Sehemu ya Wajumbe waliofuatana na Balozi Adt (hayupo pichani) nao wakifuatilia mazungumzo
Mazungumzo yakiendelea
Waziri Mahiga akiagana na Balozi Adt mara baada ya kumaliza mazungumzo.
Waziri Mahiga (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mjumbe Maalum, Balozi Adt (wa nne kushoto) pamoja na MaafisaWaandamizi kutoka Wizarani pamoja na Ubalozi wa Ujerumani nchini.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa kuhusu Mjumbe Maalum kutoka Ujerumani
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amesema kuwa
Tanzania na Ujerumani zitaendelea kuimarisha ushirikiano katika masuala
mbalimbali ikiwemo yale yanayohusu kudumisha amani na usalama duniani
pamoja na kuheshimu misingi ya haki za binadamu kupitia Jumuiya za
Kikanda na Kimataifa.
Mhe. Waziri Mahiga ameyesema hayo
alipokutana kwa mazungumzo na Balozi Harro Adt, Mjumbe Maalum wa Kansela
wa Ujerumani, Mhe. Angela Merkel kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli alipofika Wizarani kwa ajili ya
kuwasilisha ujumbe huo.
Katika mazungumzo yao, Mhe. Waziri
Mahiga alisema kuwa, Ujerumani na Tanzania zina mahusiano ya kihistoria
tangu enzi za ukoloni hadi sasa. Katika masuala ambayo Tanzania
inanufaika na ushirikiano huo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu,
maboresho katika sekta ya elimu na mchango katika uhifadhi wa
wanayamapori.
“Uhusiano wa Tanzania na Ujerumani ni wa
kihistoria tangu ukoloni. Hata hivyo Ujerumani wamejaribu kutafsiri
ushirikiano wetu katika misingi bora sasa kuliko ile ya kikoloni.
Ujerumani imekuwa ikiisaidia Tanzania moja kwa moja katika sekta
mbalimbali kama elimu, wanyamapori na miundombinu na misaada mingine
imekuwa ikipitia Umoja wa Ulaya” alisema Waziri Mahiga.
Akizungumzia ziara ya Balozi Adt nchini,
Mhe. Waziri Mahiga alisema Mjumbe huyo Maalum wa Kansela wa Ujerumani
ameleta ombi kwa Mhe. Rais na kwa Watanzania la kuiunga mkono Ujerumani
kwenye nafasi ya Mjumbe asiye wa Kudumu kwenye Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa wakati wa uchaguzi utakaofanyika mwaka 2018. Aliongeza
kusema kuwa, Ujerumani imedhamiria kugombea nafasi hiyo ikiwa na
dhamira ya kuunga mkono mageuzi ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa ikiwemo kuziunga mkono nchi za Afrika kwenye harakati za
kupatiwa nafasi mbili za kudumu kwenye Baraza hilo.
Aidha, Mhe. Waziri Mahiga alifafanua
kwamba, katika kufikia malengo hayo Ujerumani imejiwekea misingi mikuu
minne ambayo ni:- Kusaidia jitihada za amani na usalama duniani;
Kusimamia Haki ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa;
Kuhamasisha mageuzi ya Teknolojia na Kuhimiza ushirikiano na Ubia wa
Kimataifa.
Mhe. Mahiga alieleza kuwa kwa kuzingatia
misingi hiyo, amemueleza Balozi Adt azma ya Tanzania kuiomba Ujerumani
iisadie Afrika kujenga Jengo la Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu
na Watu ambapo Tanzania ndio Makao yake Makuu huko Mjini Arusha.
Mhe. Mahiga pia alimhakikishia Balozi Adt kuwa ameupokea ujumbe wa Kansela wa Ujerumani na atauwasilisha kwa Mhe. Rais.
Kwa upande wake Balozi Adt, Mjumbe
Maalum kutoka Ujerumani alisema kuwa amefurahishwa na mapokezi
aliyoyapata baada ya kuwasili nchini. Pia ana imani kuwa Tanzania ambao
ni rafiki wa kihistoria wa Ujerumani itawaunga mkono kwenye nafasi hiyo
ili kuwawezesha kutekeleza malengo waliyojiwekea ikiwemo kuhakikisha
Afrika inapata nafasi mbili za kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja
wa Mataifa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 12 Machi, 2017
0 comments:
Post a Comment