Na WMJJWM, TANGA
Serikali imetoa wito kwa wadau wa mchezo wa mpira wa miguu kutumia kombe la Ngao ya Jamii na Ligi nyingine kuelimisha jamii masuala ya maendeleo na ustawi ikiwemo kuachana na vitendo vya ukatili hasa kwa watoto.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mkoani Tanga, Agosti 12, 2023, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema tangu mashindano ya Ngao ya Jamii ya kuanza jijini humo, Agosti 09, Kampeni ya kuelimisha Jamii kuhusu ukatili wa watoto kupitia mpira wa miguu na usalama wa watoto katika mpira (Safe Sports Campaign)imeendelea kufanyika.
Amesema kampeni hiyo yenye kaulimbiu Zuia Ukatili dhidi ya Watoto; inafanyika katika mashindano hayo kwa kutambua nguvu ya mpira wa miguu kuwa ni mchezo unaopendwa na wenye wafuatiliaji wengi zaidi.
"Wizara iliwasilisha ombi la kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia mashindano yanayoendelea ya Ngao ya Jamii ili itumie jukwaa ili kutoa elimu kwa wasikilizaji na watazamaji kuhusu kukabiliana na ukatili kwa watoto." amesema Dkt. Gwajima.
Ameongeza kuwa, katika kuimarisha kampeni hiyo kwa kutumia mpira wa miguu, Wizara imefanya mazungumzo ya awali na vilabu vya Yanga na Azam ili kuwashirikisha kutokomeza ukatili dhidi ya Watoto wakati wakiendelea na ligi kwa mwaka 2023/2024.
"Tunatarajia kufanya mazungumzo na Shirikisho la Soka Tanzania ili kutumia michezo ya ligi inayoanza hivi karibuni kusaidia Wizara katika kampeni hii muhimu kwa watoto wetu. Tunafanya mawasilisano na wadau mbalimbali ili kuona namna kampeni itakavyoshirikisha wadau wengi tofauti kwa lengo la kupata matokeo makubwa zaidi.
Aidha amesisitiza kwamba, familia kama msingi wa jamii ina jukumu la kukabiliana na changamoto hizo kwa kuimarisha maadili na kuwajibika kwenye malezi yanayozingatia miiko, tamaduni, kanuni na taratibu za jamii zetu.
Waziri Dkt. Gwajima ameeleza baadhi ya juhudi za Serikali katika kukabiliana na changamoto ya ukatili kwa watoto, ikiwemo kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mwongozo wa Taifa wa Wajibu wa Wazazi au Walezi katika malezi ya watoto na Familia unaojulikana Familia Bora, Taifa Imara, unaoainisha maeneo ya msingi katika malezi na makuzi ya mtoto kuanzia miaka 0 hadi 18.
Ametaja pia uanzishwaji wa kituo cha Huduma kwa wateja cha "Jamii Call Center," ambapo wananchi wanaweza kupiga simu au kutuma ujumbe ili kupata elimu, ufafanuzi au malalamiko kwa namba 0262160250 au 0734986503.
Katika hatua nyingine Waziri Dkt. Gwajima ametumia nafasi hiyo kuzungumza na baadhi ya watoto wa mkoa wa Tanga katika shule ya msingi Pongwe ambako amesisitiza watoto kujilinda wao wenyewe na kuwasikiliza wazazi na walezi wao.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment