Monday, July 5, 2021

Mwenge wa Uhuru Kufikia miradi 74 yenye thamani ya Bil 50.3 Mkoani Mwanza





Na Mwandishi Wetu, Mwanza


Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Luteni Josephine Paul Mwambashi amewataka wahasibu na wakuu wa idara kuandaa mapema taarifa za miradi ili kusiwe na usumbufu wowote wanapofika kukagua au kuzindua miradi hiyo.


Amesema lengo lao sio kukomoa au kumuumiza mtu ni kuhakikisha miradi hiyo inatumia thamani halisi ya fedha zilizoelekezwa huku akiwataka wananchi kuitunza miradi hiyo kwani ililetwa kwa ajili yao. 


Ameyasema hayo Julai 3, 2021 wakati akizungumza na wananchi katika maeneo tofauti Wilayani Magu, wakati timu ya kukimbiza mwenge kitaifa ilipoweka mawe ya msingi, kuzindua na kukagua miradi mbalimbali ambayo ilipangwa kutembelewa na mwenge wa uhuru. 


Amesema miradi mingi ambayo ipo nchini ililetwa kwa lengo la kuwahudumia wananchi, hivyo lazima ionyeshe thamani halisi ya fedha ambayo imetolewa na Serikali wao kama wakaguzi hawatosita kutoa maelekezo pindi watakapobaini upotoshwaji wa taarifa katika mradi. 


Akipokea Mwenge huo na wakimbiza Mwenge kutoka Mkoani Simiyu Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Senyi Simon Ngaga amesema ukiwa Mkoani Mwanza Mwenge wa uhuru, utatembelea Miradi 74 yenye thamani ya shilingi bilioni 50.3 ambapo katika miradi hiyo ipo ambayo itazinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi.


Amefafanua kuwa gharama  za miradi zilizotoka  serikali kuu ni bilioni 38.7,  halmashauri shilingi bilioni 2.3, nguvu  ya wananchi ni bilioni 1.9 huku bilioni 7.2 zikichangiwa na wahisani. 


Makabidhiano ya Mwenge wa uhuru yalifanyika katika kijiji cha Salama kata ya  Ng'haya wilaya ya Magu Julai 3, 2021 na mara baada ya kukabidhiwa Mwenge huo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza aliukabidhi kwa Mkuu wa wilaya ya Magu Mhe. Salum Hamisi Kalli tayari kuukimbiza wilayani humo.


Ukiwa Wilayani Magu Mwenge huo uliifikia  miradi 14 ambapo ulifanya ukaguzi wa ujenzi wa shule ya Sekondari Bugatu, ilifanya uzinduzi wa mradi wa kampeni ya lishe, ilizindua klabu ya wapinga rushwa, pamoja na kuzindua mradi wa TEHAMA, ambapo kiongozi wa Mwenge alishuhudia mfumo  huo unavyofanya kazi.


Aidha Mwenge huo utakimbizwa katika wilaya za Ilemela Julai 4, Ukerewe Julai 5,  Nyamagana Julai 6, Sengerema Julai 7, Misungwi Julai 8, Kwimba  Julai 9 na Julai 10 utakabidhiwa Mkoani Shinyanga.

No comments:

Post a Comment