![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/moja.jpg)
Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani akiwasha umeme katika Sekondari ya Shambarai iliyopo katika
Kijiji cha Nakweni wilayani Simanjiro ikiwa ni ishara ya kuwasha rasmi
umeme kwenye kijiji hicho.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/mbili.jpg)
Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani akikata utepe kuashiria kuwasha rasmi umeme katika Kijiji cha
Naepo wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara. Wa Tatu kulia ni Mkuu wa
Wilaya ya Simanjiro, Eng. Zephania Chaula na wa Pili kushoto ni Mbunge
wa Simanjiro, James Ole Millya.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/tatu.jpg)
Mbunge wa Simanjiro, James Ole
Millya akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Nakweni wilayani
Simanjiro, Mkoa wa Manyara mara baada ya Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani (kulia kwa Mbunge) kufika kijijini hapo kukagua kazi ya
usambazaji umeme. Kushoto kwa Mbunge ni Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro,
Eng. Zephania Chaula.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/nne.jpg)
Baadhi ya wananchi katika Kijiji
cha Naepo wilayani Simanjiro wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani (hayupo pichani) aliyefika kijijini hapo kukagua kazi ya
usambazaji umeme na kuwasha rasmi umeme kwenye kijiji hicho.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/tano.jpg)
Baadhi ya miundombinu ya umeme katika Kijiji cha Nakweni wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/sita.jpg)
Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani (katikati) akivishwa vazi maalum la kimasai na kupatiwa fimbo
maalum mara baada ya kufika katika Kijiji cha Naepo wilayani Simanjiro,
Mkoa wa Manyara ili kuwasha rasmi umeme.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2019/10/saba.jpg)
Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani akiagana na wananchi katika Kijiji cha Nakweni wilayani
Simanjiro, Mkoa wa Manyara mara baada ya kuzungumza nao kuhusu kazi ya
usambazaji umeme kwenye Kijiji hicho. Dkt Kalemani pia aliwasha rasmi
umeme kwenye Kijiji husika.
………………
** Atoa agizo kwa viongozi
Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani ameeleza kusikitishwa kwake na suala la Taasisi za umma na
maeneo yanayotoa huduma za kijamii kutounganishiwa umeme katika baadhi
ya vijiji nchini huku nishati hiyo ikiwa tayari imefika kwenye vijiji
hivyo.
Dkt. Kalemani aliyasema hayo
tarehe 16 Oktoba, 2019, wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara wakati
alipofanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji umeme vijijini na kuwasha
umeme kwenye baadhi ya vijiji akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya
Simanjiro, Eng. Zephania Chaula, Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya
na watendaji kutoka TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Awali, taarifa ya TANESCO katika
Wilaya ya Simanjiro ilieleza kuwa, mkandarasi wa umeme vijijini wilayani
humo, tayari amewasha umeme katika vijiji 11 kati ya 21 alivyopangiwa
lakini ni Taasisi chache za umma zimeunganishwa na umeme.
” Ina maana baadhi ya viongozi wa
Vijiji na Halmashauri hawalipii umeme ili taasisi za umma na maeneo
yanayotoa huduma za kijamii kama visima vya maji yaunganishiwe umeme,
itabidi ifike mahala tuulizane na viongozi hawa kwa nini hawalipii umeme
kwenye Taasisi zao.” alisema Dkt Kalemani.
Kutokana na hilo, Dkt Kalemani
aliendelea kuwasisitiza viongozi hao kote nchini, kutenga fedha za
kuunganisha umeme kwenye taasisi hizo ili umeme huo uweze kuleta tija
kwa jamii.
Kuhusu usambazaji umeme wilayani
Simanjiro, Dkt Kalemani alisema kuwa, Wilaya hiyo ina vijiji 56 na
tayari vijiji 39 vimesambaziwa umeme ambapo aliagiza kuwa, ifikapo mwezi
Disemba mwaka huu, vijiji vyote vilivyosalia viwe vimesambaziwa umeme.
Aidha, akiwa wilayani humo, Dkt
Kalemani aliwasha umeme katika Kijiji cha Naepo na Nakweni ambapo
aliagiza kuwa vitongoji vya Vijiji hivyo ambavyo havina umeme,
visambaziwe umeme.
Kwa upande wake, Mbunge wa
Simanjiro, James Ole Millya, alimshukuru Rais, Dkt John Pombe Magufuli
kwa kazi inayofanyika ya usambazaji umeme vijijini na kueleza kuwa
juhudi hizo zimepelekea umeme kusambaa katika maeneo mbalimbali nchini
Aidha, alimshukuru Waziri wa
Nishati, Dkt Medard Kalemani kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya
umeme vijijini bila kubagua maeneo na kueleza kuwa Wilaya hiyo
imefaidika na miradi ya umeme vijijini kwani takriban asilimia 70 ya
vijiji wilayani humo, tayari vina nishati ya umeme.
0 comments:
Post a Comment