METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, June 4, 2021

WAZIRI MKENDA NA VIPAUMBELE SABA VYA KIMKAKATI BAJETI YA WIZARA YA KILIMO KWA MWAKA 2021/2022

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma


Katika Mpango na Bajeti ya mwaka 2021/2022 wa Wizara ya Kilimo umezingatia mambo mbalimbali katika utekelezaji wake ambayo ni Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2020-2025, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano Awamu ya Tatu (2021/2022– 2025/2026, na Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II)


Miongozo yote iliyoainishwa  imesisitizwa katika Hotuba ya Rais, Mhe Samia Suluhu Hassan, alipolihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Aprili, 2021.  Hotuba hiyo imeweka dira kwa kuanisha vipaumbele vikubwa na vya kimkakati.


Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda alibainisha hayo Tarehe 24/25 Aprili 2021 wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Kilimo mwaka 2021-2022 ambapo alisema kuwa Katika kupanga mipango ya mwaka 2021/2022 Wizara pia imezingatia vipaumbele kama vilivyosisitizwa kwenye maelekezo ya  Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Ndg Daniel Chongolo, tarehe 20 Mei, 2021.


Waziri Mkenda anasema mpango  mkubwa wa kimkakati ni kuongeza tija katika uzalishaji. Hivyo, kipaumbele cha kwanza kikubwa cha kimkakati katika kuongeza tija ni kuweka mkazo katika utafiti utakaozingatia ugunduzi wa aina za mbegu bora na mbinu bora za kilimo.


Ili kufikia malengo hayo serikali itafanya utafiti wa mbegu bora zenye tija kubwa kwa mfano tafiti zinaonesha kuwa TARI  wamefanikiwa kugundua aina za mbegu za muhogo inayozalisha wastani wa tani 22-50 kwa hekta ikilinganishwa na wastani wa tani 8 kwa hekta zinazozalishwa sasa na wakulima wengi. Kwa upande wa pamba tija ya sasa ni kilo 250-300 kwa ekari ikilinganishwa na uwezo wa kufikia wastani wa kilo 1000-2000 kwa ekari, kuongeza bajeti ya TARI kutoka Shilingi bilioni 7.35 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 11.63 mwaka 2021/2022, na kuimarisha upatikanaji wa fedha za maendeleo ya utafiti wa kilimo kwa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Utafiti kwa mujibu wa Kifungu 26(1) cha Sheria Na. 10 ya mwaka 2016 iliyoanzisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI Act No. 10, 2016).


Kipaumbele cha pili cha kimkakati cha kuongeza tija ni kuongeza uzalishaji wa mbegu bora. Waziri Mkenda amesema kuwa ili kuongeza uzalishaji wa mbegu bora nchini, Wizara imepanga kuendeleza mashamba 13 ya mbegu  ya ASA kwa kuweka miundombinu ya umwagiliaji kwa kutumia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji; kuongeza bajeti ya uzalishaji wa mbegu bora kutoka Shilingi bilioni 5.42 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 10.58 mwaka 2021/2022; na kuendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika kuzalisha mbegu bora nchini.


Katika hotuba yake Waziri Mkenda alikitaja kipaumbele cha tatu cha kimkakati ni kuimarisha huduma za ugani. Idadi ya Maafisa Ugani wanaotoa huduma za  ugani nchini katika ngazi ya Kata na Vijiji ni 6,704. Idadi hiyo, ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji ya 20,538. Pamoja na idadi hiyo kuwa ndogo, Maafisa ugani hao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa vitendea kazi pamoja na mafunzo rejea. upungufu huo wa maafisa ugani pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo huchangia wakulima wengi kukosa huduma za ugani ikiwemo matumizi ya mbegu bora, matumizi sahihi ya viuatilifu, zana bora, mbinu bora za kilimo na taarifa za masoko.


Hivyo ili kukabiliana na changamoto hizo, Wizara imeongeza bajeti ya eneo hilo kutoka Shilingi milioni 603 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 11.5 mwaka 2021/2022. Fedha hizo zitatumika katika kuimarisha huduma za ugani nchini ikiwa ni pamoja na kununua pikipiki 1,500, vifaa vya kupima afya ya udongo, visanduku vya ufundi (Extension Kit), simu janja, kuwezesha uanzishwaji wa mashamba ya mfano kwa kila Afisa Ugani na kutoa mafunzo rejea. Vilevile, maafisa ugani watasimamiwa katika kuanzisha mashamba darasa kulingana na mahitaji ya wakulima kwa ajili ya kuendeleza kilimo katika eneo husika.


Waziri Mkenda aliongeza kuwa serikali itaianza safari yake kwa kuboresha huduma za ugani katika mikoa mitatu ya kielelezo ambayo ni Dodoma, Singida na Simiyu. Mikoa hiyo ina fursa kubwa ya kuzalisha mazao ya mafuta hususani alizeti na pamba. Katika Mikoa hiyo maafisa ugani wote watapewa pikipiki, vifaa vya kupima afya ya udongo, visanduku vya ufundi (Extension Kits), simu janja, kuwezesha uanzishwaji wa mashamba ya mfano kwa kila Afisa Ugani na kutoa mafunzo rejea yatakayozingatia mazao yote yanayolimwa katika maeneo hayo. Pia maafisa ugani hao, watawezeshwa kuanzisha mashamba darasa.


Kipaumbele cha nne cha kimkakati ni kuimarisha kilimo cha umwagiliaji. Kilimo hapa nchini kinategemea mvua kwa asilimia kubwa ambazo hazitabiriki kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, Kilimo cha umwagiliaji kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ubovu wa miundombinu, kutokamilika kwa baadhi ya miradi ya umwagiliaji, kukosekana kwa miundombinu ya umwagiliaji yenye fursa za umwagiliaji, mitaji ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na elimu ndogo ya matumizi ya teknolojia za umwagiliaji.


Katika kuimarisha kilimo cha umwagiliaji nchini, Wizara imepanga kuongeza eneo la umwagiliaji kwa kuhamasisha wadau kuwekeza katika ujenzi miundombinu, uvunaji wa maji na uchimbaji wa visima kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Aidha, Wizara kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji (IDF) ulioanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 52 cha Sheria ya Umwagiliaji Na. 4 ya mwaka 2013 itakamilisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo mashamba 13 ya mbegu ya ASA, kukarabati miundombinu ya umwagiliaji, kukamilisha miradi ya umwagiliaji, kujenga mabwawa na kufanya upembuzi yakinifu kwenye miradi mipya.


Kipaumbele cha tano cha kimkakati ni kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo. Changamoto ya masoko nchini ina sura kuu mbili; kwanza ni uzalishaji mdogo usiokidhi mahitaji ya soko na pili ni kuwepo kwa uzalishaji mkubwa ikilinganishwa na upatikanaji wa masoko. Kwa mfano, viwanda vya kukamua mafuta ya alizeti vinafanya kazi takribani miezi minne kwa mwaka kutokana na ukosefu wa malighafi. Kwa upande wa mazao ya nafaka ikiwemo mahindi na mpunga, uzalishaji wake ni mkubwa na ziada inakosa soko.


Waziri Mkenda alibainisha Kipaumbele cha sita cha kimkakati ni kuimarisha KILIMO ANGA kwa ajili ya kudhibiti visumbufu vya milipuko na vihamavyo kama vile nzige, kwelea kwelea na viwavijeshi vamizi. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kumekuwa na ongezeko la visumbufu vigeni vinavyoathiri uzalishaji wa mazao na kusababisha upotevu wa mazao hadi asilimia mia moja endapo havitadhibitiwa kikamilifu na kwa wakati. Aidha, baadhi ya visumbufu kama vile nzige na kwelea kwelea udhibiti wake unahitaji vifaa maalum kama vile ndege kwa ajili ya savei na unyunyuziaji wa viuatilifu.


Kipaumbele cha saba cha kimkakati ni kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa mitaji. Akiwasilisha bajeti yake Waziri Mkenda alisema kuwa Upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya shughuli za kilimo umekuwa na changamoto kutokana na riba kubwa zinazotozwa, masharti ya kupata mikopo kutoka taasisi za fedha na vihatarishi katika sekta ya kilimo.  Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa ni asilimia 30 tu ya wakulima wanaofikiwa na huduma za mikopo. Aidha, ni asilimia kati ya 7 na 9 ya mikopo iliyotolewa na mabenki ya biashara katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imeelekezwa kwenye sekta ya kilimo.

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com