METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, February 3, 2020

SERIKALI INA UWEZO WA KUONGEZA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA KILIMO NA IKATOA MCHANGO MKUBWA KWENYE PATO LA TAIFA- WAZIRI HASUNGA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akijibu maswali Bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 3 Februari 2020.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa njia pekee ya kumkomboa mkulima ni kuondokana na kilimo cha kujikimu badala yake kuwekeza katika kilimo cha kibiashara.

Waziri Hasunga ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma jana tarehe 3 Februari 2020 wakati akijibu hoja za wabunge mbalimbali walizozitoa wakati wa bunge la kumi na nane.

Katika kuimarisha sekta ya kilimo tayari wizara ya Kilimo imeanza kutoa elimu kupitia wataalamu mbalimbali kuhusu umuhimu na ulazima wa kusimamia tija katika kilimo pamoja na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Mhe Hasunga amesema kuwa ili kuwa na mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo tayari serikali imeanza kuchukua hatua za makusudi ambazo ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa ndani wa mbegu.

Kwa mujibu wa takwimu alizozitoa Mhe Hasunga amesema kuwa uhitaji wa mbegu nchini ni Tani 187,500 lakini mbegu zilizopatikana katika msimu wa kilimo wa 2019/2020 ni Tani 71,207 ambapo kati ya mbegu hizo Tani 66,033 sawa na asilimia 93% zimezalishwa nchini.

Amesema kuwa mbegu zilizoingizwa kutoka nje ya nchi ni Tani 5,175 sawa na asilimia 7% tu ya mbegu zote zilizopatikana hapa nchini ambapo kiasi hicho kinachoagizwa nje ya nchi ni kiasi kidogo ukilinganisha na kinachozalishwa nchini.

Amesema kuwa matumizi ya mbegu mpya kwa wakulima ni madogo sana ukilinganisha na mahitaji jambo hilo linasababishwa na wakulima kuendelea kutumia mbegu za asili badala ya mbegu mpya na bora. Ambapo amesihi wakulima kuhakikisha kuwa wanaachana na matumizi ya mbegu za asili badala yake kutumia mbegu mpya.

Waziri Hasunga amesema kuwa serikali inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli inaendelea na juhudi zake za kuimarisha uzalishaji wa mbegu ili kuhakikisha kuwa Taifa linakuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha mbegu wakati wa kiangazi kwa kuimarisha skimu za umwagiliaji.

Hasunga amezitaja hatua zingine zinazoendelea kuchukuliwa na serikali kuwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa mbolea kwa wingi zenye bei nafuu na kwa wakati ambapo hata hivyo mahitaji ya mbolea yameongezeka kwa kiasi kikubwa kwa kuwa wakulima wengi wamejitokeza na kuwekeza katika kilimo.

Amesema kuwa mahitaji ya mbolea nchini ni Tani 586, 000 kwa mwaka lakini upatikanaji mpaka kufikia Februari 3, 2020 ni Tani 454,339 ndizo zilizopatikana ambapo kati ya hizo zipo mbolea za kupandia DAP ambazo ni Tani 71,000 mbolea ya kukuzia UREA Tani 100,021.

Amesema kuwa aina zote za mbolea zinapatikana nchini isipokuwa aina moja ya mbolea ya UREA zilizopungua ambapo tayari Tani 43,000 zipo bandarini na Tani 222,000 zimeagizwa na zinatarajiwa kuwasili hivi karibuni.

Waziri Hasunga aliongeza kuwa lengo la kuagiza mbolea hizo nyingi ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na mbolea za kutosha ili ziweze kuuzwa kama nguo zinavyouzwa madukani.

Akihitimisha hoja hizo Waziri Hasunga amesema kuwa sekta ya Kilimo inachangia kwa asilimia 28.7% kwenye Pato la Taifa, inachangia asilimia 65% mpaka asilimia 75% ya ajira mbalimbali ambazo watu wameajiriwa, Inachangia kwa asilimia 66% katika malighafi za viwandani huku ikichangia kwa ailimia 100% katika chakula chote kinachopatikana nchini pamoja na lishe.

Kadhalika amesema sekta ya kilimo inachangia kwa asilimia 30% ya fedha zote za kigeni.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com