Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akiongea na Viongozi wa Vyama vya Ushirika
vya Wakulima wa miwa wa Bonde la Kilombero kuhusu namna bora ya kuongeza
uzalishaji sukari kupitia Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, kikao kilchofanyika
katika ofisi za Kiwanda cha Kilombero hivi karibuni
Viongozi wa Vyama vya Ushirika wa miwa wa Kilombero wakiwa katika kikao
na Mrajis wa Vyama vya Ushirika katika ofisi za Kiwanda cha Kilombero
Afisa Ushirika wa wilaya ya Kilombero
Bw. Jackson Mshumba akifafanua
jambo wakati wa kikao na Viongozi wa Vyama vya Ushirika wa miwa
Kilombero.
Kuhama
vyama vya msingi vya Ushirika mara nyingi ni moja ya changamoto zilizobainika
kupunguza ufanisi wa uvunaji wa miwa wenye tija na faida zaidi kwa wakulima wa
miwa. Suala hili limekuwa ni changamoto kutokana na mkulima kuishi eneo tofauti
na shamba lake, hivyo kuleta ugumu wa uratibu wa rasilimali za uvunaji miwa.
Haya
yalibainishwa wakati wa kikao cha majadiliano ya muenendo wa hali ya upungufu
wa sukari nchini hivi sasa. Kikao kilichokuwa kati ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika
na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) Dkt. Benson Ndiege,
viongozi wa Vyama vya wakulima wa miwa wa Bonde la Kilombero pamoja na uongozi
wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, mkoani Morogoro hivi karibuni.
Katika
kikao hicho Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson alipata fursa ya
kujadiliana na wakulima hao changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima wa
miwa ambazo zinasababisha uzalishaji kuwa mdogo kulinganisha na mahitaji ya
soko na kuangalia kwa pamoja namna bora ya kuongeza uzalishaji wa sukari. Moja
ya changamoto kubwa zilizojadiliwa ni pamoja na ufinyu wa soko la miwa
kulinganisha na uwezo mkubwa wa uzalishaji miwa unaotokana na wakulima
kuhamasika na kilimo cha miwa, upatikanaji wa mikopo na hali nzuri ya hewa.
Aidha,
Mrajis amewaomba wakulima kuwa wavumilivu wakati Serikali inaendelea na juhudi
za kuangalia uwezekano wa kuongeza kiwanda cha uzalishaji sukari, jambo ambalo
linaenda kutoa suluhu ya soko kwa kiwango kikubwa kuliko hali ilivyo sasa.
“Nia ya
Serikali ni kujitosheleza kwa sukari, naomba Kiwanda muendelee na juhudi za
kuongeza uzalishaji wa sukari ili kuongeza kiwango cha upatikanaji wa bidhaa
hiyo muhimu katika jamii,” alisema Dkt. Ndiege
Mrajis
aliwaagiza Maafisa Ushirika pamoja na Mrajis Msaidizi wa Mkoa kusimamia
taratibu pale mkulima anapohitaji kuhama uanachama kutoka chama kimmoja kwenda
kingine ili kuondoa changamoto za uvunaji pamoja na kumbukumbu ya taarifa za
mkulima huyo katika vyama. Alishauri ni vizuri mkulima akawa na shamba katika
eneo lake la makazi. Vilevile viongozi hao wameshauriwa kufanya kazi kwa
uadilifu na kufanya uwekezaji wenye tija kwa wanachama.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa Mawasiliano Joseph Rugaimukamu amesema Kiwanda hicho mwaka
huu kimeanza uzalishaji wiki mbili mapema kuliko tarehe za kawaida za
uzalishaji kutokana na hali ya upungufu wa Sukari iliyopo nchini. Akiongeza
kuwa kiwanda kimelazimika kufanya hivyo ili kuongeza bidhaa hiyo sokoni pamoja
na kuitikia wito wa Serikali wa kusaidia upatikanaji wa sukari kwa wananchi na
kwa bei nafuu. Alisema mwaka huu lengo la Kiwanda ni kuzalisha sukari Tani
127,000 akikiri kuwa bado uwezo wa kiwanda ni mdogo kulinganisha na uzalishaji
wa miwa hivi sasa ingawa juhudi za makusudi kwa kushirikiana na Serikali
zinaendelea katika kuhakikisha kuwa uzalishaji unaongezeka.
0 comments:
Post a Comment