Na Munir Shemweta, WANMM BUKOBA
Makatibu Wakuu wa Tanzania na Uganda wanakutana mjini Bukoba mkoani
Kagera katika mkutano wa mahusiano kujadili changamoto zinazozikabili nchi hizo
ikiwemo Uimarishaji Mpaka wa Kimataifa pamoja na Matumizi endelevu ya
rasilimali za Bonde la mto Kagera..
Mkutano huo wa siku mbili umeanza tarehe 29 April 2019 mjini Bukoba na
kuwakutanisha Makatibu Wakuu wa nchi hizo mbili kutoka Wizara za Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Wizara ya Mifugo, Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya Nishati.
Kabla ya mkutano huo, Wataalamu wa sekta shiriki kutoka Tanzania na
Uganda walikutana na kujadiliana kuhusiana na changamoto zinazozikabili nchi
hizo mbili kwa nia ya kuwasilisha mapendekezo yaliyofikiwa kwa Makatibu Wakuu
wa nchi hizo.
Baadhi ya Changamoto zinazojadiliwa kwenye mkutano huo, ni pamoja
na Uimarishaji na Uthamini wa Mpaka wa Kimataifa wa Tanzania na Uganda, Mpango
kabambe wa utunzaji mto Kagera na Matumizi endelevu ya rasilimali kati ya
Tanzania na Uganda katika Bonde la Mto Kagera.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Faraja Mnyepe
alisema mkutano huo ni mfululizo wa mikutano kati ya nchi hizo mbili wenye
lengo la kutatua changamoto zinazozikabili nchi hizo kwa nia ya kuleta
maendeleo.
Alisema, pamoja na kuwepo changamoto kadhaa lakini Tanzania na Uganda
zinaendelea kufurahia mahusiano mazuri yaliyopo kwa kukutana na kujadiliana
masuala mbalimbali yenye lengo la kuleta manufaa kwa nchi na watu wake.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Profesa Faustin Kamuzora
aliuzungumzia mkutano huo kama njia ya kuzifanya nchi husika kufanya kazi
pamoja na kuzidisha ushirikiano wenye nia ya kuleta maendeleo na kusisitiza
kuwa, utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa unapaswa kufanywa kwa wakati.
0 comments:
Post a Comment