Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe.Dkt.Rehema Nchimbi (aliyeketi katikati)akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo maalum kwa wazalishaji wa mafuta ya alizeti pamoja na wauzaji wa bidhaa za vyakula na vipodozi, mara baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa VETA mkoani Singida, wengine walioketi kulia ni Afisa Biashara wa mkoa wa Singida Bw.Daniel Munyi, wa pili kutoka kulia ni Meneja wa Mafunzo na Utafiti kutoka TBS, Bw. Hamisi Sudi, kushoto ni Meneja wa SIDO Singida, Bi Agnes Yeseya na wa pili kutoka kushoto ni Kaimu Meneja wa Mkanda ya Kati - TBS Bw. Sileja Lushibika.
Wazalishaji wa bidhaa mbalimbali mkoani Singida wametakiwa kutambua kuwa suala la viwango ni la kisheria hivyo ni lazima kuthibitisha ubora wa bidhaa ili kumlinda mlaji na kupata uhakika wa soko la bidhaa wanazozizalisha.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt Rehema Nchimbi alipokuwa akifungua mafunzo ya wazalishaji wa bidhaa za vyakula yakiwemo mafuta ya alizeti na wauzaji wa vipodozi na vyakula yaliyofanyika katika ukumbi wa VETA mkoani Singida.
Dkt. Nchimbi alisema suala la ubora wa bidhaa linapaswa kuzingatiwa katika mnyororo wote wa uzalishaji ili mlaji awe salama na kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kutozingatia
viwango.
“Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ndiyo hakikisho la wazalishaji na fursa zinazotengenezwa zitakuwa dhahiri iwapo masuala ya viwango yatazingatiwa, vilevile TBS ni daraja kati ya mzalishaji na soko, hivyo mzalishaji ni lazima kufuata utaratibu,” alisisitiza Dkt. Nchimbi.
Alisema maisha ya binadamu ni chakula hivyo ni muhimu kuzingatia usalama wake, kwani bidhaa
hafifu zinagharimu afya ya walaji na kwamba magonjwa mengi yanatokana na jinsi tunavyoandaa
chakula na tunavyokula, hivyo wazalishaji wanapaswa kuwa waaminifu katika kuzalisha bidhaa yoyote.
Dkt. Nchimbi alisema TBS siyo adui wazalishaji hawapaswi kuichukia na wajenge dhana kuwa TBS ni usama hivyo wazalishaji wa Singida wahakikishe kuwa wanazalisha bidhaa bora wakati wote ili
kudhidhirisha kauli kwamba Singida ni njema wakati wote.
Akizungumzia kwa upande wa TBS, Dkt. Nchimbi alisema Shirika linapaswa kuangalia namna ya
kuongea na wajasiriamali ili kuhakikisha kuwa yale wanayowafundisha wanaelewa kikamilifu.
Mafunzo haya yawe na kipimo ili kujua kama yameeleweka vizuri na kwamba watakaopokea mafunzo ndiyo watakaowapima.
Kwa upande wake Meneja wa Mafunzo na Utafiti kutoka TBS Bw. Hamisi Sudi alisema Shirika
litaendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali ili kuhakikisha kuwa wanazalisha bidhaa kwa kuzingatia viwango.
Alisema Shirika linatambua kuwa wajasiriamali wana mchango mkubwa katika kukuza pato la taifa na kutengeneza ajira kwa wananchi walio wengi hivyo Shirika lina mchakato endelevu wa kutoa elimu kwa jamii hasa wajasiriamali kwakuwa ni mojawapo ya majukumu yake ya kila siku.
Shirika likiwa mkoani Singida limetoa mafunzo kwa wajasiriamali 221 Katika wilaya za Iramba, Singidana Manyoni, ambayo pia yamewashirikisha watendaji wa Halmashauri wakiwemo maafisa Biashara, Maendeleo ya Jamii na Afya pamoja na Maafisa kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).
Pia Shirika linatarajia kutoa mafunzo katika wilaya za Kondoa, Kongwa na ikiwa ni muendelezo wa
mafunzo katika Kanda ya Kati.
0 comments:
Post a Comment