METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, December 31, 2019

DC KATAMBI AMALIZA CHANGAMOTO YA ABIRIA WALIOKWAMA NA TRENI KUTOKEA KIGOMA



Na.Alex Sonna,Dodoma



KUFUATIA abiria waliokua wakisafiri na Treni inayotoka mkoani Kigoma kwenda Dar es Salaam kukwama jijini Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe Patrobas Katambi ameagiza abiria hao kurudishiwa nauli zao.



DC Katambi ametoa agizo hilo kwa Stesheni Meneja wa Dodoma, Bi Rose Ngauga ikiwa ni pamoja na kuwatafutia abiria hao mabasi yatakayowasafirisha hadi mwisho wa safari yao.



Akizungumza na abiria hao leo katika stesheni ya Dodoma, DC Katambi amesema Treni hiyo imekwama jijini hapa kutokana na mvua inayonyeesha ambapo maji na mchanga zimefunika sehemu ya reli katika eneo la Kilosa mkoani Morogoro.



Amewataka abiria hao kuwa wavumilivu na watulivu kwani changamoto yao ishafika mikono mwa Serikali ambapo inashughulikiwa ili waweze kuendelea na safari.



" Nafahamu wengine mnaenda Hospitali, wengine mnawahi biashara zenu lakini ndugu zangu suala la mvua haliletwi na TRC ni mpango wa Mungu lakini sisi kama Serikali ni jukumu letu kutatua changamoto za wananchi wetu.



Najua mpo abiria 648 hapa, hivyo nimeagiza mrudishiwe nauli zenu na pia nitaita wamiliki wa mabasi hapa waweze kutupa mabasi ya dharura kwa ajili ya kumalizia safari yenu.



Awali Stesheni Meneja, Rose Ngauga amesema tayari wataalamu wa Shirika la Reli wameshafika katika maeneo ambayo yamepata adha hiyo na wanaamini watatua changamoto hiyo ndani ya muda mfupi.



Kwa upande wake mmoja wa abiria Abdallah Sufiani ameishukuru serikali kwa kuingilia suala lao mapema na kulitatua kwa Mhe Mkuu wa Wilaya kuagiza warudishiwe nauli zao pamoja na kuagiza wapatiwe Chakula.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com