Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista
Mhagama, amelitaka Baraza la Vyama vya siasa nchini kuendelea kutekeleza
majukumu yake ipasavyo kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu juu ya
masuala yenye maslahi kwa Taifa kuhusiana na vyama vya siasa pamoja na
hali ya kisiasa nchini ili kuimarisha ustawi wa siasa na vyama vya
siasa nchini.
Mhe. Waziri Mhagama ameyasema hayo wakati
akifungua kikao cha siku mbili cha Baraza hilo kilichoanza jana na
kinafungwa leo, tarehe 24, Julai 2019, mjini Dodoma katika ukumbi wa
Pius Msekwa, ambapo Mhe. Mhagama amesisitiza vyama hivyo kuendelea
kushirikiana na kudumisha upendo na umoja wa kitaifa katika kutekeleza
majukumu yao ya kisiasa ili kuweza kuijenga Tanzania yenye umoja.
“Endeleeni kutumia fursa za vikao vya
Baraza kutatua matatizo yenu na niwashauri muunde kamati za Baraza na
kutumia kamati hizo katika kutatua matatizo yenu, lakini pia tekelezeni
majukumu yenu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu tulizonazo hapa
nchini ili vyama viweze kuisaidia nchi na watanzania kuyafikia malengo
yao kwa kuwajenga watanzania kuwa wamoja badala ya kuwagawanya” amesema
Mhagama
Mhe. Waziri Mhagama amefafanua kuwa
katika vikao vyao na serikali Baraza hilo walikuwa na matakwa yao ambayo
walitaka serikali iyatekeleze kupitia ofisi ya Msajili wa Vyama vya
siasa nchini ambapo tayari serikali imeyatekeleza ikiwemo kuanzisha
ofisi ya Naibu msajili wa vyama vya siasa Zanzibar.
“Serikali ya awamu ya Tano chini ya
Rais, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli, kupitia ofisi ya Waziri Mkuu,
katika bajeti yake, ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa, tayari
imetenga bajeti ya kuiendesha Ofisi ya Naibu Msajili wa vyama vya siasa
Zanzibar, lakini pia sisi serikalini tumeshakubaliana kuwashirikisha
viongozi wa Baraza la vyama vya siasa katika matukio ya shughuli za
maendeleo ya serikali ili viongozi nyie muweze kuelewa vyema mabadiliko
ya utekelezaji yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano” Amesisitiza
Mhe. Mhagama.
Aidha, Mhe. Mhagama ameeleza kuwa Wajumbe
wa Baraza hilo watakuwa wakijengewa uwezo katika masuala ya siasa ili
kuweza kuendelea kujenga msingi imara na ustawi wa demokrasia nchini.
Awali, akiongea katika kikao hicho,
Mwenyekiti wa Baraza hilo, John Shibuda, ameeleza kuwa wanashukuru kwa
ushirikiano ambao wamekuwa wakiupata kutoka serikalini kupitia Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya siasa ambapo ameomba kuendelea kushirikishwa
ipasavyo ili waweze kuelewa vyema utekelezaji wa shughuli za maendeleo
za serikali ya awam ya tano.
“Baraza tunamshukuru sana Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Mhagama kwa ushirikianao ambao amekuwa
akitupatia Baraza kimsingi hivi leo tunajivunia miaka miwili ya utendaji
wa Baraza letu lakini msingi wa mafanikio hayo ni Waziri huyu amekuwa
ufungua ambao atufungulia milango kila jambo tunalotaka kulitekeleza
kwa wakati ” amesema Shibuda.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Msajili wa
vyama vya siasa nchini, Mhe. Jaji Francis Mutungi, Naibu Msajili wa
Vyama vya siasa, Mhe. Mohammed Ally Ahmed, pamoja na wajumbe wa Baraza
hilo ambao ni vyama vyenye usajili wa kudumu. Baraza la Vyama vya Siasa
limeanzishwa chini ya kifungu cha 21B cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura
ya 258 ikiwa ni jukwaa la viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa
kukutana mara kwa mara kujadiliana masuala yanayohusu demokrasia ya
vyama vingi na siasa hapa nchini kwetu. Baraza hilo limeundwa ndani ya
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambapo, Wajumbe wa Baraza hilo
hujumuisha viongozi wa kitaifa wawili wa kila chama cha siasa chenye
usajili wa kudumu. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa ndio yenye jukumu
la kisheria ya kuratibu shughuli za Baraza la Vyama vya Siasa.
Majukumu ya Baraza hilo ni pamoja na
kumshauri Msajili wa vyama vya siasa juu ya masuala yenye maslahi kwa
Taifa kuhusiana na vyama vya siasa au kuhusiana na hali ya kisiasa
nchini Siasa na sheria zingine zinazohusu masuala.
0 comments:
Post a Comment