
Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame
Mbarawa (Mb) akikata utepe kuzindua rasmi mradi wa maji wa Kijiji cha
Shilima, Kata ya Kikubiji, Wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza.

Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame
Mbarawa (Mb) akifungua bomba la maji la mradi wa Shilima wakati wa
uzinduzi wa mradi huo Septemba 14, 2019.

Baadhi ya wananchi waliofika kushuhudia uzinduzi wa mradi wa maji wa Shilima.

Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame
Mbarawa (Mb) (mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya
viongozi waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa maji Shilima.
*****************************
Mamlaka za maji zinazotumia bei za
kukadiria (flat rates) kote nchini zimepewa miezi mitatu kuhakikisha
zinawafungia dira za maji wateja wao wote ili kila mteja alipe gharama
ya maji kwa kiasi alichotumia.
Waziri wa Maji, Profesa Makame
Mbarawa (Mb) alitoa agizo hilo Septemba 14, 2019 alipokuwa akizindua
mradi wa maji wa Kijiji cha Shilima Kata ya Kikubiji, Wilaya ya Kwimba
Mkoani Mwanza.
Waziri Mbarawa alisema
Serikali imetenga Bilioni moja kusaidia mamlaka za maji ambazo hukadiria
matumizi ya maji wateja wake badala ya kutumia dira ya maji ili kuepuka
kumbebesha mteja mzigo usiyo kuwa wake.
Waziri Mbarawa vilevile
ameziagiza mamlaka za maji za mikoa kuhakikisha zinadhibiti upotevu wa
maji kwani maji mengi yanapotea kabla ya kufika kwa wananchi sambamba na
kuongeza mtandao wa maji ili kuwaunganisha wananchi wengi zaidi.
Akizungumzia mradi wa maji wa
Shilima, Profesa Mbarawa alisema ujenzi wake ni utekelezaji wa Sera ya
Maji pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayoelekeza kuwapatia
huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 85 wakazi wote waishio
vijijini ifikapo mwaka 2020.
Aliongeza kuwa uzinduzi wa
mradi huo ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa maji katika
Vijiji vya Shilima, Mhande na Izizimba.
Alibainisha kwamba mradi wa
maji wa Shilima ulianza kutekelezwa mwaka 2013 na ulitakiwa kukamilika
katika kipindi cha miezi sita. Hata hivyo, kutokana na udhaifu wa
Mkandarasi aliyekuwa anautekeleza pamoja na usimamizi mbovu haukuweza
kukamilika kwa wakati.
Waziri Mbarawa aliwapongeza
wote walioshiriki kwenye ujenzi wa mradi kwa namna mbalimbali na kwa
ushirikiano waliotoa kwa kipindi chote cha ujenzi wake hadi unakamilika
kwa wakati kama alivyokuwa ameelekeza.
Akizungumzia ujenzi wa mradi
huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
Jijini Mwanza (MWAUWASA) ambaye alikuwa msimamizi mkuu wa ujenzi,
Mhandisi Anthony Sanga alisema walizingatia agizo la Waziri Mbarawa na
kwamba mradi huo ulikamilka tarehe 25 Agosti, 2019 kabla ya muda
uliyokuwa umeelekezwa.
Kwa upande wake Meneja wa
RUWASA Wilaya ya Kwimba, Mhandisi Boaz Matundalo alisema kuwa Kijiji cha
Shilima kina wakazi wapatao 7,526 ambapo mradi huu wenye magati 35 una
uwezo wa kuhudumia wakazi 8.750 ikiwa ni wastani wa watu 250 kwa kila
gati.
Waziri Mbarawa tarehe 3 Julai,
2019 akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani Kwimba alitoa ahadi ya
kukamilisha mradi huo kwa kutumia wataalamu wa ndani kwa kuhakikisha
wananchi wa Kijiji cha Shilima wanapata maji katika kipindi cha miezi
miwili, yaani hadi kufikia tarehe 3 Septemba, 2019, ahadi ambayo hata
hivyo ilikamilika tarehe 25 Agosti, 2019 siku tisa kabla ya tarehe ya
makubaliano.
0 comments:
Post a Comment