Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Usirika Dkt.
Titus Kamani akiongea na watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Hivi
karibuni Jijini Dodoma
Mkurugenzi wa Utawala na Menejimenti ya
Rasilimali Watu Bw. Athanas Mutwe akiongea na watumishi wa Tume wakati wa Kikao
cha Watumishi hivi karibuni
Kaimu Mrajis wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika
Dkt. Benson Ndiege akisisitiza jambo wakati wa kikao na watumishi wa Tume ya
Maendeleo ya Ushirika, Jijini Dodoma
Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika
wakifuatilia majadiliano wakati wa kikao cha Watumishi na Viongozi wa Tume
Bi. Veneranda Mugoba mtumishi wa Tume akichangia
mada iliyokuwa ikiendelea wakati wa kikao cha Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya
Ushirika Jijini Dodoma
Sekta
ya Ushirika imetajwa kuwa moja ya maeneo muhimu ambayo yana fursa kubwa katika
kushiriki na kuendeleza Uchumi wa Tanzania kupitia maendeleo ya Viwanda ili
kuifikisha nchi katika Uchumi wa kati ifikapo 2025.
Hayo
yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) Dkt. Titus
Kamani wakati wa kikao cha Watumishi wa Tume kilichofanyika Jijini Dodoma hivi
karibuni. Dkt. Kamani alieleza hayo alipokuwa akifafanua vipaumbele vya
kuzingatiwa na Tume katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ni pamoja na
kuhakikisha kuwa ajenda ya viwanda inakuwa ni miongoni mwa masuala muhimu
katika mipango na mikakati ya Taasisi hiyo.
Akizungumza
katika kikao hicho Mwenyekiti huyo alieleza Sekta ya Ushirika katika harakati
za kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye kuendeleza viwanda ni wakati muafaka
sasa kwa kila mtumishi kuangalia namna bora anavyoweza kuja na ubunifu wa namna
bora ya kusaidia kuongeza thamani ya mazao ya wakulima. Viwanda hivyo
vikichakata mazao mbalimbali ya Kilimo, uvuvi, madini na mengine.
Akiongeza
kuwa viwanda hivyo vianzishwe kwa kuzingatia masuala yanayoleta changamoto sana
katika Sekta ya Ushirika akitolea mfano eneo la vifungashio vya mazao eneo
ambalo bado lina uhitaji mkubwa nchini.
“Kila
mmoja wetu ana wajibu wa kuchangia mawazo na utekelezaji wa maeneo ya
kuendeleza, kuanzisha au kuboresha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao. Hivyo
kuongeza mnyororo wa thamani,” alisema Dkt. Kamani
Kaimu
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akiongea na watumishi wa Tume
katika kikao hicho alisema baada ya Vyama 4,413 kukaguliwa na Shirika la
Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika hivi karibuni Tume ichukue fursa hiyo kuendelea
kuboresha taswira ya Sekta ya Ushirika kwa kutumia matokeo ya kaguzi zilizofanyika
kwakuwa kaguzi hutoa picha na muelekeo wa utendaji.
Aidha,
Dkt. Ndiege alisisitiza watumishi kufanya kazi kwa weledi na kutumia taaluma
zao vizuri katika kutimiza wajibu na majukumu yao ili Tume iweze kutekeleza
wajibu na matarajio makubwa ya wananchi na wanaushirika nchini.
Kaimu
Mrajis aliongeza kuwa watumishi waendelee kuwa wabunifu kubuni miradi mipya,
njia bora za utendaji ili huduma za Ushirika ziendelee kuwa bora na kupanua
wigo wa upatikanaji wa huduma za Ushirika katika maeneo mengi zaidi. Mrajis
alishauri watumishi kuendelea kuibua tafiti na mawazo ya kuendeleza na
kuanziasha viwanda vitakavyotumia malighafi kutoka vyama vya Ushirika. Akieleza
kwa kufanya hivyo tutaisaidia Serikali kwa kuongeza ajira na kukuza pato la
Taifa.
“Tuongeze
hamasa na elimu ya Ushirika kwa wale ambao bado hawajajiunga na Vyama vya
Ushirika ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wananufaika na Ushirika ili
kupitia Ushirika wananchi waweze kupata maendeleo kwa urahisi pamoja na
kunufaika na viwanda kupitia Sekta ya
Ushirika. watumishi niwaombe muendelee kuandika mapendekezo mbalimbali
yenye lengo la kutafuta ushirikiano na wadau wa maendeleo ili tukuze na
kuendeleza viwanda vya Ushirika, alisema Dkt. Ndiege ”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na
Menejimenti ya Rasilimali Watu Bw. Athanas Mutwe akiongelea masuala ya kiutumishi katika kikao hicho
alisema Watumishi ni kiungo muhimu sana chenye mchango mkubwa katika kuendeleza
Sekta ya Ushirika na hatimaye kufikia Tanzania ya Viwanda. Bw. Mutwe aliwataka watumishi hao kuendelea
kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma kwa manufaa yao binafsi na Taifa lote.
“Niwaombe
watumishi wote kila mmoja wetu kuzingatie maadili ya utumishi wa Umma, tufanye
kazi tukijua tumepewa dhamana ya kusimamia rasilimali na sekta muhimu ya
Ushirika,” alisema Mutwe
Pamoja
na mambo mengine kikao hicho kilitoa
fursa kwa watumishi wa Tume kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali ya mabadiliko
ya Sheria ya Vyama vya Ushirika nchini
ili kuongeza tija na ufanisi zaidi wa Sekta hiyo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment