METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, July 4, 2023

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA TAWI LA NMB BUHIGWE





Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Benki ya NMB na Benki nyingine nchini kubaini maeneo ya vijijini zaidi ambayo yanakidhi vigezo vya kuwa na matawi ya Benki na kufungua matawi huko ili kurahisisha huduma za kibenki kwa wananchi. 

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 04 Julai 2023 wakati wa ufunguzi wa  tawi la Benki ya NMB Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma. Amewasisitiza kwa kuanza kutumia hata wakala au matawi ya Benki yanayotembea (mobile banking services) ili kuokoa adha kubwa wanayopata wananchi katika kufikia huduma za kibenki  hususani wanaoishi vijijini. 

Makamu wa Rais ameisisitiza Benki ya NMB kuendelea kuboresha ufanisi ili kupunguza gharama za huduma zinazotolewa kwa njia ya kidigitali. Amewataka kuendelea kuwekeza katika Tehema kwani bado gharama za baadhi ya huduma za kidigitali zikiwemo za malipo kwa kutumia kadi (Visa) ni kubwa hali inayokinzana na lengo la Taifa kupunguza matumizi ya fedha taslimu ili kurahisisha malipo, kuchochea matumizi na kuipunguzia Serikali gharama za kutengeneza sarafu. 

Amesema serikali inafurahishwa na usimamizi madhubuti wa Benki ya NMB, ikiwemo kudhibiti madeni chechefu, ambapo kiwango cha madeni chechefu kwa sasa ni asilimia 3 ya madeni yote ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 5 uliowekwa na Benki Kuu ya Tanzania. Pia ameongeza kwamba Benki ya NMB inatengeneza faida na kutoa gawio kila mwaka kwa wanahisa huku kwa upande wa Serikali gawio limekuwa likiongezeka kila mwaka hadi kufikia shilingi bilioni 45.5 ikilinganishwa na shilingi bilioni 30.6 lililotolewa kwa Serikali kwa mwaka 2021. Makamu wa Rais amesema ongezeko hilo la gawio ni kiashiria kizuri cha matunda ya uwekezaji wa kimkakati wa Serikali kwenye taasisi imara zenye utendaji bora na ufanisi kama ilivyo Benki ya NMB. 

Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Buhigwe kuendelea kufanya kazi kwa bidii,kujituma na kwa ufanisi katika sekta zote za kilimo, biashara na utumishi wa umma. Amewataka wakazi wa Buhigwe na watanzania wote kwa ujumla kujenga utamaduni wa kuweka fedha Benki kwani ni salama zaidi badala ya kuweka majumbani. 

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amewaasa wananchi wa Buhigwe kuwakaribisha vema wawekezaji katika wilaya hiyo ili kuweza kutumia vizuri fursa za kukuza uchumi katika eneo hilo. Amesema ni muhimu wananchi wakawavutia wawekezaji hususani wa viwanda kwa kutoa gharama halisi za ardhi kwa maslahi ya wilaya hiyo. Pia ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe kutenga maeneo mahususi kwaajili ya biashara, uwekezaji na taasisi. Amesema sio vema kupima viwanja kwaajili ya makazi pekee bali inapaswa kuweka mkazo pia katika kuangalia uwekezaji na biashara kwa ajili ya baadae. 

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB Filbert Mponzi amesema ufunguzi wa tawi hilo la sita la NMB kwa mkoa wa Kigoma unatarajia kurahisisha huduma za kibenki na Maisha ya wananchi wa Buhigwe na maeneo ya Jirani ambao walitembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo. 

Mponzi ameongeza kwamba tawi hilo litatoa huduma zote muhimu za kibenki ikiwemo utoaji wa ushauri wa masuala ya kifedha, kufungua akaunti, utoaji mikopo, huduma za kuweka na kutoa pesa, bima, kubadilisha fedha za kigeni pamoja na mikopo ya kilimo. Aidha amesema tayari Benki hiyo imeweka shilingi bilioni 1 ili kutoa mikopo katika tawi hilo la Buhigwe ambapo amewasihi wananchi wa wilaya hiyo kuchangamkia fursa hiyo ikiwemo kupata mikopo ya kilimo yenye riba nafuu. 

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB Edwin Mhede amesema Benki hiyo inaendelea kutekeleza jukumu lake la kisheria na kisera la kuisaidia serikali kwa kuchangia juhudi mbalimbali katika kufanya mapinduzi ya sekta ya kifedha hapa nchini kwa lengo la kuchagiza maendeleo ya sekta binafsi ambayo imekusudia kuleta mapinduzi ya Maisha ya watu kiuchumi na kijamii. 

Mhede ameongeza kwamba uwepo wa Benki hiyo wilayani Buhigwe utapelekea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo kwa kuhakikisha kila anayehitaji huduma au suluhisho la kifedha anahudumiwa kwa wakati.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

04 Julai 2023

Kigoma.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com