Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
MABINGWA watetezi, Tanzania Bara wamefanikiwa kuingia Nusu
Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA
Challenge Wanawake baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya Burundi jioni ya leo
Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Tanzania inafikisha pointi sita baada ya
kushinda mechi zake mbili za mwanzo, nyingine wakiichapa Sudan Kusini
9-0 kuelekea mechi ya mwisho dhidi ya jirani zao, Zanzibar keshokutwa.
Katika mchezo wa leo, mabao ya Kilimanjaro Qeens inayofundishwa
na kocha Bakari Nyundo Shime yamefungwa na Deonisia Daniel Minja mawili
dakika ya 35 na 65, Asha Rashid ‘Mwalala’ dakika ya 72 na Mwahamisi
Omary ‘Gaucho’ dakika ya 86.
Kilimanjaro Queens wanaowania taji la tatu la mfululizo la
michuano hiyo, wataingia kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya jirani zao
Zanzibar wakihitaji kulinda heshima tu.
Katika mchezo wa kwanza, Zanzibar walichapwa 5-0 na Sudan Kusini
hapo hapo Azam Complez na sasa timu yoyote itakayoshinda vizuri mechi
ya mwisho inaweza kuungana na Tanzania Bara katika Nusu Fainali.
Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi za Kundi B kati ya
Kenya na Djibouti kuanzia Saa 8:00 mchana na Uganda na Ethiopia kuanzia
Saa 10:30 jioni.
Kikosi cha Tanzania Bara kilikuwa; Zubeda Mgunda, Julitha
Aminiel, Happyness Hezron, Anastazia Anthony, Deonisia Minja, Stumai
Abdallah/Fatuma Khatib ‘Foe’ dk75, Asha Saada, Asha Shaaban, Amina
Ali/Janet Christopher dk85, Opa Sanga/Diana Lucas dk60 na Mwahamisi
Omary ‘Gaucho’.
Burundi; Jeanine Irakoze, Sandrine Niyonkuru, Gynette Kamwemwe,
Angelique Keza, Zilfa Suzanne, Joelle Bukuru, Charlotte Irankunda, Asha
Dfajari, Esther Nahimana, Aniella Umimana na Sakina Said.
0 comments:
Post a Comment