Serikali
ya China imeipatia Tanzania msaada wa Shilingi 29.4bilioni kwa ajili ya
kusaidia sekta ya elimu, utalii wa kijiolojia na kuukarabati Uwanja wa
Taifa Jijini Dar es Salaam.
Makubaliano
ya msaada huo yametiwa saini Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha na Mipango Doto James, kwa niaba ya Serikali, na Kaimu
Balozi wa China hapa nchini, Gou Haodong.
Katibu huyo amesema 22.4bilioni zitatumika kujenga Chuo cha Ufundi Stadi-VETA wilayani Ngara mkoani Kagera.
“Fedha
hizo zitatumika kujenga vyumba 19 vya madarasa, ujenzi wa karakana 9 za
kutolea mafunzo ya elektroniki, ufundi bomba, useremala, ufundi uashi
na upakaji rangi” amesema James
Ameeleza
kwamba kiasi hicho pia kitatumika kujenga majengo ya utawala, mabweni,
nyumba za walimu na miundombinu mingine itakayosaidia kuboresha
mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwenye chuo hicho.
“Tunaamini
kwamba msaada huo utakuwa sehemu ya kusaidia jitihada za Serikali za
kujenga uwezo wa wataalamu wake watakaochangia kukuza sekta ya
uzalishaji na hatimaye kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana
nchini” amesema James
Katibu Mkuu huyo amesema China, itatoa 6.7bilioni kwa ajili ya kuukarabati Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.
“Katika
makubaliano yetu ya msaada wa kuendeleza Uwanja wa Taifa wenye uwezo wa
kuingiza watu 60,000, China itatoa msaada wa kiufundi na vifaa vya
kisasa vya michezo na utaalamu katika usimamizi na ukarabati wa uwanja”
Amefafanua James
Amesema
kiasi kingine cha shilingi 300milioni zitatumika kwa ajili ya kufanya
upembuzi yakinifu wa kuanzishwa kwa aina mpya ya utalii ujulikanao kama
utalii wa kijiolojia “Geopark Project” katika Hifadhi ya Taifa
Ngorongoro, mkoani Arusha.
Alisema
lengo la utafiti huo ni kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika na maajabu
mbalimbali ya kitalii yaliyopo nchini ambayo hayajatumika kikamilifu
kuvutia watalii watakaoongeza pato la Taifa
“Tanzania
ina kila sababu ya kujifunza kutoka katika Hifadhi ya Kimataifa ya
Jiolojia ya Jiaozuo ya Yuntaishan ya China, iliyoanzishwa mwaka 2000
ambayo inaongeza asilimia 37.2 ya watalii kila mwaka na huchangia
asilimia 12 ya pato la Taifa la nchi hiyo”
Tangu
miaka ya 1960 mpaka sasa nchi hiyo imeendelea kuisaidia Serikali
katika ujenzi wa miradi mbalimbali ukiwemo upanuzi wa Chuo cha Polisi
Moshi, Ujenzi wa Maktaba mpya katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
ujenzi wa Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki.
Kwa
upande wake Kaimu Balozi wa China hapa nchini, Gou Haodong, amesema
ujenzi wa Chuo Cha Ufundi Veta huko Ngara mkoani Kagera utaanza haraka
kama ilivyopangwa.
Kuhusu
masuala ya utalii wa kijiolojia katika Hifadhi ya Taifa Ngorongoro,
amesema Tanzania ina bahati ya kuwa na vivutio vingi vya utalii lakini
haijavutia idadi kubwa ya watalii kutoka China kuja kuvitembelea.
“Zaidi
ya watalii milioni moja kutoka China wanatembelea nchi mbalimbali dunia
lakini kati ya hao, Tanzania inapokea watalii 20,000 tu kila mwaka
kutoka China, lakini kwa kuanzisha mradi huu, watalii wengi kutoka China
watavutiwa kuja nchini kufurahia utalii wa miamba, mandhari nzuri,
urithi wa dunia, na kutembelea hifadhi za Taifa” ameongeza Haodong
Akizungumzia
masuala ya uchumi, Balozi huyo amesema hivi sasa China imekuwa
mwekezaji mkubwa zaidi nchini Tanzania kwa kuwekeza kiasi cha Dola za
Marekani 1.77bilioni na kukuza ajira nchini.
Ameitaja
baadhi ya miradi mikubwa iliyowekezwa kuwa ni pamoja na mradi wa
miundombinu ya mtandao (Tanzania ICT broadband backbone), Bomba la gesi
la kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, mradi wa kuboresha miundombinu ya
bandari ,barabara na madaraja.
0 comments:
Post a Comment