi ya familia huko Nkuu Sinde - Kisereni,
Machame, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro. Ameacha mke na watoto wanne.
0 comments:
Post a Comment