METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, November 13, 2019

UBUNIFU CHACHU KUIMARISHA SEKTA YA USHIRIKA- DKT KAMANI


Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Usirika Dkt. Titus Kamani akiongea na watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Hivi karibuni Jijini Dodoma
Kaimu Mrajis wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akisisitiza jambo wakati wa kikao na watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Jijini Dodoma
Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika wakifuatilia majadiliano wakati wa kikao cha Watumishi na Viongozi wa Tume
Bi. Petronila  Shirima akichangia mada wakati wa kikao cha Watumishi

Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) wamepewa wito kuwa wabunifu katika maeneo yao ya kazi kwa kadri ya shughuli na matakwa ya kazi zao. Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Titus Kamani tarehe 12 Novemba 2019 wakati wa kikao cha watumishi wa Tume, Jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Titus Kamani akiongea katika kikao hicho alieleza vipaumbele mahususi katika Sekta ya Ushirika ni pamoja na kubadili Ushirika kuwa katika mlengo wa kibiashara ili mkulima aweze kunufaika zaidi na mazao anayozalisha. Akitaja ushiriki wa Sekta ya Ushirika katika Uchumi wa Viwanda ili kuchangia katika kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya Uchumi wa kati, kuongeza idadi na wigo wa wanaushirika katika sekta ya Ushirika nchini, kuhakikisha uadilifu unaongezeka katika nyanja zote kwa maendeleo ya Sekta ya Ushirika.

“Tuwe sehemu ya mabadiliko chanya, Ushirika unatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu kiuchumi na kijamii. Hivyo, nawaomba watumishi wote wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika katika ngazi zote kutekeleza wajibu na majukumu yenu kwa weledi na kuzingatia vipaumbele muhimu vilivyo mbele yetu ili kuendeza Sekta ya Ushirika,” alisema Dkt. Kamani

Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akiongea na watumishi wa Tume katika kikao hicho, amewataka watumishi kuwa wabunifu na kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia taratibu za utumishi wa Umma. 

 “Kila mmoja katika utekelezaji wa majukumu yake ajaribu kufikiria na kuja na mambo mapya ya kuboresha utekelezaji wa majukumu yake ili kuhakikisha kuwa anatoa huduma bora katika eneo lake. Hivyo, kwa pamoja wote tukiwa watu wa kujiongeza basi Sekta ya Ushirika itazidi kusonga mbele tukikumbuka kwamba huduma bora kwa wananchi ni kipaumbele chetu siku zote,” alisema Dkt. Ndiege

Pamoja na mambo mengine, Kaimu Mrajis alisema Changamoto zinaweza kubadilishwa kuwa fursa endapo wahusika wataamua kwa nia dhabiti ya mabadiliko. Hivyo kwa mtazamo huohuo aliwaomba watumishi wa Tume kuziona changamoto zilizopo katika Sekta hiyo kama fursa ya kufanya mabadiliko, kuweka mifumo mipya na ni nafasi ya kila mtumishi kufanya wajibu wake ili kutekeleza wajibu wa Tume na kutoa huduma bora kwa Wanaushirika na wananchi wote.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wafanyakazi TUGHE tawi la Tume Bw. Mshumba akichangia maoni ya uboreshaji wa utendaji waTume amesema watumishi wameyapokea maelekezo na vipaumbele vilivyoelekezwa na wako tayari kutoa ushirikiano wa dhati katika kuhakikisha Sekta ya Ushirika inaimarika na kuwa endelevu. 

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com