Na Mwandishi wetu.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Prof Godius Kahyarara amesema Serikali iko mbioni kuanzisha vituo vya biashara vya kimataifa katika maeneo ya mipakani ili kuwezesha ununuzi wa bidhaa zetu kwa urahisi.
Katibu Mkuu huyo ametoa agizo hilo wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Biashara kutoka mikoa yote nchini yaliyokuwa yakifanyika Jijini Dodoma.
“Watu wanapokuja kununua bidhaa za kitanzania sio lazima waendeshe gari kutoka namanga mpaka Tunduma,hii ni fursa kama tukiambiwa kuna ardhi tutawaita wawekezaji wataenda kuangalia maeneo hayo,tutahakikisha wanaweka vitendea kazi kwa ajili ya kupima ubora wa mazao kama ni mahindi na vitu vingine basi vipimwe hapo hapo mpakani,pia tutahamasisha taasisi nyingine za Serikali ambazo zinahusika katika kuratibu biashara kuwa na vituo vyao vya huduma katika maeneo hayo ,aliongeza Prof.Kahyarara
Pamoja na hayo Prof Kahyarara amesisitiza Maafisa biashara kote nchini kuandaa kanzi data ya ardhi ambayo itaonyesha maeneo ya uwekezaji katika mkoa husika.
“Hivi sasa Mheshimiwa Rais ameshaagiza tuwe na kanzi data ya ardhi ambapo ubora wa kanzi data hii utategemea taarifa sahihi ambazo wenzetu hawa maafisa biashara walioko mikoani watazitengeneza,ikionyesha ukubwa wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji ”Alisisitiza Prof Kahyarara.
Pia amesema kwa sasa Serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele kikubwa katika uwekezaji na lazima maafisa biashara hao waweze kushiriki katika kulifanikisha suala hilo.
Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) Bw.Daudi Riganda amesema lengo la mafunzo hayo kwa maafisa biashara hao ni kuwafundisha namna gani wanaweza kuwahudumia wawekezaji katika maeneo yao.
“Tumewaita Maafisa Biashara wote ili wafahamu namna gani wanaweza kufanikisha uwekezaji katika maeneo yao na namna gani wanaweza kushirikiana na kituo cha uwekezaji kuwawezesha wawekezaji,pili halmashauri na ofisi za wakuu wa mikoa wasaidie kutengeneza mazingira wezeshi ambayo yatafanikisha uwekezaji wa aina zote ufanyike katika maeneo yao.”alisema Bw.Riganda
Aidha kwa upande wake Afisa Biashara wa Mkoa wa Mwanza Bw. Yesaya Sikindene amesema wamejifunza mambo mengi mazuri na ambayo wanaenda kuyafanyia kazi ikiwemo kutoa elimu kwa wajasiriamali wa ngazi zote na kuhakikisha wanasajiliwa kupitia kituo cha uwekezaji nchini (TIC) na kuhakikisha wanaandaa kanzi data ya wafanyabiashara wote walio katika maeneo yao kujua wanafanya biashara gani,wako wapi na wanazalisha nini.
0 comments:
Post a Comment