![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/PMO_8141-1024x628.jpg)
*Akemea ujenzi mbovu wa kuta, aagiza zibomolewe na kurekebishwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amekagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi na
kusema kwamba hajaridhishwa na baadhi ya majengo.
Amemwagiza Mhandisi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Tengamaso Wilson abomoe kuta zenye
hitilafu na kurekebisha kasoro zilizopo kwenye majengo hayo ikiwemo
kutonyooka kwa kuta za majengo hayo.
Alitoa agizo hilo jana
(Jumatano, Oktoba 16, 2019) wakati akikagua majengo ya hospitali hiyo,
na kumweleza mhandisi huyo kwamba kuta zimepishana unene kwa sababu
hakusimamia kazi yako ipasavyo. “Ukuta huu ni mbovu kwa sababu
hukuwasimamia vizuri mafundi wako. Kuna mahali juu unaona ukuta ni mdogo
na huku chini ni mnene.”
Majengo ambayo Waziri Mkuu
aliyakagua na kuonesha kutoridhishwa nayo ni ya utawala, wagonjwa wa nje
(OPD) na maabara. Majengo mengine yanayojengwa ni jengo la wazazi, la
X-ray, la utoaji dawa na la kufulia nguo.
Alipouliza ni kwa nini
kumetokea tofauti baina ya kuta hizo, Waziri Mkuu alijibiwa kwamba
tatizo ni upigaji wa lipu. “Mhandisi wa Wilaya simamia hili, kagonge
upya kuta za jengo hili na lile. Hatuwezi kuwa na jengo la Serikali la
aina hii. Tukitoa fedha ya Serikali ni lazima mjiridhishe kama
kilichojengwa ndicho sahihi.”
“Tunahitaji majengo yote yawe smart, hata ujenzi wake nao uwe smart. Usikubali kutoa certificate kama kazi haijakamilika. Kama kuna kazi haujaridhika nayo, usikubali certificate
itoke. Zile sentimeta 30 ni lazima zirekebishwe la sivyo, itaonekana
huku uliweka matofali mengi kuliko upande ule,” alisisitiza.
Akiwa hospitalini hapo, Waziri
Mkuu alielezwa kwamba katika awamu ya kwanza, Serikali imetoa sh.
bilioni 1.5 na kuelekeza yajengwe majengo saba ya kipaumbele ambayo ni
jengo la wazazi, la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, la X-ray, la utoaji
dawa, la kufulia nguo na la utawala.
Ujenzi wa hospitali hiyo
unafanyika kwa kutumia njia ya manunuzi inayoitwa ‘Force Account’ ambapo
Halmashauri inanunua vifaa vya ujenzi na kuajiri mafundi wa kujenga
majengo yaliyoelekezwa wakisimamiwa na wataalam wa halmashauri na kamati
mbalimbali.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
amemwagiza mweka hazina wa Halmashauri hiyo, Bw. Frank Chonya
ajiridhishe na kazi za ujenzi zinazofanyika kabla hajaamua kutoa fedha
za malipo.
“Mweka hazina, wakati wote ukiambiwa kuwa certificate
imeletwa ni lazima uende ukakague mradi na kama haujaridhika, sema wazi
kwamba hujaridhika na kazi iliyofanywa,” alisema Waziri Mkuu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri hiyo, Bw. Andrea Chezue alisema kiasi chote kilichotolewa na
Serikali cha sh. bilioni 1.5 kimeshatumika, na kwamba Halmashauri
illitumia zaidi ya sh. milioni 100 ili kusafisha eneo na kulipa fidia
ili wapate eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 56.
“Mchango wa Halmashauri ya
Wilaya kwenye ujenzi wa hospitali hii, mpaka sasa ni kwamba tumelipa sh.
milioni 88.266 zikiwa ni fidia ya eneo la ujenzi na sh. milioni 14.418
zimetumika kusafishia eneo lote,” alisema.
0 comments:
Post a Comment