WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa,
akisalimiana na Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi
Atashasta Nditiye (kushoto) na mbunge wa Viti Maalum, Oliver Semguruka
Bungeni jijini Dodoma leo Novemba 14.2019
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, akijibu mwaswali ya Wabunge leo Novemba 14.2019 katika kipindi cha maswali ya Papo kwa papo
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
…………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema zoezi la usambazaji wa huduma ya nishati ya umeme linaloendelea
kufanyika nchini hususan kwenye maeneo ya vijiji kupitia Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) ni endelevu.
”Mheshimiwa Rais wetu Dkt John
Pombe Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inawaka umeme
ifikapo 2021. Kazi hiyo inaendelea vizuri kwa usimamizi wa Waziri wa
Nishati, Dkt Medard Kalemani.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Alhamisi, Novemba 14, 2019) katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu
Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Bukoba
Vijijini, Jasson Rweikiza.
Mbunge huyo alitaka kupata kauli
ya Serikali kuhusu vijiji ambavyo bado vitakuwa havijaunganishiwa umeme
hadi 2021 ambao ni muda wa ukomo wa miradi ya REA.
Waziri Mkuu amesema hakuna kijiji
kitakachokosa kuunganishiwa huduma hiyo na ili kuhakikisha inawafikia
wananchi wote gharama za kuunganisha umeme vijijini zimepunguzwa na sasa
ni sh 27,000 tu.
Amesema mbali na kupunguzwa kwa
gharama za kuunganishiwa umeme, pia Serikali imefuta gharama za bidhaa
nyingine za kupeleka umeme kwenye maeneo yao ikiwemo nguzo na nyaya.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
amesema Serikali imeendelea kutoa vibali vya ajira kwenye sekta za afya,
elimu na kilimo na hivi sasa inatarajia kutoa vibali 16, 000 vya ajira
za walimu na kisha itatoa vya watumishi wa afya.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati
akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi, ambaye alihoji, nini
mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wanapatikana watumishi wa kutosha
kuwahudumia Watanzania.
Amesema mkakati wa kujenga
miundombinu ya kutolea huduma mbalimbali nchini unakwenda sambamba na
kuajiri wataalamu watakao wahudumia wananchi katika maeneo husika.
”Serikali imeanza kutoa vibali vya
ajira katika sekta hizi mbili za afya na elimu, hata kwenye
kilimo. Mwaka jana tuliajiri watumishi 6,000 na sasa tuna kibari ambacho
kitatoka hivi karibuni cha watumishi 16,000 kwa upande wa sekondari na
msingi.”
0 comments:
Post a Comment