1.0 UTANGULIZI
Kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona, Serikali ililazimika kufunga shule zote nchini mnamo tarehe 17.03.2020 kwa lengo la kuepusha misongamano itakayopelekea kusambaa kwa maambukizi hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. ANTHONY MTAKA aliibua mjadala katika kundi la wakuu wa shule (TAHOSSA) wenye lengo la kuwasaidia wanafunzi hasa wa madarasa ya mitihani katika kipindi hiki cha likizo ya CORONA. Mjadala huu uliwashirikisha pia baadhi ya viongozi wakuu wa Mkoa kama vile Katibu Tawala wa Mkoa Ndg. JUMANNE SAGINI, Afisaelimu Mkoa Ndg. ERNEST HINJU pamoja na viongozi wengine wa elimu ngazi ya Mkoa na Wilaya.
Baada ya majadiliano ya kina yaliyoshirikisha wadau mbalimbali wa elimu kama vile RICHARD MABALA (Mwandishi wa vitabu vya Fasihi), Mkoa uliazimia kuja na Mkakati utakao wawezesha wanafunzi kupata masomo wakiwa nyumbani kutoka kwa walimu wao (Online teaching).
Hii ni baada ya kufanya tathmini na kubaini kuwepo kwa changamoto za wanafunzi kukosa msaada wa kimasomo kwa kipindi hiki wakiwa nyumbani, na waathirika zaidi ni madarasa ya mitihani ambayo ni darasa la IV, VII kidato cha II, IV, na VI. Mpango mkakati huu ni njia mojawapo ya kuendelea kuboresha elimu Mkoani simiyu. Ikumbukwe kwamba Mkoa wa Simiyu umeazimia kuwa miongoni mwa Mikoa michache nchini inayofanya vizuri zaidi kwenye elimu.
Kutokana na changamoto hizo, Mkoa umekuja na mapendekezo/Mikakati itakayowasaidia wanafunzi, walimu, wazazi na wadau wengine wa elimu katika kuinua taaluma Mkoani Simiyu.
2.0 LENGO KUU LA MKAKATI WA MKOA.
Kuufanya Mkoa uendelee kufanya vizuri kitaifa kama ilivyo adhima yetu ya kuingia tatu bora kitaifa.
3.0 MALENGO YA MPANGO MKAKATI WA MKOA.
Mpango mkakati huu umejikita hasa katika kuendeleza malengo ya mkoa dhidi ya kuboresha elimu. Malengo yamejikita katika maeneo makuu matatu:-
1.1.1 Kumwezesha mwanafunzi kuendelea na kulazimika kujifunza akiwa likizo
1.1.2 Kumwezesha mwalimu kuwa na mawasiliano ya kitaaluma na mwanafunzi
1.1.3 Kuwawezesha wazazi kuwa na uelewa na kufanya ufuatiliaji wa taaluma kwa watoto wao kipindi hiki cha likizo.
1.1.4 Kuwafanya watoto / wanafunzi kutumia muda wa likizo ya CORONA kutulia nyumbani kujisomea kwa maelekezo ya walimu kuepuka kuzurura na kujihatarisha na kuambukizwa ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu
4.0 MKAKATI WA ELIMU MKOA WA SIMIYU KATIKA KIPINDI HIKI CHA LIKIZO YA UGONJWA WA CORONA.
4.1 Kuandaa ‘Packages’ za maswali na mitihani.
Kila mwalimu wa somo husika anatakiwa kuandaa au kutunga kazi/maswali/mitihani mingi yenye ubora unaotakiwa kadiri ya miongozo ya Baraza la Mitihani (NECTA FORMAT) kwa kugusia kila mada kwa kuzingatia vigezo vyote vya utungaji kama vile Mtaala wa wa masomo kwa ngazi husika na ‘Table of specification’. Kila mwalimu wa somo hususani anayefundisha Darasa la Nne na la Saba, Kidato cha Pili, cha Nne na Sita aandae kazi, maswali na majibu yake yatakayotolewa kupitia njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo kwenye nyumba za Ibada.
Maswali hayo yatamwezesha mwanafunzi kufanya na kumrejeshea mwalimu ili aweze kuona na kumrekebisha. Maswali mengine hasa ya madarasa ya chini yaandaliwe kwa viwango vya mwanafunzi kuweza kujisahihisha mwenyewe palepale, majibu hayo yafichwe na baada ya mwanafunzi kufanya ndipo yatolewe/ayatoe na kujisahihishia. Hii inaweza kutumika kwa maswali ya Multiple choices, Matching items, Filling the blanks and Short answers.
Katika mkakati huu pia walimu wa masomo hasa wale watakaoteuliwa rasmi au wenye vipaji maalum watatakiwa kuandaa vipindi vyenye sifa ya kuweza kurushwa moja kwa moja na vituo vya TV , TV za mitandaoni (On line TVs) na Redio zitakazokubali kuungana nasi kutusaidia kutekeleza mkakati huu. Hii itahitaji matumizi ya studio na vifaa vingine muhimu vya kuboresha vipindi hivi.
Aidha walimu wanaweza kukusanya kazi na maswali haya kutoka kwenye vitabu na vyanzo mbalimbali kama ifuatavyo:-
4.1.1 WhatsApp groups
4.1.2 E-mails
4.1.3 Website mbalimbali
4.1.4 TV channels mbalimbali
4.1.5 Youtube
4.1.6 Wataalam na walimu wabobezi mbalimbali mfano;- Mzee Mabala
4.1.7 Redio; mfano Redio Sibuka FM.
Lengo la mkakati huu ni kuona kila mwalimu wa somo anawajibika kuandaa kazi zenye viwango hitajika tayari kwa kushirikiana na walimu wengine wa somo husika kabla ya kuyawasilisha kwa wanafunzi ambao wako nyumbani kwao kwa ajili ya likizo ya Corona. Aidha kazi hizi lazima ziwe zimeandaliwa maalum kumwezesha mwanafunzi amudu kuilewa na kuijibu mwenyewe bila msaada mkubwa wa maelekezo kutoka kwa walimu (Distance learning).
4.2 Kuwa na mtandao wa walimu kimasomo.
Kila walimu wa somo husika ngazi ya Mkoa na Halmashauri waunde group la whatsApp au Telegram n.k ambalo litaongozwa na walimu viongozi watatu wa kila somo (Orodha ya walimu hawa imeambatishwa pamoja na mkakati huu). Mtandao huu wa walimu uwasaidie kufanya majadiliano ya kina kuhusu kazi/maswali, mtihani pamoja na nukuu za somo na kukubaliana kabla ya kuwasilisha kwa wanafunzi kupitia WhatsApp group, Website za shule, e-mail, TV na Redio, Nyumba za ibada na njia ya simu/message.
Walimu viongozi wa masomo wahakikishe wanasimamia mijadala ipasavyo na kuwasilisha maswali, mitihani pamoja na nukuu za somo zilizokubalika ili kufikia malengo ya Mkoa. Kwa mfano nukuu za fasihi kutoka kwa mdau wa elimu RICHARD MABALA, Mdau huyu aungwe kwenye group la somo husika.
Aidha mbali ya makundi haya ya masomo bado makundi makubwa ya whatsApp ya wakuu wa shule (TAHOSSA), Walimu wakuu na Maafisaelimu kata yataendelea kupokea kazi toka kwa walimu na wataalam mbalimbali. Wakuu wa shule na Walimu wakuu watawafikishia walimu wa masomo husika kwenye makundi ya masomo na kwenye shule zao tayari kuwasilisha kwa wanafunzi kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Mitandao hii ya walimu kwa kila somo itaendelea kutumika hata baada ya kupita kwa tishio na ugonjwa huu wa CORONA kwani ni utekelezaji wa mkakati wa uwepo wa Kamati za taaluma kama ilivyo kwenye mkakati mkubwa wa kuboresha taaluma wa Mkoa.
Kwa hali hii walimu viongozi wa masomo walioorodheshwa wanapaswa kufungua whatsApp group za masomo yao mara moja na kushirikishana kazi mbalimbali kabla ya kuzifikisha kwa wanafunzi walengwa. Kila kundi la somo liwaunge walimu wengine wa somo hilo pamoja na wataalam wengine waliobobea ikiwemo Wathibiti Ubora wa Shule.
4.3 Kuwa na mtandao wa wanafunzi na walimu kuwasiliana, kupokea na kurejesha kazi.
Kutakuwa na mitandao ya wanafunzi na walimu ya kutumiana, kupokea na kurejesheana kazi/maswali na mitihani. Mitandao hii iwe imara sana kwa ngazi ya shule na isimamiwe na wakuu wa shule/walimu wakuu kuona kwamba kazi zilizokubaliwa zinawafikia wanafunzi husika na wao wanarejesha kwa walimu kwa ajili ya kuona usahihi wake na kufanyia masahihisho yake.
Mtandao huu utasaidia wanafunzi kupokea maswali, mitihani pamoja na nukuu mbalimbali za somo kutoka kwa walimu. Pia kupitia mtandao huu wanafunzi watapata nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa maswali yenye changamoto kutoka kwa walimu. Mtandao huu utawaweka karibu kitaaluma walimu na wanafunzi katika kipindi hiki cha likizo ya CORONA (Online teaching).
Aidha mitandao hii inaweza kuhusisha wanafunzi na walimu wote wa Halmashauri /Mkoa chini ya viongozi wa TAHOSSA na Maafisaelimu wa Halmashauri na Mkoa. Mawasiliano haya ya kihalmashauri yanatakiwa yatumie website ya mkoa au shule kubwa kama Shule ya Sekondari Simiyu n.k
Mtandao huu / mawasiliano haya yanaweza kutumia njia zifuatazo;-
4.3.1 WhatsApp group ya shule husika
4.3.2 Website ya shule husika
4.3.3 E-mails za shule na za wazazi/ wanafunzi
4.3.4 Jumbe fupi za simu/ sms na simu za kuongea
4.3.5 Websites na emails za shule za Sekondari Simiyu na Bariadi
4.3.6 Vituo vya TV, TV mtandao na Redio zitakazokubali kama Sibuka FM
4.3.7 Njia nyinginezo hasa kwa Darasa la Nne, Saba , Kidato cha Pili na madarasa yasiyo ya mitihani ikiwepo mawasiliano kupitia nyumba za Ibada na viongozi wa ngazi za chini wa serikali ya kijiji na vitongoji.
Kupitia mkakati huu ndio masomo yenyewe yatakapoendeshwa ambapo itahitajika kuratibiwa vizuri kujua wanafunzi wangapi wanashiriki na wangapi hawashiriki na hatua za mara kwa mara kuchukuliwa ili kazi kubwa na ya maana ifanyike hapa. Kila Jumatatu mwalimu mkuu na mkuu wa shule atafikisha taarifa ya utekelezaji kwa Afisaelimu Kata ,ambaye naye siku ya Jumanne atafikisha taarifa yake kwa Afisaelimu Wilaya/Mkurugenzi.
Afisaelimu wa wilaya / Mkurugenzi naye ataandaa taarifa yake na kuifikisha kwa Afisaelimu Mkoa/ Katibu Tawala Mkoa. Taarifa hii iwe fupi ikionesha pamoja na vitu vingine takwimu za wanafunzi wanaoshiriki na wasioshiriki, ushiriki wa walimu, masomo yaliyofanyiwa kazi kwa wiki, Changamoto, utatuzi na ushauri kama upo.
4.4 Kuwaelekeza wanafunzi fursa nyingine za kupata masomo kupitia mitandao mbalimbali
Walimu wawasiliane na wazazi na wanafunzi kuwaelekeza mitandao mingine iliyopo inayotoa masomo wawapo nyumbani (online platform, tv education channels). Baadhi ya mitandao hiyo ni hii ifuatayo;
4.4.1 Azam tv, channel 100 (Azam extra),TBC
4.4.2 DSTV- PTP 315 na EDU 316
4.4.3 THL application.
4.4.4 TESEApp
4.4.6 Kupitia redio (mfano redio sibuka FM).
4.4.7 Website za shule mbalimbali na vyanzo vingine vitakavyoelekezwa na vitakavyojitokeza
Lengo la mkakati huu ni kuwawezesha wanafunzi kwa wakati wao kufuatilia masomo kwenye mitandao iliyopo kwa ajili ya kujiongezea maarifa ukiachilia masomo wanayolazimika kuyafuatilia kupitia walimu wao. Aidha walimu pia wanaweza kupata maarifa ya kuwapatia wanafunzi kupitia vyanzo hivi.
5.0 NJIA ZITAKAZOWAFANYA WANAFUNZI WAZINGATIE MPANGO MKAKATI WA MKOA
Zifuatazo ni njia pendekezwa ambazo zitawafanya walimu na wanafunzi kuendana na mpango mkakati.
5.1 Walimu wakuu na wakuu wa shule kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na wazazi kwa njia ya simu nk kuhusu maendeleo ya mwanafunzi kitaaluma kipindi hiki cha likizo ya ugonjwa wa CORONA.
5.2 Kutangaza deadlines kwa kazi / maswali na mitihani inayotolewa.
5.3 Kueleza hatua mbalimbali zitakazochukuliwa kwa wanafunzi ambao hawatashiriki katika mpango huu. Kwa mfano kukaririshwa darasa endapo watashindwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na walimu wa masomo.
5.4 Ratiba ya mtihani itolewe kwa kila darasa la mtihani na utaanza siku ya tatu baada ya kufungua shule.
6.0 WAJIBU WA WADAU WA ELIMU KATIKA KUTEKELEZA MKAKATI WA ELIMU.
6.1 Wadau wa elimu ndiyo watu muhimu sana katika kutekeleza Mkakati wa Elimu katika kipindi hiki cha likizo.
Wajibu wao ni kama ifuatavyo.
6.2 Kila mwalimu wa somo aweze kuandaa, kutafuta kazi /maswali na nukuu za somo, kutunga mitihani pamoja na kusahihisha kazi na mitihani hiyo
6.3 Walimu viongozi waanzishe magroup ya masomo husika na kuyasimamia ipasavyo. Wahakikishe ubora wa kazi unazingatiwa kabla ya kuziwasilisha kazi hizo kwa wanafunzi kwa njia zilizokubalika
6.4 Maafisa elimu kata, wakuu wa shule na Walimu Wakuu wahakikishe wanafikisha taarifa muhimu kutoka ngazi ya juu na kuzifikisha kwa walimu husika. Pia wasimamie na kuona kwamba walimu wao wanatekeleza maelekezo kutoka ngazi ya juu. Vilevile Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu walete taarifa ya takwimu ikibidi orodha ya wanafunzi wanaoshiriki na wale wasioshiriki masomo haya kwa njia za mitandao.
6.5 Viongozi ngazi ya Mkoa/Wilaya pamoja na TAHOSSA Mkoa/Wilaya watakuwa na jukumu la ufuatiliaji wa mkakati wa elimu kwa kufanya vikao vya awali kujipanga na vya tathimini ili waweze kuona namna ya kuboresha mahali panapoonesha changamoto. Kwa mfano kila Halmashauri kutakuwa na kikao cha walimu viongozi wa masomo (walimu mahiri) ili kupeana maelekezo ya kusimamia mkakati huu.
7.0 HITIMISHO:
Mkakati huu utafanikiwa zaidi iwapo kila mmoja wetu atatekeleza majukumu yake aliyopangiwa ipasavyo. Hii itapelekea kufikia malengo ya Mkoa kuingia tatu bora Kitaifa kwa kila aina ya Mtihani wa Taifa.
Aidha, ni matarajio ya Mkakati huu kuwa Wazazi watatoa ushirikiano wa kutosha kuwafanya watoto wao/wanafunzi wa Madarasa ya mitihani na yasiyo ya mitihani kutekeleza vyema maelekezo na kazi kutoka kwa walimu wao huku wakijiepusha na tabia zinazoweza kuwafanya waambukizwe na Ugonjwa huu hatari wa Homa kali ya Mapafu (CORONA).
Nice ideal go ahead
ReplyDeleteNice ideal go ahead
ReplyDelete