Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo amekabidhi watumishi 42 wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga
pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kwa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa mkoani Rukwa kwa uchunguzi wa upotevu wa fedha wa
zaidi ya shilingi milioni 916 baada ya kuonekana utetezi wao juu ya
upotevu wa fedha hizo kutokuwa na vielelezo vya kutosha.
Mh. Wangabo ametoa maelekezo hayo
baada ya kuitisha kikao cha Wakurugenzi, Wawekahazina, wahasibu na
watendaji wa vijiji na kata wa halmashauri zote nne mkoani hapa ambao
mfumo wa ukusanyaji mapato ngazi ya halmashauri (Local Government
Revenue Collection Information System – LGRCIS) kuonesha kuwa fedha za
makusanyo yao kubaki mifukoni mwao.
Aidha, Ametoa siku saba kwa wale
wote ambao hawajawasilisha fedha za makusanyo yao benki kuhakikisha
wanawasilisha fedha hizo ikiwemo wale waliokabidhiwa kwa TAKUKURU na
kuonya kuwa endapo fedha hizo hazitawasilishwa kesi hiyo itatoka
TAKUKURU na Kuhamia Jeshi la Polisi ili kuwafikisha mahakamani.
“Mimi natafuta fedha ukishindikana
tutakufunga, na ndio maana nimesema jambo hili kwanza lishughulikiwe
kwanza na TAKUKURU mpaka uturudishie hizo fedha kwa muda maalum ambao
nimeutoa, nimeshatoa siku sita zimeisha leo hii natoa siku saba
nyingine, wacha hawa ambao watakuwa wamerudisha, wale ambao watakuwa
hawajakabidhisha fedha zao, nitatoa siku saba baada ya hapo kesi hii
itatoka TAKUKURU na kuhamia polisi ili iende mahakamani,” Alisema
Katika kujadili sababu mbalimbali
zinazopelekea fedha za makusanyo kutumiwa bila ya utaratibu maalum
mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Joseph Sengerema
amesema kuwa matatizo ya upotevu wa fedha hizo yanasababishwa kutokana
na kukiuka sheria ya fedha za Serikali za Mitaa ambayo hairuhusu
Mtendaji kufanya matumizi yoyote bila ya ridhaa ya mkurugenzi wa
Halmashuri na kabla ya kuwasilisha fedha hizo benki.
“ Ukiangalia katika Halmashuri ya
Wilya ya Nkasi mimi nishatahadharisha kwamba, kuna hatari kubwa mtendaji
wa kijiji anapokusanya fedha halafu anapeleka fedha hiyo kwa mtendaji
wa kata bila ya kuwa na nyaraka maalum inayokiri upokezi wa fedha hizo,
kwa hali hiyo unawezaje kusimamia ili fedha hizi zisipotee? Na pia
mtendaji wa kata anapozifikisha idara ya fedha anahakikishaje zinfishwa
benki kwa wakati?” Alihoji.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya
Nkasi Mh. Said Mtanda limshukuru Mh. Wangabo kwa kuwasaidia kupambana na
upotevu wa mapato katika halmashauri jambo ambalo wamekuwa wakilitolea
maelekezo akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya bila ya
matunda.
“Usikivu wa watendaji wetu ni
mdogo sana lakini nikuahidi kwamba maelekezo uliyoyatoa ya siku saba
nitayafanyia kazi na kesho Defaulters (wadaiwa) wote tukutane pale
ukumbi mdogo wa halmashauri ili niweze kuwakabidhini kwa Halmashauri ili
Mkaanze utaratibu wa uchunguzi,” Alisisitiza.
Mmoja wa Watendaji hao Lusilus
Bruno wa Kata ya Kirando, Wilayani Nkasi alikiri kuwepo kwa makosa ya
kufanya matumizi kabla ya fedha hizo kufikishwa kwenye halmashauri jambo
linalokwamisha kupokelewa kwa fedha pungufu wakati wa kuzipeleka benki
na kusema kuwa upungufu huo unatokana na matumizi wanayoyafanya katika
shughuli za kila siku za vijiji na kata.
“ Mtendaji wangu wa kijiji Tarehe
15 alinikabidhi shilingi 439,500/= ambazo tulitoa matumizi ya shilingi
150,000/= ambayo tuliandika dokezo kama kawaida na kumpa Mkurugenzi
akakataa na kusema kuwa matumizi hayo ni makubwa, hilo deni likafika
shilingi 540,100 kwa maana kwamba ile bili ilikuwa bado inasubiri ile
150,000 ili iende benki lakini mpaka jana ilikuwa bado makusanyo ni
shilingi 100,800/= ambazo alinikabidhi kwahiyo tulishindwa kusafisha
bili kwasababu ya upungufu wa shilingi 150,000,” Alisema.
Kati ya hao waliokabidhiwa
TAKUKURU watumishi 22 ni watendaji wa kata na vijiji kutoka Halmashauri
ya wilaya ya Nkasi, na watumishi 18 ni watendaji wa kata na vijiji
kutoka Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na mmoja ni mweka hazina na
mhasibu wote wa Wilaya ya Nkasi na wengine 16 kutoka halmashauri ya
wilaya ya Sumbawanga walitakiwa kuandika maelezo pamoja na kuambatanisha
vielelezo vya kuwasilisha fedha zao kwa mweka hazina wa halmashauri ya
Wilaya ya Sumbawanga.
0 comments:
Post a Comment