METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, May 1, 2019

Biteko akutana na viongozi waandamizi wa wizara na Tume ya madini


Na Issa Mtuwa, Dodoma

Waziri wa madini Doto Biteko amewataka wafanyakazi wa wizara ya madini pamoja na taasisi zake kufanya kazi na kutekeleza majukumu yao kwa wakati ili kufikia malengo ya wizara hiyo.

Ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao chake na viongozi waandamizi wa wizara ya madini na tume ya madini. Katika kikao hicho pamoja na mambo mengine amezungumzia juu utekelezaji wa maagizo anayoyatoa na usimamizi wa utekeleza wa maagizo yake. Ameongeza kuwa anawategemea sana viongozi hao na wafanyakazi wote katika kufanikisha kazi na malengo ya wizara hiyo.

Ametolea mfano wa maagizo aliyowahi kuyatoa ni pamoja na ufutwaji wa leseni zisizo hai ndani ya siku 7 na zingine siku 30 na lile linalo husu mgodi wa North Mara kuhusu utiririshaji wa maji yenye sumu kwenda kwenye makazi ya wananchi ambapo alitoa pia siku 30 kuhakikisha maji hayo yanadhibitiwa.

Amewaambia viongozi hao kuwa akishatoa maagizo, kazi ya kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo ni kazi yao. Amemshukuru na kumpongeza Mwenyekiti wa Tume Prof. Idris Kikula na tume yake kwa kazi nzuri wanayoifanya na ziara zake mikoani zimekuwa na tija.

Biteko amesisitiza kuwa anatambua mchango wa watumishi wote wa wizara yake hivyo amewaomba kuongeza bidii  na kuongeza umakini katika utekelezaji wa majukumu yao huku wakizingatia weledi na uadilifu.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila na Makamishna. Kwa upande wa tume ya madini waliohudhuria ni pamoja na Mwenyekiti wa Tume Prof. Kikula, Mtendaji mkuu wa tume ya madini Prof. Shukrani Manya, Mkurugenzi wa Leseni Mhandisi Yahya Samamba, Mkurugenzi wa Biashara Dkt. Venance Bahati.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com