METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, October 21, 2020

BODABODA WAASWA KUWA MABALOZI WA ULINZI NA USALAMA

Waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda wameaswa kuwa mabalozi wazuri wa ulinzi na usalama kwa kuhakikisha wanashirikiana na vyombo vya dola kufichua waharifu katika jamii.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na waendesha pikipiki wa kata ya Kitangiri VIWAPIKI (Vijana Waendesha Pikipiki Kitangiri) katika sherehe za kutimiza miaka 12 ya kikundi chao ambapo amewaasa kushirikiana na Serikali katika kudumisha amani, ulinzi na usalama pamoja na kuwachukulia hatua watu wote wenye nia mbaya katika jamii

‘.. Kazi mnayoifanya ni nzuri, Lakini kubwa nyie ni mabalozi nambari moja wa ulinzi na usalama kwa sababu matukio mengi ya uharifu yanafanyika kupitia nyinyi, Mna uwezo wa kubeba mtu kumbe ndio jambazi ..’ Alisema

Aidha Dkt Mabula akawaasa waendesha pikipiki hao kufuata sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali zisizo za lazima sambamba na kuwataka kujiunga katika vikundi ili waweze kukopesheka na kujiari kwa kununua pikipiki mpya za kwao binafsi badala ya kutegemea kuajiriwa pekee.

Akisoma risala ya kikundi hicho, Bwana Maiga Malegesi akasema kuwa kikundi chao kilianzishwa mwaka 2008 kikiwa na wanachama 12 na mpaka sasa kinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mtaji wa mradi rasmi wa kikundi ambapo wamefanikiwa kuchangishana kiasi cha shilingi milioni moja na laki mbili hivyo kuomba kuchangiwa kiasi cha milioni moja na laki nane ili waweze kuanzisha mradi kikundi.

Nae afisa wa jeshi la polisi wilaya ya Ilemela Inspekta Rusendela akawahakikishia ushirikiano waendesha pikipiki hao huku akiwashukuru kwa mchango wao kwani pamoja na nchi kuingia katika uchumi wa kati mchango wa waendesha pikipiki katika mafanikio hayo hauwezi kutenganishwa.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com