METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, October 15, 2020

RUWASA YAKUMBUSHWA KUZIJENGEA UWEZO JUMUIYA ZA WATUMIAJI MAJI NCHINI

 Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA, Profesa Idrissa Mshoro akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Maofisa wa RUWASA kutoka Mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Pwani na Simiyu (hawapo pichani).

 Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA, Profesa Idrissa Mshoro (katikati) na watendaji wa RUWASA wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Mkama Bwire (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Maofisa wa RUWASA kutoka Mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Pwani na Simiyu.

Wakala ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imetakiwa kuhakikisha Jumuiya za Watumiaji Maji (CBWSOs) zinakuwa na uwezo wa kupanga, kukusanya na kusimamia maduhuli yatokanayo na mauzio ya maji ili kuwa na miradi endelevu.

Maelekezo hayo yalitolewa hivi karibuni Mkoani Mwanza na Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA, Profesa Idrissa Mshoro wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Maofisa wa RUWASA kutoka Mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Pwani na Simiyu.

Profesa Mshoro alisisitiza kwamba ili miradi inayotekelezwa na RUWASA iwe endelevu ni lazima Jumuia za Watumiaji Maji (CBWSOs) wakajengewa uwezo kuanzia hatua za awali.

“Menejimenti mnatakiwa kuimarisha uwezo wa Jumuiya kwa mipango madhubuti ya kujenga uwezo, kudhibiti na kusimamia taasisi na huduma, CBWSOs ziwe na uwezo wa kupanga, kukusanya na kusimamia maduhuli yatokanayo na mauzo ya maji yatakayowezesha uendeshaji na matengenezo ya mradi,” alisisitiza Profesa Mshoro.

Aliwaelekeza watendaji wa RUWASA kuhakikisha wanaimarisha uhusiano na ushirikiano na taasisi zingine zikiwemo Ofisi za Mabonde, Mamlaka za Maji, Ofisi za Serikali za Mitaa, Halmashauri na Ofisi za Wakuu wa Wilaya na Mikoa ili kufikia malengo na mipango walionayo.

Alisema kumekuwa na changamoto kwa Halmashauri kutopata taarifa za RUWASA kama inavyopasa na hivyo alielekeza watendaji kuhakikisha wanawasilisha ripoti zao kwenye Ofisi za Halmashauri na Mikoa na Wilaya kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Mbali na hilo, Profesa Mshoro aliitaka Menejimenti ya RUWASA kuonesha njia kwa kudumisha dhana ya ushirikiano katika ngazi ya mipango, bajeti na mawasiliano na taasisi zilizochini ya Wizara ya Maji.

“Undugu huo wa uasili na usambazaji wa rasilimali maji unafanya kusiwe na mjadala katika umuhimu na ulazima wa kushikiana kwa taasisi hizi; tutumie fursa ya mtazamo, msimamo na msisitizo wa wizara ya maji katika ufanyaji kazi kama wizara moja, huduma moja, mlengwa mmoja,” alielekeza Profesa Mshoro.

Mara baada ya kikao hicho, Washiriki watafanya ziara ya kutembelea baadhi ya miradi inayotekelezwa na RUWASA Mkoani Mwanza kwa lengo la kujionea hali ya utekelezaji wake sambamba na kubadilishana uzoefu.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com