METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, November 26, 2019

UKEREWE YAJIPANGA KUKABILIANA NA USAFIRISHAJI HARAMU WA WATOTO

Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cornel  Lucas Boniphace Magembe
Mratibu wa mradi wa kupinga biashara haramu ya usafirishaji watoto wilayani Ukerewe Amos Juma
Mkurugenzi wa Kiwohede Bi Justa Mwaituka
.................
Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza Cornel Lucas Boniphace Magembe amewataka Madiwani,  Watendaji wa kata,  Maafisa elimu,  Maafisa ustawi,  Jeshi la Polisi, mashirika yasiyo ya Kiserikali na jamii kwa ujumla kushirikiana pamoja katika kupinga biashara haramu ya usafirishaji  watoto. 

Mkuu Huyo ametoa rai hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kujadili namna ya kupambana na biashara hiyo wilayani humo ulioandaliwa na shirika la Kiwohede.

Amesema tatizo la biashara haramu ya usafirishaji wa watoto katika wilaya hiyo ni ukubwa sana huku baadhi yao wakisafirishwa nje ya wilaya ingawa pia wapo wanaosafirishwa ndani ya wilaya hiyo wakipelekwa katika maeneo ya kambi za uvuvi wakifanyishwa kazi za uvuvi,  kuanika dagaa,  na wengine wakifanyishwa kazi za kutoa samaki kwenye nyavu. 

“watoto wengi wamekuwa wakiachishwa masomo yao ili kwenda kufanya shughuli hizo sasa niwatake wote waliohudhuria mkutano huu kushirikiana kwa pamoja na sisi Kama serikali tuko bega kwa bega nanyi Kiwohede katika vita hii na ninaagiza mamlaka husika kushirikiana nanyi hata mtakapoanza kupita kwenye jamii kwa ajili ya kuelimisha” alisema 

Aidha amelipongeza shirika la Kiwohede kwa kuiona wilaya hiyo nao Kama serikali wamekuwa wakitoa maelekezo kwamba biashara hii haramu haipati nafasi na Wala haiwezi kukubalika na watatoa ushirikiano wote katika kuhakikisha watoto wa ukerewe wanaokolewa. 

“Niwapongeze sana kwa kuiona wilaya yetu na nimekuwa nikijiuliza maswali mengi kwanini sisi Ukerewe ndio tutoe wasichana wanaoenda kufanyishwa kazi za ndani,  naamini mradi huu utaleta tija sana hapa kwetu nami nawakaribisha sana kwahiyo fanyeni kazi”

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Bi Justa Mwaituka  amesema wako kwenye mkakati wa kupinga ukatili wa kijinsia wa kitaifa wa mwaka 2017, 2018, 2021 na 2022 na hivyo wanafanyakazi katika eneo ambalo limetengenezewa mikakati ya kitaifa na kushushwa kwenye ngazi ya Halmashauri,  Kata,  kaya mpaka mtu mmoja mmoja. 

Amesema kwa zaidi ya miaka 20 sasa shirika limekuwa likijishughulisha na vijana wenye umri mdogo wa wasichana na pia wameanza kupokea wavulana wakipinga udhalilishaji,  unyonyaji pamoja na ufanyishwaji wa biashara ya ngono na wamekuwa wakifanya shughuli zao kwenye mikoa 10 na wilaya 38 nchini. 

Ameongeza kuwa uwepo wa mradi huo wa kupinga usafirishaji haramu wa watoto katika wilaya ya Ukerewe umekuja kufuatia takwimu walizonazo kila wakifanya utafiti Ukerewe imekuwa ikitajwa mara kwa mara hivyo wameona waje kwenye kiini cha tatizo

Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo wilaya ya Ukerewe Bw Amos Juma amesema kwa miezi mitatu(3) tangu wazindue mradi huo wamefanikiwa kuwaokoa watoto waliokuw wakitumikishwa lakini pia wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari,  vilabu vya wanafunzi pamoja na kushirikiana na Maafisa ustawi wa jamii.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com