![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/PICHA-1-4-1024x512.jpg)
Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu(wa pili kulia aliyekaa) akisikiliza jambo kutoka kwa Mkuu wa
Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama( aliyesimama), kushoto aliyekaa ni
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Amour Juma wakati wa kuzindua na
kuwasha umeme katika Kijiji cha Mpiji, Halmashauri ya Wilaya ya
Kibaha,mkoani Pwani.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/PICHA-2-3-1024x512.jpg)
Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu( wa pili kulia) akikata utepe kuashiria kuzindua na kuwasha umeme
katika moja ya nyumba za Kijiji cha Mpiji katika Halmashauri ya Wilaya
ya Kibaha,kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Amour Jumaa, na
wapili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/PICHA-6-1-1024x512.jpg)
Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu( aliyesimama),akizungumza na wakazi wa Misugusugu baada ya kupata
malalamiko kuwa baadhi ya kaya zimerukwa na mradi wa usambazji umeme
vijiji, hata hivyo amewahakikishia wananchi hao kuwa wote watapata
umeme, kulia aliyekaa ni Mbunge wa Kibaha mjini, Silvestry Koka
……………….
Na Zuena Msuya , Pwani
Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu amewaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Nchini(TANESCO)kutoa
taarifa za utekelezaji wa Miradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini kwa
viongozi wa vijiji pamoja na wananchi wa maeneo husika ili wafahamu
hatua zaidi za utekelezaji wa miradi hiyo.
Mgalu alisema hayo kwa nyakati
tofauti, Oktoba 16, 2019 wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuzindua na
kuwasha Umeme katika Kijiji cha Mpiji, Kata Boko katika Halmashauri ya
Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani na kukagua maendeleo ya Mradi wa
Usambazaji Umeme katika vijiji vya Kiluvya, Misugusugu, Mkombozi pamoja
na katika Mtaa wa Mwambisi wilayani humo.
Aidha Mgalu alisema, kuwa TANESCO
wakiweka utaratibu wa kuzungumza na Viongozi wa Vijiji pamoja na
wananchi mara kwa mara juu ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa
mradi husika ,kutaondoa maswali mengi pamoja na wasiwasi walionao
wananchi dhidi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa usambazaji wa
umeme.
“Unajua watanzania ni waelewa
sana,unapompa mtu taarifa ya kile kinachofanyika katika eneo lake kwa
wakati sahihi inamfanya awe na amani na wale waliopewa dhamana ya
kutekeleza jambo husika, pia kuendelea kuiamini serikali katika
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wake, na hii
itawaondolea hofu na maswali mengi wananchi, sasa msipofanya hivyo, wao
watajuaje kinachoendelea katika maeneo yao!? Tanesco waelezeni wananchi
kila hatua inayofikiwa katika kutekeleza miradi ya umeme”, alisisitiza
Mgalu.
Vilevile alitumia ziara hiyo
kuwaeleza watanzania ambao bado hawajafikiwa na miradi ya usambazaji wa
umeme kuwa na subira wakati serikali inaendelea kutekeleza kazi hiyo
kwa awamu, kwa kuwa si jambo jepesi kuwafikia wananchi wote kwa siku
moja.
Aliweka wazi kuwa lengo la
serikali ni kufikisha huduma ya umeme kwa kila mtanzania, na kueleza
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani Vijiji 2018 tu,
ndiyo vilikuwa na umeme, sasa hivi idadi imeongezeka na kufikia zaidi ya
vijiji 8100 na tayari zaidi ya vijiji 6000 vimeunganishwa, lengo ni
kuvifikia vijiji vyote 12,319 nchi nzima ikifikapo mwezi Juni ,2021.
“ Serikali ya Awamu ya Tano
inatekeleza miradi mingi na muhimu katika kila sekta, kuna miradi ya
Afya, Elimu, Barabara, Maji na kadhalika, hii yote inahitaji fedha
nyingi na iwafikie wananchi wote na kwa wakati, serikali yetu ni sikivu
na inatekeleza haya yote kwa kwa wananchi wake, hivyo fedha inayopatika
inagawanywa katika kila sekta ili kutekeleza huduma zote muhimu kwa
awamu kadri fedha inavyopatikana, hivyo wale ambao bado hamjafikiwa
kuweni na subira, lengo ni kuwapatia wananchi wote huduma bora”, alisema
Mgalu.
Mgalu alieleza kuwa,
mkandarasi wa kampuni ya Sengerema amefikia 90% ya utekelezaji wa mradi
wa usambazaji wa umeme katika vijijini vyote vya Wilaya ya Kibaha,kazi
kubwa aliyonayo sasa ni kuwasha vijiji hivyo hadi mwezi Desemba
2019,kisha kuangalia mapungufu yalipo na kuyafanyia kazi, ili ifikapo
mwezi Juni 2020 awe amemaliza mradi huo na kuukamilisha kwa wakati.
Aliendelea kumsihi mkandarasi huyo
kuongeza kasi ya kuwaunganisha wateja ambao tayari wamelepia huduma
hiyo, sambamba na hilo aliwahimiza wananchi kulipia haraka gharama za
kuunganishiwa umeme ambayo ni shilingi 27,000 tu.
Serikali ilitenga zaidi ya
shilingi Bilioni 17, kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji
Umeme Vijijini katika Mkoa wa Pwani, pia iliongeza shilingi Bilioni 14
kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Peri Urban katika Wilaya ya Kibaha
pekee, vilevile kupitia mapato ya ndani ya TANESCO, miradi ya usambazaji
umeme 11 itatekelezwa katika wilaya hiyo kutokana kuwepo kwa mahitaji
makubwa ya umeme katika wilaya hiyo yanayosababishwa na uwepo wa
viwanda.
Aidha katika mazungumzo yake
na wakazi wa Kijiji cha Misugusugu,aliitaka TANESCO kuwafungia Transfoma
inayokidhi mahitaji ya umeme katika kijiji hicho na maeneo
yanayowazunguka ili kuondoa adha ya kukatika umeme katika eneo hilo mara
kwa mara ambayo inasababishwa na kulemewa kwa transfoma iliyopo.
Hata hivyo aliwaagiza watendaji wa
TANESCO kufanya uchunguzi upya kubaini kaya za maeneo ya kijiji cha
Misugusugu zilizoachwa katika awamu zilizotangulia ili na wao wapate
umeme katika awamu zijazo kwa kuwa zoezi la kusambza umeme vijijini na
kuwaunganisha wateja ni endelevu kwa kuwa kila siku mahitaji ya umeme
yanaongezeka nchini.
0 comments:
Post a Comment