Na Mwandishi
Wetu, Mwanza
Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Luteni Josephine Paul
Mwambashi amewataka wahasibu na wakuu wa idara kuandaa mapema taarifa za miradi
ili kusiwe na usumbufu wowote wanapofika kukagua au kuzindua miradi hiyo.
Amesema lengo lao sio kukomoa au kumuumiza mtu ni kuhakikisha
miradi hiyo inatumia thamani halisi ya fedha zilizoelekezwa huku akiwataka
wananchi kuitunza miradi hiyo kwani ililetwa kwa ajili yao.
Ameyasema hayo Julai 3, 2021 wakati akizungumza na wananchi
katika maeneo tofauti Wilayani Magu, wakati timu ya kukimbiza mwenge kitaifa
ilipoweka mawe ya msingi, kuzindua na kukagua miradi mbalimbali ambayo
ilipangwa kutembelewa na mwenge wa uhuru.
Amesema miradi mingi ambayo ipo nchini ililetwa kwa lengo la
kuwahudumia wananchi, hivyo lazima ionyeshe thamani halisi ya fedha ambayo
imetolewa na Serikali wao kama wakaguzi hawatosita kutoa maelekezo pindi
watakapobaini upotoshwaji wa taarifa katika mradi.
Akipokea Mwenge huo na wakimbiza Mwenge kutoka Mkoani Simiyu
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Senyi Simon Ngaga amesema ukiwa Mkoani Mwanza
Mwenge wa uhuru, utatembelea Miradi 74 yenye thamani ya shilingi bilioni 50.3
ambapo katika miradi hiyo ipo ambayo itazinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi.
Amefafanua kuwa gharama za miradi zilizotoka
serikali kuu ni bilioni 38.7, halmashauri shilingi bilioni 2.3,
nguvu ya wananchi ni bilioni 1.9 huku bilioni 7.2 zikichangiwa na
wahisani.
Makabidhiano ya Mwenge wa uhuru yalifanyika katika kijiji cha Salama
kata ya Ng'haya wilaya ya Magu Julai 3, 2021 na mara baada ya kukabidhiwa
Mwenge huo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza aliukabidhi kwa Mkuu wa wilaya ya Magu
Mhe. Salum Hamisi Kalli tayari kuukimbiza wilayani humo.
Ukiwa Wilayani Magu Mwenge huo uliifikia miradi 14 ambapo
ulifanya ukaguzi wa ujenzi wa shule ya Sekondari Bugatu, ilifanya uzinduzi wa
mradi wa kampeni ya lishe, ilizindua klabu ya wapinga rushwa, pamoja na
kuzindua mradi wa TEHAMA, ambapo kiongozi wa Mwenge alishuhudia mfumo huo
unavyofanya kazi.
Aidha Mwenge huo utakimbizwa katika wilaya za Ilemela Julai 4,
Ukerewe Julai 5, Nyamagana Julai 6, Sengerema Julai 7, Misungwi Julai 8,
Kwimba Julai 9 na Julai 10 utakabidhiwa Mkoani Shinyanga.
0 comments:
Post a Comment