Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa Tatu
kushoto) akimkambidhi mfano wa Hundi, Mwalimu Mkuu wa Shule Msingi Njopeka (wa
Nne kulia) ambayo imetolewa na Shirika
la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Wa Pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji
wa TPDC, Dkt James Mataragio.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akikata utepe
kuashiria uzinduzi wa umeme katika Kijiji cha Kingwira wilayani Kibiti mkoa wa
Pwani.
Naibu Waziri wa Nishati,, Subira Mgalu (kulia)
akikabidhi vifaa vya tiba kwa Zahanati
ya Kijiji cha Mangwi wilayani Kibiti. Wa Pili kulia ni Mbunge wa Kibiti Ally
Ungando. Wa Tatu kutokaa kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt James
Mataragio.
Wananchi katika Kijiji cha Mangwi wakimpokea Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu mara alipofika kijijini hapo kukabidhi vifaa
vya tiba.
.................
Na Hafsa Omar
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa, mradi
wa matumizi ya gesi majumbani ambao utazinduliwa hivi karibuni katika mkoa wa
Mtwara utasaidia kuepuka matumizi ya mkaa ambao licha ya kuharibu mazingira,
husabisha maradhi mbali mbali.
Alisema hayo, Septemba 14, 2019 kwa nyakati tofauti wilayani
Kibiti, Mkoa wa Pwani, alipokuwa akizungumza na wananchi katika vijiji vya
Mangwi na Njopeka, wakati alipoenda kushiriki katika tukio la kukabidhi vifaa
tiba kwa Zahanati ya Mangwi na mfano wa hundi ya shilingi milioni 19,480,000
kwa shule ya msingi Njopeka vilivyotolewa na Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC).
Naibu waziri, alitoa wito kwa wananchi watakaopitiwa
na mradi huo kutumia gesi katika shughuli
zao mbali mbali za kila siku majumbani hali itakayopunguza matumizi ya mkaa na
kutunza mazingira na kwamba mradi
huo unatarajiwa kufika hadi katika wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani.
Vilevile, Naibu Waziri aliipongeza TPDC kwa kazi nzuri
wanayoifanya ya kusimamia sekta ya Mafuta na Gesi nchini na jitihada zao
zimewezesha masuala mbalimbali ikiwemo
kupelekea asilimia 50 ya umeme nchini kuzalishwa kwa kutumia Gesi
Asilia.
“Niwapongeze pia
kwa kusimamia vyema bomba la Gesi linalozewesha gesi kusafirishwa mpaka Dar es
Salaam na kuanza kusambazwa kwa matumizi
ya majumbani, pia limewezesha kupata umeme mwingi ambao sasa tunausambaza hadi vijijini
kupitia mradi wa REA na TANESCO.” Alisema Mgalu
Wananchi wa
vijiji hicho walimpongeza Naibu Waziri kwa jitihada mbalimbali anazofanya ili kuleta
maendeleo kupitia nyanja mbali mbali na kutatua changamoto mbali mbali
zinazowakabili.
Akiwa wilayani humo, Naibu Waziri aliwasha umeme
katika Kijiji cha Kingwira ambapo aliwasihi waatalamu ambao wanafanya kazi za
wiring kupunguza bei ili kila mwananchi aweze kumudu gharama.
‘Serikali imewatengenezea mazingira wezeshi, imewapa
kazi, wapunguzieni gharama wananchi ili waweze kumudu gharama. ’’alisema Mgalu
Naibu Waziri pia alisisitiza kuhusu suala la nguzo kutolipiwa katika miradi
ya umeme vijijini na kuwapongeza
Mameneja wa TANESCO wanaohakikisha kwamba agizo hilo la Serikali linatekelezwa.
0 comments:
Post a Comment