Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akipongezana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa mpango wa Taifa wa Kuzuia na
Kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza katika Uwanja wa Jamuhuri jijini
Dodoma leo Novemba 14/2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akizindua mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza
katika Uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma leo. Novemba 14/2019 . Wengine
kutoka kulia, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt.
Teguest Mengtsu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu, Waziri mkuu mstaafu wa Tanzania, John Malecela na
Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akiwaaga wananchi baada ya kuzindua mpango wa Taifa wa Kuzuia na
Kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza katika Uwanja wa Jamuhuri jijini
Dodoma leo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akiteta jambo na Waziri mkuu mstaafu wa Tanzania, John Malecela baada ya
uzinduzi wa mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa
yasiyoambukiza katika Uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma leo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya Tanzania
Bwana Benedikti Konga. wakati alipotembelea maonyesho ya uzinduzi wa
mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza katika
Uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma leo Novemba 14,2019.
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
…………………
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amesema kuanzia tarehe 17 – 23 Novemba, 2019 litaanza zoezi la
kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo ametoa onyo kwa yeyote
atakayevuruga zoezi hilo kuwa atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Vikundi vya ulinzi wa jadi au
vya ulinzi binafsi au vya mashabiki wa vyama vya siasa havitaruhusiwa
kutumika kwenye maeneo ya mikutano ya kampeni au maeneo ya uchaguzi.”
Waziri Mkuu ametoa onyo hilo
leo (Alhamisi, Novemba 14, 2019)alipozindua Wiki ya Kuzuia na Kudhibiti
Magonjwa Yasioambukiza sambamba na Mpango wa Taifa wa Kuzuia na
Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza
Waziri Mkuu amesema kuwa
vyombo vya Ulinzi na Usalama hususan Jeshi la Polisi, Mgambo wenye sare
na Maafisa wanaosimamia ulinzi vitatumika kuhakikisha kunakuwepo na
utulivu wakati wa kampeni na uchaguzi.
Kadhalika,Waziri Mkuu ametumia
fursa hiyo kuendelea kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya
kupiga kura na Serikali imejipanga vya kutosha kuhakikisha zoezi hilo
linafanyika kwa ufanisi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
amewataka wananchi kuchukua hatua stahiki za kujikinga na magonjwa
yasiyoambukiza ikiwa ni pamoja na kubadili tabia na mwenendo wao wa
ulaji wa vyakula kwa kuongeza ulaji wa mbogamboga, matunda.
Waziri Mkuu amesema kila mtu ana
wajibu wa kudhibiti matumizi ya vilevi kama sigara na pombe; kuhamasisha
jamii kushiriki mazoezi au shughuli za nguvu; kuzingatia mlo unaofaa
hasa kwa kuondoa au kupunguza chumvi, sukari na mafuta. “Tujipange
kukabiliana na madhara mengine yatokanayo na uharibifu wa mazingira na
tabianchi.”
Waziri Mkuu amesema wananchi
wanatakiwa wajenge utamaduni wa kufanya mazoezi angalau dakika 30 mara
tatu kwa wiki. “Katika eneo hili, niweke msisitizo kwa Sekretarieti za
Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendeleza utaratibu wa mazoezi
uliozinduliwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluh Hassan.
“Tuendelee kuhamasisha
kuanzisha na kujiunga kwenye vikundi vya mazoezi ya pamoja ambavyo
husaidia sana kuleta hamasa ya kufanya mazoezi. Tutumie vikundi vya joggingvilivyopo kwenye kata na mitaa au vijiji vyetu ili kupata mwendelezo wa jitihada zao.
Amesema Halmashauri zote
zihakikishe zinatenga na kuyaendeleza maeneo ya wazi katika kila kata au
mitaa ili pamoja na shughuli nyingine wananchi pia watumie maeneo hayo
kwa ajili ya kufanya mazoezi.
“Kwa upande wa wanafunzi
kuanzia sasa kabla ya kuingia darasani wawe wanakimbia mchaka mchaka ili
waweze kujiimarisha kiafya jambo ambalo litawaepusha na magonjwa
yasiyoambukiza.”
Amesema magonjwa
yasiyoambukiza yamekuwa tishio kwenye jamii na ulimwenguni kote, takwimu
za Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mwaka 2016 zinaonesha kuwa
magonjwa hayo yanachangia zaidi ya vifo milioni 41, sawa na asilimia 71
ya vifo vyote milioni 57 vilivyotokea mwaka 2016.
“Taarifa za mwaka 2013 za
Shirika la Maendeleo Duniani (UNDP) zinaonesha kuwa, pamoja na
changamoto hizo za kiafya, magonjwa yasiyoambukiza yanaathiri sana
nyanja nyingine za maisha. Inakadiriwa kuwa katika kipindi cha miaka 20,
kuanzia mwaka 2013 gharama zitokanazo na magonjwa haya zitafikia Dola
za Marekani trilioni 47.”
Waziri Mkuu amesema fedha hizo
zingeweza kutumika kupunguza umaskini kwa watu bilioni 2.5 kwa kipindi
cha miaka 50. Kwa nchi za uchumi wa kati na chini, magonjwa hayo
yatagharimu mataifa hayo Dola za Marekani, trilioni saba katika kipindi
cha 2011 hadi 2025.
Amesema gharama hizo
zinatokana na kuongezeka kwa gharama za huduma za matibabu na upotevu wa
nguvukazi unaosababishwa na maradhi hayo, mfano, makadirio yanaonesha
kuwa gharama za huduma kwa magonjwa yasiyoambukiza itafikia asilimia 75
ya mzigo wote wa bajeti ya afya. Ugonjwa wa kisukari pekee utagharimu
zaidi ya Dola za Marekani bilioni 465 sawa na asilimia 11 ya bajeti yote
ya afya duniani.
Awali,Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema
magonjwa yasiyoambukiza yanajumuisha magonjwa ambayo hayawezi kusambazwa
kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.
Aliyataja magonjwa hayo kuwa
ni pumu, shinikizo la juu la damu, kisukari, saratani, siko seli,
magonjwa ya akili, ajali, magonjwa mengi ya macho, kinywa, masikio, pua
na koo. “Magonjwa haya yamekuwa yakiongezeka duniani kote na kuathiri
nyanja zote za kimaisha.”
Waziri Ummy alisema katika
kipindi cha miaka mitatu iliyopita Tanzania ilishuhudia ongezeko la
idadi ya watu waliopatiwa huduma za magonjwa yasiyoambukiza kutoka
wagonjwa milioni 3.4 kwaka 2016 hadi wagonjwa milioni 4.2 mwaka 2018,
ilkiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 24.
Kwa upande wao, wadau wa
masuala ya afya wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na
Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuongeza kiwango cha bajeti ya dawa
kutoka sh. bilioni 31 hadi sh. bilioni 270.
0 comments:
Post a Comment