METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, May 13, 2021

Zaidi ya Bilioni 7 zatumika kufikisha umeme Kisiwa kilichopo Ziwa Tanganyika

Kiongozi wa Wazamiaji kutoka Zanzibar Faki Musa akiufunga kamba waya wa umeme kwaajili ya kuvutwa na kuingia ziwani ili kuufikisha katika kisiwa cha Mandakerenge, Wilayani Naksi Mkoani Rukwa.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo (kulia) akishirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda (wa pili kushoto) kuvuta waya wa umeme unaopitishwa ziwa Tannganyika kuelekea kisiwa cha Mandakerenge.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mj. Joachim Wangabo na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi mh. Said Mtanda wakiangalia namna waya a umeme unavyopitishwa chini ya maji katika ziwa Tanganyika. 

Zoezi la kupakua waya wa umeme na kuupitisha katika ziwa Tanganyika likiendelea katika kijiji cha kipili, kata ya kipili, Wilayani Nkasi , Mkoani Rukwa. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kaundasuti nyeusi) akisikiliza maelezo ya Meneja wa TANESCO Mkoa wa Rukwa Mhandisi Yusuf Ismail juu ya mawe yanayoshikilia waya ndani ya maji ziwani.

Baadhi ya wafanyakazi wa TANESCO wakishirikiana na wananchi kuupakua waya kwaajili ya kuupitisha ziwani kwenda katika kisiwa cha Mandakerenge kilichopo umbali wa km 1.2.

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupitia Nakuroi Investment Co. Ltd inayotekeleza Mradi wa awamu ya tatu mzunguko wa kwanza wanaendelea na zoezi la kulaza nyaya chini ya maji katika ziwa Tanganyika ili kufikisha umeme katika kisiwa cha Mandakerenge, kilichopo kata ya Kipili Wilayani Nkasi, Mkoani Rukwa.

Zoezi hilo litakalogharimu zaidi ya shilingi bilioni 7 ni la kipekee kufanyika katika ziwa Tanganyika, na mikoa ya kanda ya ziwa, hali iliyopelekea Meneja wa Tanesco Mkoa wa Mwanza na timu kutoka makao makuu ya Shirika la umeme nchini (TANESCO) kufika katika eneo hilo na kujifunza utandazaji wa nyaya hizo ili kuja kuutumia ujuzi huo kufikisha umeme kisiwani Ukerewe, Mkoani Mwanza.

Akiongea wakati wa kushiriki kulaza nyaya hizo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema kuwa tukio hilo linaonesha ni kwa namna gani serikali inavyowatahamini wananchi wake na kuzingatia haki zao za kupata huduma za kijamii saw ana watu wanaoishi katika mengine ya nchi.

Aidha amewapongeza wazamiaji wazawa wanaofanya kazi hiyo, TANESCO Mkoa Pamoja na Mkandarasi wa Mradi huo pamoja na kuwaomba wananchi wa kisiwa na Kijiji cha Mandakerenge kuutumia umeme huo vizuri ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vya kuchakata samaki pamoja na mashine za kusaga na kukoboa

“Serikali ya Tanzania inathamini wananchi popote pale walipo na umeme huu utakwenda kila mahali ndani ya vijiji vyetu vya mkoa wa Rukwa, baada ya kufikisha umeme katika kisiwa cha Mandakerenge itakuwa ni takriban vijiji 181 vitakuwa vimefikiwa na umeme na nimeambiwa huyu mkandarasi Nakuroi amebakiza kama vijiji viwili vitatu ili vitimie vijiji 184 ambavyo vitakuwa vinapata umeme na vijiji vinavyobaki kama 155, hivi vijiji vitapata umeme ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu,” Alisema.

Amesema kuwa katika ya vijiji hivyo 155 vilivyobaki, vijiji 125 vimeingizwa katika mradi wa awamu ya tatu mzunguko wa pili na vijiji 30 vimeingia kwa maombi maalum na hivyo kufanya jumla ya vijiji vya mzunguko wa kwanza na wapili kuwa 339 ambavyo ni idadi ya vijiji vilivyopo mkoani Rukwa.

Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Rukwa Mhandisi Yusuf Ismail alieleza kuwa zoezi hilo lilitakiwa kukamilika ndani ya wiki nne lakini kutokana ushiriki mzuri wa wanakijiji katika mradi, hali nzuri ya hewa ziwani Pamoja na kasi ya kazi hiyo huenda zoezi hilo likamalizika chini ya muda uliopangwa.

“Serikali imewashirikisha wananchi ili kwanza wajue thamani ya mradi ambayo imewekezwa hapa lakini pia iwe ni kutoa elimu kwa wavuvi wengine au kwa wananchi wengine ambao wako ng’ambo ambao wanaweza kukutana na kitu kama hiki wajue thamani yake, mheshimiwa mkuu wa mkoa naomba nikushuruku kwa kuja kutupa moyo katika kazi hii naamini wazamiaji na wafanyakazi wote wa TANESCO tumfurahia ujio wako,” Alimalizia.

Kwa upande wake mwakilishi wa mkandarasi wa mradi huo wa REA Mkoani Rukwa Mhandisi Pascal Ndunguli alisema kuwa kwa upande wao walikabdihiwa kukamilisha mradi huo katika vijiji 137 na kati yahi vyo vijiji 135 tayari vimewashwa umeme na hivyo kubakiwa na vijiji 2 kimojawapo kikiwa ni hicho cha kisiwa cha Mandakerenge ambacho wanatazamia kukimaliza kabla ya mwezi wa sita mwaka huu.

“Mpaka sasa tupo hatua ya kulaza nyaya na baada ya hapo, wazamiaji watakuwa hawana kazi watafuata watu wa kitengo cha umeme na hivyo wahandisi watakuja kwaajili ya kukamilisha zoezi na baada ya hapo tutawaalika TANESCO kuja kufanya majaribio na kuthibitisha kuwa umeme unapita na kisha tutafikisha umeme katika Kijiji hicho na umeme utaanza kufanya kazi,” Alisema.

Katika ziara hiyo alikuwepo mwakilishi wa wavuvi na wanakijiji cha Kijiji cha Mandakerenge Seif Seba ambaye naye alitoa shukurani kwa serikali ya Tanzania, “Tunatoa shukurani za dhati kwa serikali yetu kwa kutujali kwa suala la kutuletea umeme hapo kisiwani na tunaiahidi serikali kuwa tutaulinda huu way ana hakuttotokea athari ya namna yoyote,” Alimalizia.

Kisiwa cha Mandakerenge kipo umbali wa km 1.2 kutoka bara ambapo shughuli kubwa za wanakijiji wa kisiwa hicho ni uvuvi na TANESCO wametandaza waya wenye urefu wa km 1.7 kutoka bara kwenda kisiwani ili wanakijiji hao nao wafaidike na mradi huo.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com