Sehemu ya wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo wakifurahia tuzo ya ushindi wa kwanza wa Wizara waliyokabidhiwa wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya wakulima (NANENANE) jana Tarehe 8 Agosti 2020.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA umeibuka kidedea kwa kushika nafasi ya kwanza kwenye tuzo zilizotolewa kwa washindi walioshiriki kwenye maadhimisho ya wakulima (Nanenane) yanayofanyika kwenye Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu kwa kupata Pointi 72.9
Tuzo hiyo ya NFRA ina maana kubwa kwani umewaacha nyuma washindani wengine ambao ni Wakala wa Nishati Vijijini (REA) iliyoshika nafasi ya pili kwa kupata Pointi 70.3 na mshindi wa tatu ambaye ni Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania-TASAC kwa kupata Pointi 68.9
Kwa upande wa tuzo za Wizara katika maonesho hayo ni Wizara mama ya Kilimo ndio imewaning’iniza wenzake kwa kuongoza kwa Pointi 91.7 huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi yenye Pointi 87.1 na nafasi ya tatu imechukuliwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEM).
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa kombe la ushindi Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Kusaya amewashukuru wafanyakazi wa Wizara hiyo kwa ushirikiano mkubwa wa uandaaji wa maonesho hayo jambo lililopelekea kuibuka washindi.
Kusaya amesema kuwa maonesho hayo yatakuwa endelevu ili wakulima waendelee kunufaika na elimu inayotolewa kuhusu mbinu bora za kilimo ikiwa ni pamoja na matumizi ya zana bora za kilimo.
Maadhimisho ya wakulima (NANENANE) yamefika ukomo jana tarehe 8 Agosti 2020 ambapo mgeni rasmi aliyefunga maonesho hayo kitaifa Mkoani Simiyu Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa amezipongeza Wizara zote za kisekta zinazohusika na kilimo, Taasisi za Umma na binafsi kadhalika wakulima na wananchi wote walioshiriki katika Maonesho hayo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment