METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, May 24, 2021

REA III mzunguko wa Pili na PERI URBAN kwa Kanda ya Kaskazini, yazinduliwa rasmi

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na Wakazi wa Kijiji cha Terati katika Wilaya ya Arusha Jiji wakati wa uzinduzi Mradi wa Kusambaza umeme katika Vijiji vilivyopembezoni mwa Miji (PERI URBAN) kwa Kanda ya Kaskazini uliofanyika mkoani Arusha, Mei 23, 2021.

 

Wakazi wa Kijiji cha Kiseriani katika Kata ya Engikageti wilayani Longido mkoani Arusha wakimsikiliza Waziri wa Nishati (hayupo) pichani, akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu( REA III) mzunguko wa pili kwa Kanda ya Kaskazini uliofanyika mkoani humo, Mei 23,2021.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akikabidhi kifaa cha Umeme Tayari( UMETA) kwa Wakazi wa Kijiji cha Kiseriani katika Kata ya Engikageti wilayani Longido mkoani Arusha, wakati wa uzinduzi rasmi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu( REA III) mzunguko wa pili kwa Kanda ya Kaskazini uliofanyika mkoani humo, Mei 23,2021.

Wazee wa Kimila( kushoto) wa Kijiji cha Terati katika Wilaya ya Arusha Mji wakimkabidhi zawadi Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani(kulia)  baada ya kumsimika na kumpa jina la Ole Kalemani wakati wa uzinduzi rasmi Mradi wa Kusambaza umeme katika vijiji vilivyopembezoni mwa miji(PERI URBAN) kwa Kanda ya Kaskazini uliofnyika mkoani Arusha, Mei 23, 2021.

Na Zuena Msuya, Arusha

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua rasmi Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu( REA III) mzunguko wa Pili na ule wa Usambazaji wa Umeme kwa Vijiji vilivyoko Pembezoni mwa Miji (PERI URBAN) kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

Uzinduzi huo umefanyika mkoani Arusha katika wilaya mbili tofauti, ambapo REA III mzunguko wa pili ulizinduliwa katika Kijiji cha Kiseriani Kata ya Engikageti wilayani Longido na PERI URBAN ulizinduliwa katika Kijiji cha Terati Wilaya ya Arusha Jiji mkoani humo, Mei 23, 2021.

Kanda ya Kaskazini inahusisha Mikoa minne ambayo ni Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati akizindua mradi huo, Dkt. Kalemani aliwataka wakazi wa maeneo husika kuanza kutandaza nyaya katika nyumba zao ili kujiandaa kuunganishiwa umeme katika nyumba zao wakati wakandarasi wakifanya kazi ya kuusambaza katika maeneo yao.

Aidha aliwaeleza wananchi hao kuwa gharama za kuunganishiwa umeme huo ni shilingi 27,000 na kwamba wasikubali kutozwa gharama zaidi na watu wasiowaaminifu.

“Wanzania kwa sasa suala la  kuweka umeme ni lazima ndugu zangu, serikali imeamua kubeba gharama zote na kuwataka kuchangi 27,000 tu, hii ni kuhamasisha kila mwananchi aunganishiwe, utakuwa mtu wa ajabu serikali imeleta umeme katika eneo lako na kwa bei nafuu halafu wewe usiweke umeme tutakushanga kwakweli, hii fursa itumieni vizuri” alisisitiza Dkt. Kalemani.

Dkt.Kalemani aliweka wazi kuwa REA III mzunguko wa pili utatekelezwa ndani ya kipindi cha miezi 18 na unatekelezwa na kampuni ya SAGEMCOM kutoka nchini Ufaransa na Peri Urban utatekelezwa ndani ya kipindi cha miezi 12 na unatekelezwa na Kampuni ya DERM ambayo ni ya Kitanzania.

Hata hivyo aliwaeleza wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo, kufanya kazi usiku na mchana ili kumaliza kazi hiyo hata kabla ya muda uliopangwa, na kwamba wachukue vijana kutoka kila eneo husika ili kutekeleza kazi za uchimbaji wa mashimo, kusimika nguzo na kufunga waya ili na wao wanufaike na uwepo wa mradi huo.

Aliwaeleza wakandarasi hao kuwa serikali haitaongeza muda wa ziada kwa mkandarasi yeyote atakayechelewa kukamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa, na kwamba ikitokea mkandarasi akafanya hivyo atakatwa asilimia 10 ya fedha zake ikiwa ni adhabu kama makubaliano ya mkataba yanavyoelekeza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Nishati Vijiji (REA), Mhandisi Amos Maganga aliwaeleza wakandarasi hao kuwa wanatakiwa kujitambulisha kwa uongozi wa ngazi za Wilaya, Kijiji na Kata kabla ya kuanza kazi zao ili wafahamike na kupewa ushirikiano.

Vilevile aliwataka wananchi kushirikiana vyema na wakandarasi hao ili waweze kufanya kazi zao kwa urahisi, na kwamba wanakijiji wawe walinzi wa miundombinu ya umeme pamoja na vifaa vitakavyokuwa vikitumika.

Aidha aliwasisitiza wananchi kuwa gharama za kutandaza nyaya katika nyumba zao ni makubaliano kati yao na fundi atakayetekeleza kazi hiyo, pia aliwataka kuwatumia mafundi walioidhinishwa na shirika la umeme Tanzania (TANESCO) kufanya kazi hiyo.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com