Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akikagua mbegu ya pamba inayofanyiwa utafiti kuangalia uwezo wa kuhimili viuatilifu vya ugonjwa wa Mnyauko Fuzari katika shamba la majaribio la kituo cha utafiti TARI Ukiriguru kituo cha Bwanga wilaya ya Chato leo
Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshika mbegu ya pamba katika shamba la majaribio ya mbegu kijiji cha Bwanga wilaya ya Chato.Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt.Geofrey Mkamilo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyevaa koti la blu) akiongea na watumishi wa chama Kikuu cha Ushirika Chato alipotembelea kukagua kiwanda cha kuchambua pamba.Kushoto kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Geita Bw.Claudio Bandisa
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshika cherehani inayotumika kuchambua na kutenganisha pamba mbegu na pamba sufi alipotembela kiwanda cha kuchambua pamba cha Chato .
Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akitazama shamba la pamba la majaribio ya viuatilifu vya pamba chini ya TARI toka kwa watu binafsi kuona endapo vinauwezo wa kudhibiti ugonjwa wa Mnyauko Fuzari lililopo kijiji cha Bwanga Chato.
Serikali imesema inafanya tathmini ya hali ya
ununuzi wa zao la pamba msimu wa mwaka 2019 ili kuondoa changamoto
zilizojitokeza kabla msimu mpya wa ununuzi kuanza mwaka huu.
Akizungumza na viongozi wa wilaya ya Chato mara
baada ya kutembelea viwanda vya kuchambua pamba, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Gerald Kusaya amesema msimu mpya wa ununuzi utatangazwa mara baada ya tathmini
ya msimu uliopita kufanyika.
“ Wizara imegundua kuwa hali ya mazao shambani
kwa pamba bado ,kwani hata vitumba bado havijapasuka kutokana na uwepo mvua
nyingi ,hivyo baada ya ziara hii kwenye mikoa ya kanda ya ziwa serikali itakaa
na watalaam ili kuamua lini wakulima wataanza kuuza pamba yao kupitia Vyama Vya
Ushirika vya Msingi (AMCOS) “ alisema Kusaya
Aliongeza kusema kabla msimu haujafunguliwa
serikali itahakikisha madeni ya wakulima,wanunuzi na ushuru wa AMCOS,
halmashauri pamoja na mfuko wa pembejeo yanalipwa.
“Kila mwananchi atalipwa madai yake na jitihada
za serikali ni kuona madeni haya yanalipwa kabla ya msimu mpya wa ununuzi wa
pamba kuanza” alisitiza Katibu mkuu
Katika hatua nyingine Chama Kikuu cha Ushirika
Chato( CCU) kimetakiwa kuhamasisha wakulima wengi zaidi kuzalisha zao la pamba
ili ipate malighafi za kutosha kutumika kwenye kiwanda chake cha kuchambua
pamba.
Kusaya alitoa wito huo kufuatia taarifa ya
Meneja Mkuu wa Chama hicho Joseph Masingiri kusema kiwanda kimeshindwa
kuendelea na uchakataji marobota kutokana na uhaba wa pamba ambapo msimu wa
2019 ni kilo milioni 13.6 ,000 tu
zilinunuliwa wakati uwezo wake ni kilo milioni 30.
Ili kukabiliana na changamoto za zao
hilo,Katibu Mkuu Kusaya amewataka wataalam wa halmashauri na wa chama
kikuu kuhamasisha wakulima kuzalisha
mazao ya mkonge na korosho ili kuwa na uhakika wa kipato pale zao la pamba linapoyumba.
“ Tulime pamba na mazao mengine ya biashara
kama mkonge na korosho yanayostawi vizuri kwenye mkoa huu wa Geita na kanda ya
ziwa yote .Wizara ya kilimo ipo tayari kuleta mbegu bora za mkonge na korosho
toka taasisi za utafiti ili zigawiwe kwa wakulima “ Kusaya.
Kusaya alitaja faida za zao la mkonge kuwa
katika kipindi cha miaka mitatu baada ya
kupanda mkulima ataanza kuvuna na kuendelea hadi miaka kumi na tano huku
akiendelea na kilimo cha mazao mengine .
Katika kuhakikisha mkoa wa Geita unaongeza
uzalishaji wa mazao nchini,Katibu Mkuu huyo ameelekeza mkoa uwasilishe wizarani
maandiko ya miradi ya kipaumbele ya umwagiliaji ili serikali itafute wadau wa
kuitekeleza.
Nae Katibu Tawala Mkoa wa Geita Dennis Bandisa
aliyeshiriki ziara hiyo aliishukuru wizara ya kilimo kwa kuonesha nia ya
kusaidia kukuza kilimo cha umwagiliaji na kuwa kuahidi kuwa maandiko
atayawasilisha wizarani ndani ya kipindi kifupi.
Taarifa ya
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Eliurd Mwaiteleke kuhusu
sekta ya kilimo ilisema wilaya hiyo ina eneo la hekta 10,810 zinazofaa kwa
umwagiliaj lakini ni hekta 3,416 tu sawa na asilimia 31.6 zinamwagiliwa.
Katika msimu wa mwaka 2019 jumla ya kilo milioni
10.8 za pamba mbegu zilinunuliwa wilayani Chato kupitia AMCOS zenye thamni ya
shilingi Bilioni 13.06 ililipwa kwa wakulima.
0 comments:
Post a Comment