METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, December 19, 2019

MHE HASUNGA AANZA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU TATU MKOANI MBEYA, APONGEZA SKIMU ZA UMWAGILIAJI WILAYANI MBARALI

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua mashamba ya mpunga mara baada ya kutembelea shamba la mpunga la Mbarali la Highland Estates Ltd lililopo katika wilaya ya Mbarali, tarehe 19 Disemba 2019 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mapogoro kilichopo kata ya Miyombeni katika wilaya ya Mbarali, tarehe 19 Disemba 2019 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya. 
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua kiwanda cha kuchakata mpunga ili kuongeza thamani wakati alipotembelea shamba la mpunga la Kapunga katika wilaya ya Mbarali, tarehe 19 Disemba 2019 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya. 
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati alipotembelea na kukagua skimu ya Umwagiliaji ya Madibira katika wilaya ya Mbarali, tarehe 19 Disemba 2019 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa shamba la mpunga la Mbarali la Highland Estates Ltd lililopo katika wilaya ya Mbarali baada ya kukagua hali ya upatikanaji wa mbolea, tarehe 19 Disemba 2019 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya. 

Na Mathias Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mbeya

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 19 Disemba 2019 ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya ambapo pamoja na mambo mengine anatembelea na kukagua skimu za umwagiliaji, kuzungumza na wananchi na viongozi wa vyama vya ushirika na kuangalia hali ya msimu wa kilimo ikiwa ni pamoja na kukagua upatikanaji wa Pembejeo.

Ziara hiyo ameianza katika Wilaya ya Mbarali kwa kutembelea skimu ya umwagiliaji ya ushirika (Madibira Amcos ltd) ambapo kuna jumla ya hekta 5634 huku hekta zilizojengwa kwa miundombinu ya Umwagiliaji kwa ajili ya kilimo cha mpunga zikiwa ni 3241.

Mhe Hasunga ameupongeza uongozi wa Skimu hiyo kwa uwezo mkubwa wa uzalishaji wa mpunga ambapo uzalishaji ni wastani wa Tani 7-8 kwa hekta kwa mbegu inayopandikizwa yenye umri wa siku 21 na wastani wa Tani 10-12 kwa hekta kwa mbegu inayopandikizwa yenye umri wa siku 9-15.

Katika ziara hiyo Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ametembelea shamba la mpunga la Mbarali la Highland Estates Ltd ambalo linatumia maji ya mto Mbarali kwa ajili ya kilimo cha Umwagiliaji ambapo kampuni hiyo katika msimu wa mwaka 2018/2019 imelima jumla ya Hekta 1000 na imevuna wastani wa Tani 8000 ambao ni wastani wa Tani 8 kwa Hekta.

Waziri Hasunga amepongeza Uongozi wa shamba hilo kwani mbali na kilimo cha mpunga kampuni pia inafanya shughuli zingine ikiwemo kilimo cha maembe, ufugaji wa kisasa wa Ng'ombe wa maziwa, mbuzi, kondoo na samaki, kilimo cha mikorosho, kilimo cha mahindi pamoja na huduma za usambazaji wa Pembejeo za kilimo kama madawa na mbolea.

Kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima hususani ndege waharibifu wa mpunga maarufu kama kweleakwelea, Mhe Hasunga amesema kuwa atasimamia kwa weledi upatikanaji wa Pembejeo kwa ajili ya kuua ndege hao ili wakulima waweze kunufaika zaidi na kilimo. 

Kadhalika Mhe Hasunga pia ametembelea shamba la mpunga la Kapunga lenye ukubwa wa Hekta 5500 ambapo eneo linalotumika kwa kilimo cha mpunga na lenye miundombinu mizuri ya umwagiliaji likiwa ni Hekta 3500.

Mhe Hasunga amepongeza uongozi wa kampuni hiyo kwa matumizi ya teknolojia ya hali ya juu pamoja na wataalamu waliobobea katika kilimo cha zao la mpunga pamoja na uwepo wa vitendea kazi kama vile mashine ya kupandia mpunga, kunyunyizia dawa, matrekta ya kisasa pamoja na mashine kubwa za kuvunia mpunga.

Pia amepongeza uwepo wa kiwanda kikubwa cha kuongeza thamani ya zao la mpunga, ambapo kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha Tani 100 za mchele kwa siku.

Katika ziara hiyo Waziri Hasunga ameiagiza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuhakikisha kuwa inaboresha Skimu zote za umwagiliaji ili kuongeza mapato ya mpunga kwa wakulima Pamoja na pato la Taifa kwa ujumla.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com