Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Jakaya Kikwete amezitaka nchi za Afrika, hususani za ukanda wa SADC kutumia ipasavyo rasilimali walizojaliwa kwa maendeleo ya wananchi ikiwemo kwa kuziongezea thamani ndani ya nchi zao badala ya kuzisafirisha kwenda nje zikiwa ghafi.
Amezitaka nchi za SADC kuendelea kuwa na mshikamano ili kuepuka kuingia katika mtego wa kinyang'anyiro cha rasilimali kinachozidi kushika kasi barani Afrika baina ya mataifa makubwa duniani.
Dkt Kikwete ameyasema hayo leo tarehe 17 Agosti 2023 katika Chuo cha Diplomasia cha Venâncio de Moura kilichopo Luanda, Angola wakati alipohudhuria Mhadhara Maalumu ulioandaliwa na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kama sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC utakaofanyika nchini humo.
Akiwasilisha mada inayohusu umuhimu wa amani na usalama kwa maendeleo ya eneo la kusini mwa Afrika, Rais Mstaafu Kikwete, pamoja na mambo mengine, amehimiza umuhimu wa kutazama suala la amani na usalama kwa ujumla wake badala ya kuchukulia tafsiri iliyozoeleka ya kwamba amani na usalama maana yake ni kutokuwepo kwa fujo ama vurugu.
Amesema kuwa ili jamii na nchi iwe na amani ni lazima Serikali zitimize wajibu wake kikamilifu si tu wa kulinda mipaka ya nchi, bali pia kuhakikisha wananchi wake wanapata mahitaji muhimu yanayotakiwa kutolewa na serikali kama vile huduma za afya, elimu, na ujenzi wa miundombinu ya msingi.
Watoa mada wengine katika Mhadhara huo ni pamoja na Luisa Diogo, Waziri Mkuu Mstaafu wa Msumbiji na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, João Bernardo de Miranda. Mhadhara huo umehudhuriwa na Viongozi wa Serikali ya Angola, Wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali za SADC, wanafunzi, nk.
Rais Mstaafu Kikwete anatarajiwa pia kutumia fursa ya kuwepo nchini Angola kushiriki Mkutano wa Kilele wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (Troika) utakaofanyika tarehe 16 Agosti 2023 ambapo anatarajiwa kutoa taarifa ya Mgogoro wa Lesotho kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la SADC (POE) ambalo limepewa jukumu la kutafuta suluhu ya mgogoro uliopo nchini humo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment