METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, February 24, 2020

WENYEVITI WA MITAA WAASWA KUSIMAMIA MAENDELEO

Wenyeviti wa mamlaka za Serikali za mitaa wametakiwa kuacha kulalamika badala yake  kushirikiana na wataalamu wa ngazi yao kutatua kero za wananchi na kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu ya Kata ya Bugogwa na Shibula akiwa katika ziara yake ya kawaida ya kusikiliza kero, kupokea ushauri na kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo ambapo  amewaasa wenyeviti hao kushirikiana na wataalamu waliopo katika ngazi za mitaa yao kutatua kero za wananchi badala ya kusubiria viongozi wa ngazi za juu kufanya hivyo 

'.. Wewe ndio kiongozi wa mtaa wako, Wataalamu hawa tupo nao kwaajili ya kutusaidia mambo ya kisheria na kitaalamu tu, Tunaowajibu wa kusimamia maendeleo katika maeneo yetu ..' Alisema

Aidha Mhe Dkt Mabula amewataka viongozi hao wa mitaa kutimiza wajibu wao kwa haki na uadilifu mkubwa bila ya kuwabagua wananchi kwa itikadi za vyama, jinsi au hali ya kiuchumi.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela ambae pia ndie mkuu wa idara ya ardhi na mipango miji Ndugu Shukrani Kyando amewataka wenyeviti hao kupitia kamati za upimaji katika mitaa yao kuzichukulia hatua kampuni zote zinazosuasua katika kutekeleza zoezi la urasimishaji makazi kwa kuziita katika vikao vya mitaa na kuzihoji na kama hazitaridhishwa na majibu yanayotolewa washirikiane na ofisi ya mkurugenzi kwa hatua zaidi ikiwemo kuvunja mikataba walioingia hapo awali badala ya kuendelea kulalamika kwa viongozi wa juu.

Nae mhandisi David Christopher kutoka Wakala wa Serikali barabara za mjini na vijijini TARURA amefafanua kuwa wilaya ya Ilemela imetengewa bajeti ya bilioni 1.3 kwa mtandao wa Km 875.85 za barabara zilizopo katika jimbo hilo bajeti ambayo haitoshelezi hivyo kuwaomba viongozi wa Serikali za mitaa kuhamasisha jamii kufungua barabara zilizosahaulika na baadae kuomba msaada TARURA kwa msaada zaidi badala ya kusubiria Serikali peke yake.

Akihitimisha Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM wilaya ya Ilemela Ndugu Hamza kwa niaba ya viongozi wengine wa CCM walioambatana na Mbunge huyo mbali na kumpongeza  kwa kazi kubwa anayoifanya amewaomba wenyeviti wa mitaa kuacha kujitenga na chama kwa kufanya hivyo ni kukwamisha utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com