Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa kongamano la vijana uliofanyika katika eneo la Vwawa wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe na kushirikisha zaidi ya vijana 600, leo tarehe 24 Februari 2020.
Sehemu ya wajumbe walioshiriki katika kongamano la vijana kujadili fursa za kilimo, mifugo na uvuvi toka mikaoa ya Songwe, Mbeya, Rukwa na Katavi, leo tarehe 24 Februari 2020.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na vijana Wilayani Mbozi wakati alipowasili kwa ajili ya ufunguzi wa kongamano la vijana uliofanyika katika eneo la Vwawa wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe na kushirikisha zaidi ya vijana 600, leo tarehe 24 Februari 2020.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na vijana Wilayani Mbozi wakati alipowasili kwa ajili ya ufunguzi wa kongamano la vijana uliofanyika katika eneo la Vwawa wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe na kushirikisha zaidi ya vijana 600, leo tarehe 24 Februari 2020.
Na Revocatus Kassimba, Wizara ya Kilimo-Songwe
Vijana nchini wametakiwa kutumia ardhi nzuri iliyopo kukuza uchumi kupitia shughuli za kilimo kutokana na mazingira wezeshi yaliyowekwa na serikali na wadau.
Kauli hii imetolewa leo mjini Vwawa Songwe na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga wakati akizindua kongamano la kitaifa la kujadili fursa za kilimo kwa vijana
Waziri Hasunga amewaeleza vijana kuwa sekta ya kilimo imetoa ajira kwa watanzania asilimia 58 na imechangia asilimia 30 ya mapato yatokanayo na mauzo ya nje hivyo kuwa na fursa nzuri ya kukuza uchumi.
“ Katika nchi yetu ya Tanzania vijana wapo milioni 16.1 sawa na asilimia 35 ya idadi ya watu wote takribani milioni 55” alisema Hasunga
Waziri Hasunga amesema sekta ya kilimo imechangia asilimia 28.2 ya pato la Taifa ambapo Sekta ndogo ya Kilimo inayojumuisha mazao ya biashara, mazao ya bustani na mazao mengine (nafaka, mikunde na mazao ya mafuta) ilichangia kwa 16.2% ya pato la Taifa kwa mwaka 2018.
Aliongeza kusema kuwa uwepo wa nguvu kazi hii ya vijana ni fursa nzuri ya kutumia ardhi iliyopo kuzalisha mazao ya kilimo,mifugo na uvuvi ili kupata malighafi za viwanda na chakula.
Waziri huyo wa kilimo amewafahamisha vijana kuwa Tanzania ina eneo linalofaa kwa kilimo ambalo ni hekta 44 milioni kati ya hizo hekta milioni 29.4 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji lakini zinazomwagiliwa ni kidogo.
Katika hatua nyingine Waziri Hasunga amewataka vijana kujiunga pamoja na kuanzisha shughuli za kilimo kama uzalishaji mbegu za mazao kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo.
“Mahitaji ya mbegu kwa nchi ni tani 187,000 wakati uzalishaji nchini ni tani 71,000 kwa mwaka hali inayowapa vijana kuwa na fursa ya kuzalisha” alisisitiza Waziri wa Kilimo.
Waziri Hasunga amewata vijana wa Songwe kutumia eneo la Sasanda wilaya ya Mbozi lenye ekari zaidi ya 700 kuzalisha mazao ya kilimo,mifugo na uvuvi kupitia kuunda vikundi vya ushirika.
“Mafuta ya kula yanahitajika sana kwa kiwango cha lita 650,000 wakati uwezo wa kuzalisha nchini ni lita 250,000 tu hivyo vijana zalisheni alizeti na michikichi kwa wingi kutokana na uwepo wa soko la mafuta ” alisema Waziri wa Kilimo.
Kwa upande Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela amewaeleza vijana kuwa mkoa wa wake una ardhi nzuri na yenye rutuba ya kutosha hivyo wajitokeze kuzalisha mazao.
Alisema mkoa wa Songwe katika mwaka 2019 ulishika nafasi ya tatu kitaifa kwa uzalishaji mazao ya chakula nchini kutokana hivo ni fursa kwa vijana kujiajili kwenye kilimo,mifugo na uvuvi.
“Songwe imebarikiwa kuwa na eneo takribani ekari milioni mbili zinazofaa kwa kilimo na kati ya hizo 18,000 zinafaa kwa umwagiliaji” alisema Mkuu wa Mkoa
Kuhusu madai ya ukosefu wa ardhi kwa vijana wa Songwe,Mkuu wa Mkoa huyo alisema “ nasikitika kusikia vijana wana matatizo ya upatikanaji ardhi ya kilimo wakati sijawahi kuwasikia kabla ya hapa” na kuahidi kuwa baada ya kongamano hili vijana wafike ofisini kwake kuweka mikakati mizuri.
Kongamano la vijana kujadili fursa za ajira katika kilimo ni utekelezaji wa Mkakati wa Miaka Mitano wa Taifa kwa Vijana kushiriki katika sekta ya kilimo (National Strategy for Youth Involvement in Agriculture- NSYIA) wa mwaka 2016/17 hadi 2020/21.
Kongamano hilo linaratibiwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau kama Ofisi ya Waziri Mkuu,Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ANSAF, ESRF, SUGECO, FAO, JATU, HEIFER International na ASDP II.
Jumla ya vijana wapatao 680 toka mikoa ya Songwe,Mbeya,Katavi na Rukwa wanashiriki kongamano hili mkoani Songwe.
0 comments:
Post a Comment