Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Muigizaji wa Tamthilia maarufu ya
ESMERALDA kutoka nchini Mexico, aliyekuja nchini kwa mapumziko ya siku
saba na watoto wake, wakati Waziri Mkuu akiwa mkoani Arusha kwenye ziara
ya kikazi. Julai 23.2019. Tokea kushoto ni watoto wa muigizaji huyo,
Carlo Collado (14) na Luciano Collado (15).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wafanyakazi wa hoteli ya The Retreat at Ngorongoro iliyoko wilayani Karatu, wakati akiwa mkoani Arusha kwenye ziara ya kikazi. Julai 23.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
………………..
*Zimo Ngorongoro, Serengeti, Manyara na Tarangire
*Ni Leticia Calderon, aliyeigiza filamu ya ESMERALDA
MUIGIZAJI maarufu wa filamu kutoka
Mexico, Bi. Leticia Calderon (51) amesifia rasilmali ya hifadhi za
wanyama ambayo Tanzania imejaliwa kuwa nayo.
Muigizaji huyo ambaye amefanya kazi hiyo
kwa miaka 36, na ameigiza sinema maarufu ya ESMERALDA, yuko nchini kwa
mapumziko ya siku saba kwenye hifadhi za wanyama za ukanda wa Kaskazini.
Akisalimiana na Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa aliyekuwa mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi, Bi. Calderon
amesema amevutiwa na uzuri wa hifadhi za Tanzania na idadi kubwa ya
wanyama aliowaona kwenye hifadhi za Taifa za Tarangire, Manyara na
Ngorongoro.
“Kwa miaka mingi nilikuwa natamani sana
kuja Tanzania kuona wanyama. Tuliyoyaona yametufurahisha mimi pamoja na
wanangu. Nchi yenu ina uzuri wa kustaajabisha. Watu wenu ni wema na
wakarimu,” alisema Bi. Calderon.
“Ninafurahi kwamba ndoto yangu imetimia.
Tulienda Tarangire, Manyara na Ngorongoro ma sasa tunajiandaa kwenda
Serengeti. Tulipokuwa Ngorongoro, tuliona simba wanne, majike wawili na
madume wawili. Tumefurahi sana na nikirudi nyumbani, nitawaonyesha picha
marafiki zangu na kuwaalika waje kutembelea Tanzania,” alisema.
Bi. Calderon ambaye amefuatana na wanaye
wawili Luciano Collado (15) na Carlo Collado (14) alisema wakimaliza
mapumziko yao huko Serengeti watakwenda Masai-Mara kwa siku tatu na
kisha wataelekea Paris, Ufaransa kumtembelea rafiki yake ambaye
waliigiza filamu pamoja huko nyuma.
Bi. Calderon pia ameigiza tamthilia ndefu (soap operas) 29 katika jiji la Mexico City ambalo ni mji mkuu wa Mexico. Mbali ya Esmeralda, filamu nyingine maarufu ambazo ameigiza ni En Nombre del Amor (In the Name of Love); Amor Bravia (Valiat Love) na La Indomable (The Taming of the Shrew).
Waziri Mkuu alimshukuru mwanamama huyo na
wanaye kwa kuichagua Tanzania kwa mapumziko yao na akawatakia heri
katika safari yao ya mbugani.
Akizungumza na wafanyakazi wa hoteli ya The Retreat at Ngorongoro iliyoko
Karatu ambako muigizaji huyo alikuwa amefikia, Waziri Mkuu aliwataka
wafanyakazi wa hoteli hiyo na wengine walioko kwenye hifadhi za Taifa,
wafanye kazi kwa bidii ili huduma zao ziwavutie watalii wengi zaidi.
“Tunampongeza mwenye hoteli kwa uwekezaji
huu mkubwa lakini niwasihi wafanyakazi mchape kazi ili wageni wengi
zaidi waweze kuvutiwa na huduma zenu,” alisema Waziri Mkuu.
“Sasa hivi tunapata watalii wengi na watu
maarufu kama hawa, wamechagua kuja kupumzika Tanzania. Mheshimiwa Rais
Magufuli ameshanunua ndege sita, nyingine mbili zinakuja, moja itawasili
Oktoba, na nyingine Januari, mwakani. Na tayari kuna ndege tatu
nyingine zimeagizwa. Lengo lake ni kuimarisha usafiri wa ndani kwa
kutumia ndege,” alisema.
“Zamani ilikuwa ni vigumu sana kuja
Tanzania moja kwa moja. Ili mtalii afike, ilibidi apitie nchi nyingine
na huko akidakwa anaondokea hukohuko. Sasa hivi, akitoka kwao ataweza
kuja Tanzania moja kwa moja, akitua KIA anakuja Karatu au Serengeti moja
kwa moja,” alisema.
0 comments:
Post a Comment