Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela ameutaka
uongozi na watendaji wa Wilaya ya Ileje kusimamia ubora katika ujenzi wa
Hospitali ya Ileje ili makosa yaliyojitokeza awali katika ujenzi wa hospitali
hiyo, yasijirudie.
Brig. Jen. (Mst) Mwangela ameyasema hapo mapema jana mara baada ya
kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali hiyo ambapo serikali ilitoa shilingi
bilioni 1.5 mwezi Disemba 2018 huku majengo yaliyo anza kujengwa yakionekana
kuwa na hitilafu za baadhi ya nguzo kupinda na kuwa na nyufa.
“Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri, Madiwani na watendaji wote,
jengo lilioanza kujengwa na kuwa na nyufa na kupinda pinda liwe funzo kwetu
tuhakikishe makosa hayo yasirudie tena katika ujenzi unao endelea sasa, pia
wataalamu wote msimamie taaluma zenu na hatutawavumilia endapo mtafanya
tofauti” amesisitiza Brig. Jen. (Mst) Mwangela.
Ameongeza kuwa Wananchi wameitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli wa kujitolea kwa ajili ya kujiletea
maendeleo hivyo basi watendaji wasiwaangushe.
“Serikali imeleta fedha na wananchi wametoa nguvu zao, halafu sisi
wataalamu tuiharibu kazi, mimi siko tayari kuona kazi inaharibika, kila
mtalaamu atimize wajibu wake, wataalamu wa hospitali wasimamie ujenzi uendane
na mahitaji ya hospitali lakini wahandisi wasimamie ubora wa majengo hayo”,
ameelekeza Brig. Jen. (Mst) Mwangela.
Brig. Jen. (Mst) Mwangela amesema licha ya ujenzi wa Hospitali hiyo
kuchelwa kuanza kwakuwa serikali ilitoa fedha mwezi Disemba 2018, ujenzi huo
ufanyike kwa haraka na kwa viwango ili uwe na ubora unaotakiwa na sio kufanya
haraka bila kuzingatia ubora huku akiahidi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara
Amewataka viongozi wa hospitali waliopewa fedha za ujenzi wa hospitali
hiyo wawe waaminifu huku akiwataka madiwani kusimamia na kuhoji kwa kufuata
taratibu ili waweze kufahamu kila senti ya fedha hizo imetumikaje pia viongozi
hao watoe taarifa kwa madiwani kwani ndio wawakilishi wa wananchi ili kuepusha
malalamiko kutokana na wananchi kutokuwa na taarifa sahihi.
Aidha Brig. Jen. (Mst) Mwangela amesema kuwa imefikia kipindi cha mavuno
hivyo basi madiwani na watendaji wa halmashauri washirikiane katika kukusanya
mapato kwani hali ya ukusanyaji mapato sio nzuri
Amewashauri wananchi wachukue tahadhari ya kutouza sana mazao yao
kwakuwa si mikoa yote imevuna vizuri hiyvo bei ya mazao inaweza kuwa nzuri
zaidi hapo mbeleni hivyo wasifanye haraka kuuza chakula chao na kusisitza kuwa
hilo sio katazo kwa wananchi ushauri wa kuchukua tahadhari.
Brig. Jen. (Mst) Mwangela amewataka Madiwani wasikae na kero
na malalamiko ya wananchi bali wawafikishie Wakuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa ili
kero hivo ziweze kutafutiwa ufumbuzi na pia wawahimize wananchi kujitokeza na
kueleza kero, maoni na malalamiko yao.
0 comments:
Post a Comment