Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekuwa kiktoa taarifa kwa wananchi mara
kwa mara kuhusiana na mwenendo wa magonjwa ikiwemo magonjwa ya milipuko
(epidemic diseases) nchini na hatua zinazochukuliwa kuzuia na kudhibiti
magonjwa haya.
Magonjwa yanayofuatiliwa kwa
karibu na kutolewa taarifa mara moja pindi yakitokea ni, kumi na nne
(14) ambayo ni pamoja na Kipindupindu, Polio, Kimeta, Kuhara Damu, Homa
ya Uti wa Mgongo, Mafua makali ya ndege, Surua, Pepopunda ya watoto
wachanga, Kichaa cha Mbwa, Ndui, Magonjwa yanayosababishwa na Virusi na
Homa yanayosababisha damu kuvuja (Ebola, Marburg, RVF, Homa ya Dengue,
Chikungunya), Macho mekundu, Tauni, na Homa ya Virusi ya Manjano.
Utoaji wa taarifa za magonjwa
haya zimerahisishwa, ambapo vituo vyote vya kutoa huduma za Afya nchini
kuanzia ngazi ya chini hutoa taarifa hizi kwa kupitia mfumo maalum kwa
njia ya simu (Integrated Disease Surveillance and Response – IDSR). Hii
hupelekea taarifa zote muhimu kuhusu magonjwa kupatikana kwa haraka na
hatua kuchukulia mapema na wizara ili kudhibiti magonjwa haya.
Kwa kipindi cha mwezi Septemba
2019, Wizara imeendelea kufuatilia magonjwa haya na matukio hatarishi
kwa afya, kutoka kwenye mikoa yote nchini. Katika mwezi Septemba,
ugonjwa wa Dengue na Surua tu ndio magonjwa ya milipuko yaliyotokea hapa
nchini.
Kwa Kipindi cha mwezi Septemba
2019, jumla ya wagonjwa 10 walithibishwa kuwa na Homa ya Dengue na
hakukuwa na kifo. Wagonjwa hawa walitolewa taarifa kutoka mikoa 2 ambayo
ni Dar es salaam – wagonjwa 4 (Hospitali ya Taifa Muhimbili – 4) na
Tanga – wagonjwa 6 (Tanga jiji – 6). Ugonjwa huu umeendelea kudhibitiwa
kwa kiasi kikubwa nchini na umeendelea kupungua mwezi hadi mwezi.
Takwimu za miezi mitatu (Julai, Agosti na Septemba, 2019) zimeonyesha
kupungua kwa ugonjwa huu kwa kiasi kikubwa ambapo mwezi Julai 2019
kulikuwa na wagonjwa waliothibishwa 732, mwezi Agosti wagonjwa 92 na
mwezi Septemba wagonjwa – 10. Aidha tangu mlipuko huu uanze mwezi
Januari 2019 hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2019 kumekuwa na jumla
ya wagonjwa waliohisiwa kuwa na Dengue 14,369 na kati yao
waliothibishwa ni 6,785 na vifo 13 (Dar-6259, Tanga-365, Pwani-115,
Morogoro-22, Lindi-8, Arusha-5, Singida-3, Dodoma-3, Ruvuma-2, Kagera-2
na Kilimanjaro-1).
Ili kukabiliana na magonjwa
yaenezwayo na wadudu dhurifu wakiwemo mbu, Wizara ilizindua mpango
mkakati wa kukabiliana na wadudu dhurifu na mbu (National Vector control
strategy 2019 – 2023) tarehe 27 Julai 2019, Dar es Salaam. Uzinduzi huu
uliambatana na uzinduzi wa kitaifa wa zoezi la upuliziaji wa dawa
kupambana na mbu wapevu na unyunyiziaji wa dawa za kuua viluwiluwi wa
mbu waenezao magonjwa kama vile Malaria, Dengue na nk,. Dawa za
kuangamiza wadudu zilinunuliwa pamoja na mashine kubwa (4) za kupulizia
dawa (Fogging Machine) ambazo zilisambazwa katika mikoa iliyoathirika na
ugonjwa wa Dengue yaani Dar es Salaam, Tanga pamoja na Dodoma. Wizara
imeshaagiza mashine nyingine 4 ili kuweka mkakati endelevu wa zoezi
hili.
Mikoa hii pia (Dar es salaam,
Dodoma, Tanga) ilishafanya uzinduzi wa Mkakati wa Kudhibiti Mbu na
Wadudu wadhurifu pamoja na kuendesha zoezi la kuangamiza mbu. Hatua hii
imesaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Dengue nchini kama
inavyoonyeshwa katika takwimu. Aidha, zoezi hili la uzinduzi linaendelea
kufanyika katika Mikoa yote ili kutokomeza magonjwa yaenezwayo na
wadudu hao. Elimu endelevu pia inaendelea kutolewa kwa wananchi juu ya
namna kujikinga na kudhibiti ugonjwa huu
Mwenendo wa Ugonjwa wa Kipindupindu nchini.
Ugonjwa wa Kipindupindu
umedhibitiwa, na kwa sasa HATUNA KABISA mgonjwa wa Kipindupindu nchini.
Mara ya mwisho kupata mgonjwa wa Kipindupindu nchini ilikuwa tarehe 14
mwezi Julai 2019.
Kwa kipindi cha kuanzia tarehe 1
Januari hadi Julai 2019, kulikuwa na jumla ya wagonjwa 424 na vifo 8 vya
ugonjwa wa Kipindupindu. Wizara inaendelea kuchukua hatua za kudhibiti
ugonjwa huu, ikiwa ni pamoja kufuatilia hatua zinazochukuliwa za kuzuia
ugonjwa huu na timu ya Mkoa na Halmashauri ambazo ni pamoja na; Kutoa
elimu ya afya kwa wananchi ya namna kujikinga kupata ugonjwa huu,
Ufuatiliaji wa usafi wa mazingira.
Wizara inakamilisha Mpango
Mkakati wa Kipindupindu wa mwaka 2019 hadi 2023 ambao utekelezaji wake
utajikita katika maeneo yanayotoa wagonjwa mara kwa mara (Hotspot areas)
ambayo ni Dar es Salaam (Halmashauri zote), Ngorongoro (Arusha),
Simanjiro (Manyara), Handeni na Mkinga (Tanga), Kilwa (Lindi), Ulanga
(Morogoro), Mbarali na Chunya (Mbeya), Songwe, Sumbawanga DC (Rukwa),
Mpanda (Katavi), Nyasa (Ruvuma) na Iringa DC (Iringa). Mpango
huu, unalenga kutokomeza Kipindupindu kabisa. Katika mpango huu maeneo
yalijikita ni pamoja na: Uratibu na ushirikishwaji wa wadau katika ngazi
zote katika kudhibiti ugonjwa, kuimarisha ufuatiliaji na upimaji wa
wagonjwa, Kuimarisha utoaji wa matibabu sahihi na mapema kwa wagonjwa,
ushirikishwaji wa jamii katika kudhibiti na ugonjwa, kuweka mazingira ya
kuwepo kwa maji safi na salama na masuala ya matumizi ya vyoo na
vilevile kuimarisha utoaji wa chanjo kwa maeneo sugu na vigezo
vitakavyotumika.
Wizara imeendelea pia na
utekelezaji wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira yenye kaulimbiu
isemayo “USICHUKULIE POA NYUMBA NI CHOO”, ikiwa ni moja ya mikakati ya
kutokomeza Kipindupindu na magonjwa ya kuhara. Kampeni hii ambayo ipo
katika awamu ya pili, ilizinduliwa rasmi Disemba, 2017 na Mhe. Samia
Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uanzishwaji wa Kampeni hii ni sehemu ya jitihada za serikali kujielekeza
katika kutekeleza lengo namba 6.2 la Malengo ya Maendeleo Endelevu
(Sustainable Development Goals) pamoja na lengo namba 3 linahusu
kuboresha Afya. Katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji
(2016-2019), jumla ya kaya 2,464,225 zimejenga au kuboresha vyoo kufikia
kiwango cha ubora kati ya lengo la kaya 3,360,000. Hii ni sawa na
asilimia 73.3. Kwa upande wa taasisi, shule 1,670 kati ya lengo la shule
2,520 zimejenga vyoo bora kwa kuzingatia uwiano.
Kwa ujumla kaya zenye vyoo bora
katika ngazi ya kaya zimeongezeka kutoka asilimia 46 Julai, 2016 hadi
asilimia 57.2 Juni, 2019, na kaya zisizokuwa na vyoo zimepungua kutoka
asilimia 7.5 hadi asilimia 2.5 katika kipindi hicho.
Mwenendo wa Ugonjwa wa Surua nchni.
Katika kipindi cha mwezi Septemba
2019, mlipuko wa ugonjwa Surua ulitokea katika kitongoji cha Kashasha,
Kakoma na kijiji cha Kibare wilayani Kyerwa mkoa wa Kagera. Jumla ya
wagonjwa 17 walipatikana na ugonjwa wa surua ambapo kati yao; wagonjwa
saba walithibitishwa kwa kipimo cha maabara. Mgonjwa wa mwisho kupatwa
na dalili za surua katika eneo la Kibare ilikuwa tarehe 14/09/2019. Kwa
takribani wiki mbili sasa hakuna mgonjwa mwingine aliyepatikana.
Wagonjwa wote wamepona na elimu ya jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa
surua imetolewa na pia kuhamasisha kuwaleta watoto katika kampeni ya
kitaifa shirikishi ya chanjo ya surua na rubella, watoto wote chini ya
miaka mitano.
Katika ufuatiliaji wa ugonjwa
surua nchini wagonjwa wenye dalili za homa na vipele hufuatiliwa na
kuchukuliwa sampuli kupima kubaini kama wana ugonjwa wa surua. Kwa
kipindi cha mwezi Septemba 2019, jumla ya sampuli 222 za wagonjwa
waliokuwa na dalili ya homa na vipele zilipokelewa na kufangashwa na
kuwasishwa maabara ya Taifa kutoka kwenye mikoa 23 ya Tanzania bara.
Mwenendo wa Ugonjwa wa Polio nchini.
Hadi sasa hakuna mgonjwa wa Polio
aliyethibika hapa nchini tangu mwaka 1996. Hii inatokana na jitihada
kubwa za Serikali katika kutoa chanjo na kufuatilia dalili za wagonjwa
wenye ugonjwa huu na pia kwa kununua chanjo za Polio ambazo zimeweza
kuwafikia watoto wote chini ya miaka mitano (5) kwa zaidi ya asilimia
90%. Katika ufuatiliaji wa ugonjwa huu, wagonjwa wote wa dalili za
kupooza ghafla (Acute Flaccid Paralysis – AFP) hufuatiliwa na sampuli
kuchukuliwa na kupimwa kujua kama wana ugonjwa wa Polio. Kwa mwezi
Septemba 2019, jumla ya sampuli 63 za AFP 63 zilifungashwa na kupelekwa
maabara kwa ajili ya vipimo. Aidha katika ufuatiliaji wa virusi vya
polio katika mazingira, ambapo kirusi hiki pia hukaa kwa muda nao
unaendelea na hadi sasa kirusi hiki kimeonekana kuwa hakipo katika
mazingira yetu. Ufuatiliaji wa mara kwa mara unaendelea. .
Katika mpango wa kutokomeza vifo
na ulemavu kutokana na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. Wizara ya Afya
kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo na kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais –
TAMISEMI, itaendesha kampeni ya chanjo dhidi ya Magonjwa ya Surua,
Rubella na Polio mnamo tarehe 17 hadi 21 mwezi Octoba 2019. Kampeni hii
itafanyika nchi nzima kwa watoto wote lengwa walio na umri wa chini ya
miaka mitano. Nawasihi wananchi wote washiriki ili Serikali ifikie lengo
la kampeni hii.
Mwenendo wa Ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuripotiwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
Wizara imekuwa ikifuatilia kwa
karibu mwenendo wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuripotiwa nchini DRC na
kuchukua hatua za tahadhari za kuzuia na kukabiliana na ugonjwa huu
hususani kwa kuwa kwa sasa ugonjwa huu unaendelea kusambaa na kuingia
kusini mwa DRC. Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia tarehe 30
Septemba 2019, jumla ya wagonjwa 3,194 walithibitishwa kuwa na ugonjwa
huu, na vifo 2133 (CFR 66.8%). Kutokana na ukaribu wa nchi hii na
Tanzania, Wizara imeendelea kuchukua hatua za utayari kuzuia na
kujiandaa kukabiliana na ugonjwa huu
Hatua za utayari na kujiandaa
kukabiliana na ugonjwa huu nchini ni pamoja na kuimarisha uchunguzi wa
Wasafiri kwenye mipaka yetu yote. Kuimarisha utambuzi katika ngazi ya
vituo vya kutolea huduma za Afya; Kuhakikisha uwepo vya Vifaa Kinga
hususani kwa watumishi wa Afya; Kuimarisha utambuzi wa Ugonjwa na
kuendelea kutoa Elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga ugonjwa
huu. Wizara inayo namba ambayo hutumika bila malipo na wananchi kutoa
taarifa za kuwepo kwa tetesi za ugonjwa huu ambazo ni 0800110124 au
0800110125. Kuanzia 2018 hadi sasa, tetesi 28 za wagonjwa wanaohisiwa
kuwa na Ebola (washukiwa 2 kwa mwezi Septemba), zimekwisha kutolewa
taarifa na uchunguzi kufanyika kwa ukamilifu na kuthibitisha wagonjwa
hawa hawakuwa na Ebola, na taarifa zake kupelekwa pia katika Shirika la
Afya Duniani. Aidha Wizara imeendelea kufanya pia mazoezi ya kujinoa na
kijipima utayari wa kukabiliana na ugonjwa huu (Simulation Exercises)
katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro na Arusha.
NAPENDA KUSISITIZA KUWA HADI SASA
HAKUNA MGONJWA ALIYETHIBITISHWA KUWA NA UGONJWA WA EBOLA HAPA NCHINI.
WIZARA INAWASIHI WANANCHI KUTOKUWA NA HOFU NA KUPUUZA TAARIFA
ZINAZOTOLEWA KILA KUKICHA NA BAADHI YA VYOMBO VYA HABARI NA MITANDAO YA
KIJAMII.
Katika kudhibiti ugonjwa wa Ebola
na magonjwa mengine ya milipuko yenye madhara makubwa duniani, nchi
yetu kila wakati imekuwa mstari wa mbele ikiwa ni pamoja na kusimamia
kwa ukamilifu na kutekeleza Kanuni za Kimataifa za Afya (International
Health Regulation – IHR 2005). Mnamo mwaka 2016, Tanzania ilikuwa nchi
ya kwanza duniani kuweza kukubali bila kipingamizi kuleta wataalam
duniani kuja kupima utayari wa nchi yetu katika kukabiliana na magonjwa
haya hatarishi (Joint external evaluation). Hatua hii kubwa na ya uwazi
ilifanywa kwa mara ya kwanza Duniani, kama moja ya njia ya kuhakikisha
nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani, wanatekeleza Kanuni hizi za
Kimataifa (IHR 2005). Aidha nchi nyingine zenye uwezo mkubwa duniani
zilisita kufanyiwa tathmini hadi miaka miwili baadae, na nyingine hadi
sasa hazijafanya zoezi hili. Hivyo basi, taarifa zinazoenea kuelezea
kuhusu Tanzania kutokuweka wazi taarifa za magonjwa hususan uwepo wa
ugonjwa wa Ebola nchini, si za kweli na hivyo ziendelee kupuuzwa.
Taratibu za utoaji wa taarifa za magonjwa ya milipuko zinajulikana na
ninatoa rai kwa sote tuzingatie sheria na taratibu za nchi husika na za
kimataifa.
Ikumbukwe kuwa, ugonjwa wa Ebola
ambao unaweza kusambaa kwa haraka, na ambao madhara yake ni makubwa na
yanajulikana duniani kote, kamwe hauwezi kufichwa na nchi yetu. Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua madhara makubwa ya kuficha
ugonjwa kama huu kwa wananchi. Narudia tena na kuwataka wananchi
kutulia na kupuuza taarifa zisizo rasmi kutoka kwenye baadhi ya vyombo
vya habari na mitandao ya kijamii, maana HAKUNA UGONJWA WA EBOLA NCHINI
TANZANIA. Inaonekana kuna njama ovu za kueneza taarifa hasi dhidi ya
nchi yetu. Ninaendelea kuwasihi Wananchi kuwa watulivu na kushikamana
kwa pamoja katika kuzuia ugonjwa huu usiiingie nchini.
Aidha, Serikali inapenda
kuwahakikishia Mataifa yote kuwa nchi yetu ni SALAMA na HATUNA UGONJWA
WA EBOLA. Nirudie tena kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana
na nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Shirika la Afya
Duniani katika kujenga utayari wa kukabiliana na tishio la ugonjwa wa
Ebola. Na endapo kutatokea mtu atakaethibishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola
nchini tutaendelea kuzingatia miongozo na taratibu za kimataifa ikiwemo
kutoa Taarifa WHO kwa mujibu wa Kanuni za Kimataifa za udhibiti wa
magonjwa hatari ya kuambukiza (IHR 2005).
Kipaumbele cha Wizara kwa sasa ni
kuendelea kuimarisha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huu usiingie
nchini na endapo kutatokea kisa cha ugonjwa huu nchini tuweze
kukabiliana nao na kuudhibiti mara moja.
0 comments:
Post a Comment