Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akisistiza jambo wakati akifungua mafnzo ya mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini ya mwongozo wa namna bora ya uchukuaji wa sampuli za uchunguzi na uchenjuaji madini Mkoani Ruvuma.
Baadhi ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Ruvuma wakifuatilia mafunzo yaliyotolewa na GST kwa wachimbaji wadogo wa madini
Sehemu ya Wachimbaji wadogo wa madini wakifuatilia ufunguzi wa mafunzo ya nmana bora ya uchukuaji wa sampuli za uchunguzi na uchenjuaji wa Madini Mkoani Ruvuma.
Katibu Mkuu wa wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila katika picha ya Pamoja ya Watumishi wa Ofisi ya Madini Mkoa wa Ruvuma
Na Asteria Muhozya, Ruvuma
Imeelezwa kuwa, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) inatarajia kuongeza wigo wa huduma kwa kuanzisha Vituo vya Huduma za Maabara na Ushauri Elekezi katika Kanda zenye uzalishaji wa Madini kwa wingi.
Hayo yamebainishwa Mei 12, 2021 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila wakati akifungua mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini ya mwongozo wa namna bora ya uchukuaji wa sampuli za uchunguzi na uchenjuaji madini Mkoani Ruvuma.
Prof. Msanjila ameongeza kuwa, hivi karibuni GST itaanza kutoa huduma hizo katika Mkoa wa Geita na baadaye Chunya, na hivyo kuwataka wachimbaji wadogo nchini kuitumia vyema taasisi hiyo kutokana na manufaa watakayoyapata kutoka kwa wataalam wenye ujuzi na waliobobea katika fani mbalimbali katika Sekta ya Madini.
‘’Ni muda muafaka sasa kushirikiana na GST kwa karibu zaidi kwa kuanza kuchukua sampuli zitakazozingatia mafunzo haya na kuziwasilisha maabara ya GST kwa huduma bora na majibu ya uhakika ikizingatiwa kwamba, maabara ya GST inatambuliwa kimataifa kwa kuwa na ITHIBATI ya ubora katika uchunguzi wa dhahabu,’’ amesisistiza Prof. Msanjila.
Ameongeza kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu inatambua umuhimu wa wachimbaji wadogo, hivyo, kutokana na wajibu wa GST katika kuhakikisha sekta inafanya vizuri imepelekea kufanyika kwa mafunzo hayo ambayo yanalenga kuwasaidia wachimbaji wadogo kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha kwa kufanya uchimbaji endelevu na wenye tija ili kuwasaidia wachimbaji kuongeza uzalishaji na hatimaye kuongeza mchango wao kwenye pato la taifa ambao hivi sasa bado ni mdogo .
Aidha, Prof. Msanjila ameipongeza GST kwa jitihada inazozifanya katika kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini ikiwemo kuwa karibu nao kwa kuwapatia elimu mbalimbali zinazohusiana na masuala ya madini kupitia machapisho, vitabu, huduma za maabara, ushauri elekezi na mafunzo mbalimbali yakiwemo hayo ambayo yanatolewa katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Prof. Msanjila ameipongeza Ofisi ya Madini Mkoa wa Ruvuma kwa kuvuka lengo la makusanyo katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 ambapo hadi kufikia mwezi Aprili, 2021 imekusanya shilingi bilioni 8.9 sawa na asilimia 141 na hivyo kuvuka lengo la kukusanya shilingi bilioni 7.5 iliyopangiwa kukusanya.
‘’ Nipende kuwaambia mnafanya kazi nzuri sana. Kama wizara, tunajua Ruvuma mnafanya vizuri ndiyo sababu hata migogoro hakuna. Nawaomba pamoja na kuendelea na majukumu yenu lakini mzidi kujiendeleza kielimu,’’ amesisitiza Prof. Msanjila.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Steven Ndaki ameipongeza wizara
na GST kwa kuwezesha mafunzo hayo kufanyika mkoani humo na kueleza kwamba, yatawawezesha wachimbaji kufanya shughuli zao kwa uhakika. Aidha, ameipongeza wizara kwa kuanzisha masoko ya madini mkoani humo hivyo kurahisisha biashara ya madini.
Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Ruvuma , Issack Ngaladela ameishukuru GST kuwezesha mafunzo hayo na kusema kuwa, awali wachimbaji walikuwa wanachimba kwa hisia na kwa miaka mingi imewapelekea kupoteza muda mwingi na mitaji. ‘’ Mafunzo haya yatatubadilisha, sasa tutachimba kisayansi,’’ amesema.
Mbali na wachimbaji, katika siku ya kwanza mafunzo hayo pia yamewashirikisha Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo, Makatibu Tawala na viongozi wa wachimbaji wa mkoa husika.
Vilevile, katika ziara hiyo pia, Prof, Msanjila ametembelea Mgodi wa wachimbaji wadogo wa Makaa ya Mawe wa GodMwanga uliopo katika kijiji cha Malinyi wilaya ya Nyasa kwa lengo la kusikiliza changamoto na kushauri namna bora ya kufanya shughuli zao.
0 comments:
Post a Comment