METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, March 11, 2020

MSIZEMBEE MAFUNZO YA CORONA- RC MWANGELA



Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela (mwenye miwani) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya  Momba Juma Saidi Irando wakifuatilia mafunzo ya utayari wa kupambana na magonjwa ya dharura ya Corona na Ebola.

Wataalamu wa afya Zaidi ya 40 wakifuatilia mafunzo ya utayari wa kupambana na magonjwa ya Dharura ya Corona na Ebola ambapo wameelekezwa kutofanya uzembe wowote.
Wataalamu wa afya Zaidi ya 40 wakifuatilia mafunzo ya utayari wa kupambana na magonjwa ya dharura ya Corona na Ebola ambapo wameelekezwa kutofanya uzembe wowote.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amewataka wataalamu wa afya Zaidi ya 40 kutofanya uzembe katika kusikiliza na kutekeleza mafunzo wanayo patiwa ya utayari wa kupambana na magonjwa ya Dharura ya Corona na Ebola.
Brig. Jen. Mwangela ameyasema hayo mapema leo wakati alipo tembelea eneo la mafunzo ya kukabiliana na Ebola na Corona  yanayo endeshwa kwa muda wa siku tano na Wizara ya Afya kwa Kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Ninasisitiza mafunzo haya ni muhimu sana, Msifanye uzembe wowote katika kusikiliza au hata itakapo tokea mgonjwa japo hatuombei atokee, kwani kwa kufanya uzembe ni hatari na hakuna atakaye tusamehe kwa katika hilo.”, amesisitiza Brig. Jen. Mwangela.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa Mkoa wa Songwe hasa kwakuwa ni lango la SADC na kuna muingiliano Mkubwa wa watu katika Mpaka wa Tunduma, huku kukikwa tayari na Nchi mbili za SADC ambazo kuna washukiwa wa ugonjwa huo.
Brig. Jen. Mwangela amesema Nchi za Kongo na Afrika Kusini tayari kuna washukiwa wa Ugonjwa wa Corona ambapo nchi hizo zina muingiliano Mkubwa na nchi yetu hivyo mafunzo haya yatasaidia kuweka utayari kwa kuzuia ugonjwa huo usiingie nchini au kutoa matibabu endapo atatokea mgonjwa.
Mkufunzi wa Magonjwa ya Dharura Dkt Prosper Mashaka amesema wamewajengea utayari watoa huduma za afya ambao ni madaktari, wauguzi, wateknolojia wa dawa na maabara, watu wanao husika na mazishi ili waweze kukabiliana na ugonjwa wa corona kwakuwa Songwe ni mpakani.
Dkt Mashaka amesema matarajio ya wakufunzi hao ni kuwa timu hiyo itawezesha utoaji wa huduma ya kuzuia au kutibu endapo atatokea mgonjwa wa corona lakini pia waliopata mafunzo watatoa elimu kwa watoa huduma wengine ili kuunda timu kubwa zaidi ya wataalamu wenye ujuzi huo.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt Dunstan Ligasiwa amesema Mkoa wa Songwe umechukua tahadhari zote Muhimu za kukabiliana na ugonjwa Corona na Ebola ikiwa ni pamoja na kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya.
Dkt Ligasiwa amesema halmashauri zote Mkoani Songwe zimeelekezwa kutenga vituo vya Afya vitakavyo shughulika na wagonjwa wa Corona endapo watatokea pia kutenga vyumba maalumu katika kila kituo cha kutolea huduma za Afya kwa ajili ya upimaji endapo atabainika mshukiwa wa ugonjwa huo.
Ameongeza kuwa Mkoa umekusanya vifaa tiba vyote muhimu kwa ajili ya kukabilina na Ugonjwa huo pia mawasiliano na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwa ajili ya kuomba dawa na vifaa tiba vingine muhimu yamefanyika.
Dkt Ligasiwa amesema katika eneo la Mpaka wa Tunduma kila mgeni anayeingia Nchini anapimwa endapo ana ugonjwa wa Corona au Ebola huku mafunzo kwa wataalamu wengine wa afya yakiendelea ili kuwa na timu kubwa ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Naye Mteknolojia wa Dawa kutoka Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe Prosper Alex Mfutakamba amesema mafunzo ya utayari wa kukabiliana na magonjwa ya Corona na Ebola yatawasaidia watoa huduma za Afya kujikinga wao wenyewe kwanza na pia kuweza kutoa huduma kwa wengine kwa usahihi Zaidi.
Muuguzi kutoka Hospitali ya Mwambani Wilaya ya Songwe Sharifa Soroiya amesema baada ya mafunzo hayo watoa huduma hao wako tayari endapo atatokea mgonjwa wa Corona lakini pia wanaiomba serikali kuweka vitendea kazi vyote muhimu ili waweze kutoa huduma hizo kwa usahihi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com